Tuesday, May 24, 2016

SERIKALI KUZITAMBUA NA KUZIRASIMISHA BANDARI BUBU ZILIZOKIDHI VIGEZO KWA LENGO LA KUKUSANYA KODI

Na Aron Msigwa - MAELEZO

Serikali imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa kuzitambua na kuzirasimisha bandari Bubu zote zilizokidhi vigezo ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara kupitisha bidhaa mbalimbali ili ziweze kuchangia katika Pato la Taifa kulingana na  wingi wa bidhaa zinazopitishwa katika bandari hizo. 

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kujua mkakati wa Serikali katika kudhibiti bidhaa zinazoingizwa nchini na wafanyabiashara wasio waaminifu kupitia bandari bubu hali inayoikosesha  serikali mapato.

Mhe. Ngonyani amekiri kuwepo kwa ongezeko la wafanyabiashara wasio waaminifu wanaotumia bandari hizo katika maeneo mbalimbali nchini hasa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na maeneo ya mipakani ambayo yanaingia moja kwa moja kwenye makazi ya watu akieleza kuwa wengi wa wafanyabiashara wanakwepa kodi na kutafuta urahisi wa kupitisha mizigo yao.

Amesema maeneo hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha upitishaji wa bidhaa zisizokidhi viwango, Silaha na Biashara haramu na kubainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa ndani wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na raia wa kigeni kuagiza na kuingiza bidhaa hizo kupitia bandari hizo kwa lengo la  kukwepa kodi.

Amesisitiza kuwa  Serikali ya Awamu ya tano inalishughulikia kwa nguvu zote suala hilo kupitia watendaji wake wakiwemo wakuu wa mikoa wa maeneo husika ambao hushirikiana na mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti njia na maeneo yote yanayotumiwa na wafanyabiashara hao.

" Kama Serikali tunaendelea kufanya vikao kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na mamlaka zinazohusika kuangalia namna ya kurasimisha bandari bubu zilizobaki ili tuweze kukusanya mapato ya Serikali yaliyokuwa yakipotea kutokana na wingi wa mizigo inayopitishwa" Amesema Mhandisi Ngonyani.

Amefafanua kuwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2015 na mwezi Januari,  2016, doria zilizofanyika katika maeneo yanayotumiwa na wafanyabishara hao zilifanikisha kukamatwa kwa wafanyabiashara 98 ambao wote walichukuliwa hatua za kisheria ikiwem mali zao kutaifishwa pamoja na  kuwafikisha mahakamani.

Kuhusu bandari bubu zilizotambuliwa na kuzirasimishwa na Serikali katika  Pwani ya Bahari ya Hindi ni  Mbweni ya jijini Dar es salaam, Mlingotini mkoani Pwani, Kisiju na Nyamisati mkoa wa Pwani na Bandari bubu ya Kilambo mkoani Mtwara.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa kurasimisha bandari binafsi umefanyika katika ziwa Victoria mkoani Mwanza na maeneo mengine ambayo serikali inaendelea kuyafanyia kazi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni  amesema kuwa Serikali inaendelea kuvijengengea uwezo vikosi vyake vya ulinzi na usalama kwa kuviongezea vifaa vya kisasa ili viweze kuimarisha doria nchi nzima ili kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjaji wa sheria.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wananchi kukusanya taarifa za kiharifu ili kuwabaini na kuwakamata wafanyabishara wote wanaojihusisha na uagizaji na uingizaji wa bidhaa kupitia bandari bubu  ambaoumekua ukiisababishia serikali ikose mapato.

" Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kukusanya taarifa za kiharifu kutoka kwa wananchi ili kukabiliana na wimbi hili, pia tunaendelea kuviongezea nguvu vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kutimiza majukumu yao ipasavyo" Amesisitiza Mhe.Masauni.

No comments: