Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi na Udhibiti wa Uzalishaji na Biashara ya
Madini, Mhandisi Godfrey Kasekenya Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (TMAA),( aliyesimama), akifafanua jambo katika Kikao
kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa
Justin Ntalikwa (wa kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha
Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral
DM Sudan (hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna
wa Madini, Mhandisi John Shija.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa
(kulia) akikabidhiwa Ngao ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini
India ambayo alikabidhiwa na Admiral DM Sudan (kushoto). Ujumbe
kutoka Chuo hicho ulifika katika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza
masuala ya ukaguzi wa madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa
(katikati) akiwa katika kikao na Ujumbe Chuo cha Ukamanda na Unadhimu
cha nchini India (NDC)ulioongozwa na Admiral DM Sudan (Kulia kwa
Katibu Mkuu). Ujumbe huo ulifika katika Wizara ya Nishati na Madini ili
kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini. Kushoto kwa Katibu Mkuu ni
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
Meneja wa Mipango na Utafiti Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA), Julius Moshi, (aliyesimama), akielezea shughuli za
Wakala huo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Profesa Justin Ntalikwa (katikati) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda
na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan
(hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa
Madini, Mhandisi John Shija.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mazingira na Ukaguzi wa Mazingira
Migodini, Emanuel Sumay Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA),(aliyesimama), akifafanua jambo katika Kikao kilichohudhuriwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (wa
kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu
cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan (hayupo
pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini,
Mhandisi John Shija.
Na Teresia Mhagama
Watendaji kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India
(NDC) wameupongeza Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
kwa umakini wake katika Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za uzalishaji
na Biashara ya Madini nchini, ambazo zimeifanya Serikali kupata mapato
stahiki kutokana na rasilimali hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Chuo hicho
Admiral D. M Sudan, katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara
ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam ambapo Ujumbe huo ulikutana na
watendaji wa Wizara na TMAA wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Ujumbe huo kutoka nchini India uliofika Wizara ya Nishati na Madini ili
kujifunza namna Wakala huo unavyosimamia shughuli za uzalishaji na
biashara ya madini nchini, ulieleza kuwa TMAA inafanya kazi nzuri kwani
imekuwa ni mwangalizi wa madini nchini hasa katika juhudi zake za udhibiti
wa utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi.
Awali, Meneja wa Mipango na Utafiti wa TMAA, Julius Moshi aliueleza
Ujumbe huo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala huo
ikiwemo ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka
kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia ya “vat leaching” katika kuchenjua
marudio ya dhahabu katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Geita.
Alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, jumla ya kilo
1,114.49 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 73.5 zilizalishwa na
Mrabaha wa Shilingi Bilioni 2.9 kulipwa serikalini kutokana na shughuli hizo
za uchenjuaji madini.
“Siyo hivyo tu, TMAA pia tumejikita katika kudhibiti Utoroshaji na Biashara
Haramu ya Madini ambapo kazi hii tunatekeleza kwa kushirikiana na Jeshi
la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege (TAA), Idara ya Madini na Usalama wa Taifa kwa kufanya ukaguzi
kupitia madawati maalum yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Julius
Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro, Mwanza, Songwe (Mbeya) na
Arusha,”,” alisema Moshi.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2015 hadi Januari 2016,
ukaguzi uliofanyika kupitia madawati yaliyopo katika viwanja hivyo vya
ndege, umewezesha kukamatwa kwa watoroshaji wa madini katika matukio
16 yaliyoripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye thamani ya Shilingi
bilioni 3.2.
Aidha Moshi alisema kuwa Wakala huo pia umeweka Wakaguzi katika
migodi yote mikubwa nchini ambapo juhudi hizo zimezaa matunda kwani
Ukaguzi uliofanywa na TMAA kwa kushirikiana na TRA umewezesha
baadhi ya kampuni za uchimbaji madini kuanza kulipa kodi ya mapato
ambapo katika kipindi cha mwaka 2009 hadi Machi 2016, kampuni
mbalimbali zimelipa jumla ya Shilingi bilioni 680.5 kama kodi ya mapato.
Vilevile, alisema kuwa Wakala huo umekuwa ukifanya ukaguzi wa mara
kwa mara wa shughuli za ukarabati na utunzaji wa mazingira katika
maeneo ya migodi mikubwa, ya kati na midogo ambapo Wahusika
wamekuwa wakipewa maelekezo yenye lengo la kuboresha hali ya
mazingira kwenye maeneo yao, suala lililopelekea kuimarika kwa shughuli
za utunzaji wa mazingira nchini katika maeneo ya migodi mikubwa, na
baadhi ya migodi ya kati na midogo nchini.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin
Ntalikwa aliukaribisha Ujumbe huo kutoka nchini India na kukishukuru
Chuo hicho kwa kuamua kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini nchini
kwani suala hilo limepelekea pande zote mbili kujadiliana na kutoa maoni
yatakayoboresha Sekta ya Madini katika nchi za India na Tanzania.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kutoka
nchini India kuwekeza katika uzalishaji umeme nchini kwa kutumia vyanzo
mbalimbali kama gesi asilia na Nishati jadidifu ili kuweza kuwa na umeme
wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment