Mkuu wa Chuo
cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia)
akiangalia moja ya mashine ya kisasa inayotumika kufundishia wanafunzi wa Fani
ya Mizani na Vipimo ndani ya karakana ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam
wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyoongozwa na kauli mbiu
isemayo Vipimo katika dunia inayobadilika.
Mkufunzi wa Mizani
na Vipimo wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi Dar es salaam Ishigita Shunashu
akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosomea fani hiyo leo
jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo duniani.
Baadhi ya
wanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza katika Fani ya Mizani na Vipimo katika
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE). wakiangalia moja mashine ya
kujifunzia masomo hayo iliyofungwa ndani ya Karakana ya Idara ya Vipimo na
Mizani.
Mkufunzi
katika Idara ya Mizani na Vipimo ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam
(CBE) Bi. Rabia Katula akitoa ufafanuzi kuhusu namna wanavyowajengea wanafunzi wa
kuhakiki ubora wa mizani na
kushughulikia matatizo mbalimbali ya mizani.
Mkuu wa Chuo
cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (wa tatu
kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakufunzi wa chuo hicho, Idara
ya Vipimo na Mizani.
Mkuu wa Chuo
cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (wa tatu
kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza
wanaosomea shahada ya mizani na Vipimo.
Na. Aron
Msigwa – Dar es salaam.
Vijana wa
kitanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za mafunzo katika fani ya vipimo na
uendeshaji wa mitambo mbalimbali ili Tanzania mpya ya viwanda iweze kujengwa na
wataalam wazawa kutoka ndani ya nchi.
Kauli hiyo
imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es
salaam Prof. Emanuel Mjema mara baada ya kutembelea maonesho ya mizani na
vipimo kwa vitendo vitendo yaliyoandaliwa na walimu na wanafunzi wa chuo hicho yakihusisha
matumizi ya vifaa na teknolojia ya kisasa ya Mizani na Vipimo.
Amesema Tanzania
inahitaji wataalamu wengi wa vipimo kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo kuanzia
ngazi ya kijiji hadi taifa katika sekta ya Mafuta kwenye makampuni yanayouza
mafuta, mafundi wa pampu za mafuta pia kwenye mitambo ya Gesi na kuongeza kuwa mahitaji
wa wataalam hao kwa sasa ni makubwa kuliko idadi ya wataalam wanaozalishwa kwa
mwaka.
Ameeleza kuwa
sekta ya vipimo duniani kote ni sekta mtambuka kwa kuwa inagusa maeneo
mbalimbali ya maisha ya mwanadamu na huchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa
maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mazingira,teknoloji, Gesi, ubunifu
ambayo yote yana vipimo vyake.
Amesema kuwa CBE
kama chuo kinachofundisha fani ya Mizani na Vipimo nchini kimeungana na taasisi
nyingine za elimu duniani kuadhimisha Siku ya Vipimo duniani ambayo mwaka huu
inaongozwa na kauli mbiu isemayo Vipimo katika ulimwengu unaobadilika kuweka
msisitizo katika ufundishaji unaokwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na
Teknolojia yanayotokea duniani ili
kukidhi mahitaji ya soko.
Amesema Siku hiyo
iliasisiwa mwaka 1870 kwa lengo la kuweka viwango kwenye upimaji wa kutumia Mita
na kuongeza kuwa kuanzia wakati huo siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa duniani
kote.
Amefafanua
kuwa chuo cha CBE kimedhimisha siku hiyo kwa kuwa ni chuo pekee kinachotoa taaluma
ya elimu na watalaam wa Vipimo Afrika Mashariki, Kati na Kusini na kubainisha
kuwa nchini Tanzania taasisi za Serikali ikiwemo Wakala ya Vipimo ambayo
watalaam wake wengi wamefunzwa katika chuo hicho.
Prof. Mjema amesisitiza
kuwa suala la vipimo linagusa maisha ya kila siku ya wananchi kutokana na umuhimu
na kuzitaja sekta kama vile viwanda, madini na uchimbaji wa Mafuta na Gesi haziwezi
kufanikiwa bila kuwa na watalaam vipimo.
Ili kuhakikisha
sekta ya vipimo na Mizani katika chuo hicho inakwenda na mabadiliko yanayotokea duniani chuo hicho
kimekuwa kikibadilisha mbinu za kufundishia wanafunzi na kuandaa mitaala mipya
ili kukidhi mabadiliko hayo.
Aidha, amesema
wao kama watalaam wa vipimo wanasimamia na kutoa ushauri kuhusu masuala
mbalimbali ikiwemo kupiga vita ufungashaji wa mazao kwa kutumia vifungashio
vilivyozidi maarufu kama Lumbesa ambayo vinamnyonya mkulima na kusababisha
apate kiwango kisichoendana fedha na wingi wa mazao yake.
Amefafanua
kuwa katika kukabiliana na changamoto ya
mabadiliko inayotokana na uvumbuzi wa Gesi na Mafuta nchini Tanzania CBE ilianzisha mitaala ya ufundishaji wa
nishati hizo kuwajengea uwezo wanafunzi wanaodahiliwa ili waweze kumiliki
uchumi na kusimamia rasilimali za taifa kwa manufaa ya watanzania.
Prof. Mjema
ameeleza kuwa licha ya vifaa vya kisasa vya kufundishia kupatikana gharama
kubwa,chuo hicho imeendelea kufanya maboresho ya ndani kununua teknolojia mpya
za kisasa zinazotumia mfumo wa digitali ili kuwawezesha wanafunzi kutumia mitambo
mipya.
Amesisitiza
kuwa CBE imeendelea na program mbalimbali za kuwajengea uwezo wakufunzi wake kwa
kuwasomesha ndani na nje ya nchi ili waweze kutoa elimu yenye ubora na viwango
vinavyokubalika.
“Ni kweli
dunia imebadilika na teknolojia imebadilika sana tofauti na miaka ya nyuma, ili
kuendana na mabadiliko haya tumebaresha mbinu zetu za ufundishaji ili wahitimu
wetu waweze kumudu mahitaji ya soko kwa kukidhi viwango vya ndani na nje ya
nchi kwa kuwa suala la vipimo halina mipaka” Amesisitiza Prof. Mjema.
Kwa upande
wake Mkufunzi wa Chuo hicho Bw. Boniface Nyamweru amesema kuwa mafunzo
anayoyatoa kwa wanafunzi wake yanalenga kuwajengea ujuzi na uwezo wa kubuni na
kuanzisha vifaa vyao wenyewe vinavyoweza kutumika kwenye masuala ya Mizani na
Vipimo.
Amesema kuwa
yeye kama mtalaam wa masuala ya Mizani na Vipimo anawafundisha wanafunzi wake namna
ya kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusiana na ufundi kwenye Mizani, kufanya ukaguzi wa Mizani na Mita za
kupimia vimiminika mbalimbali kama mafuta ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mizani
na vipimo nchini inapata wataalam wa kutosha wenye ujuzi.
“Mpaka sasa
tunao wataalam wa ndani wazawa ambao tumewajengea uwezo wa kukabiliana na
changamoto mbalimbali za kiufundi , wengi wao tumewafundisha sisi hapa chuoni
na wana uwezo wa kufanya ukaguzi na uhakiki wa Mizani na vifaa mbalimbali vya
Vipimo katika viwango na ubora unaotakiwa” Amesisitiza.
Kuhusu
matumizi ya huduma ya Mizani na vipimo nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria
huku akifafanua kuwa vipimo vinavyofanyika nchini ikiwemo matumizi ya mita ya
kupimia mafuta (Flow Meter) eneo la bandari ya Dar es salaam vimeruhusiwa
kisheria.
Faudhia Nchila
mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosomea fani ya Mizani na Vipimo
katika chuo hicho amesema kuwa sekta ya Vipimo na Mizani ina mchango mkubwa
katika maendeleo ya nchi kwa kuwa inagusa shughuli za kila siku za maisha ya
wananchi.
Amesema vipimo
vinagusa sekta ya ujenzi, maji, vifaa, teknolojia na shughuli mbalimbali za
ufundi katika maeneo mbalimbali nchini huku akisisitiza kuwa mahitaji ya
wataalam wa vipimo nchini kwa sasa ni makubwa kutokana na mchango wake katika maendeleo
ya nchi na kutoa wito kwa vijana wengi zaidi kujiunga na masomo hayo.
Naye Dunstan
Binamu mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesomea masuala ya sheria katika fani
ya Mizani na Vipimo akieleza mchango wa fani anayoisomea katika maendelea ya
nchi amesema kuwa inalenga kulinda Haki ya mlaji katika kwa kuhakikisha masuala
vipimo na mizani yanafanyika katika
viwango vilivyowekwa.
No comments:
Post a Comment