Thursday, May 12, 2016

Muhimbili Kutoa Tiba Wagonjwa wa Homa Sugu ya Ini.

 Mtaalamu kutoka Marekani, Dk Brian McMahon akizungumza na madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuhusu tiba ya homa sugu ya ini inayosababishwa na virusi vya Hepatitis B. 
  Dk Aaron Haris kutoka Marekani akielezea jinsi mradi huo utakavyowanufaisha Watanzania ambao wameambukizwa virusi vya vya Hepatitis B. 
Madaktari na wauguzi wakimsikiliza Dk McMahon wakati akielezea kuanza kwa mradi wa tiba ya homa ya ini kwa watu mbalimbali. 
 Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Tumbo, Dk John Rwegasha (kushoto) akifuatilia mada iliyowasilishwa na Dk Edwin Masue na Dk Eva Uiso wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine ni Dk McMahon na Dk Haris kutoka Marekani.
Dk Edwin Masue wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akiwasilisha mada kuhusu dalili za homa sugu ya ini inayosababishwa na virusi vya Hepatitis B.
Picha zote na John Stephen, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Na Neema Mwangomo-MNH.
Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH-inatarajia kuanza kampeni ya kupima na kutoa tiba kwa  ugonjwa wa Homa Sugu ya Ini ambao  unasababishwa  na Virusi vya  HEPATITIS B .
 
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Edwin  Masue amesema kundi la ndio limeonekana kuathirika zaidi  kwa kuwa mtoto anapata maambukizi kutoka kwa mzazi  .
 
Kwa mujibu wa Dk. Masue mtoto anapozaliwa lazima apatae chanjo,  na pia mama mjamzito ambaye anagundulika kuwa ana Virusi vya HEPATITIS B  hupatiwa dawa ya  kumkinga mtoto katika miezi mitatu ya mwisho kabla ya kujifungua .
“Tuangalie uwezekano ili watu waelewe tatizo hili mapema , wapime na wawahi kupata matibabu kwani maambukizi makubwa yanatoka kwa mama kwenda mtoto  na kwa wale wanaoanza kutumia dawa za VVU wanatakiwa kupima ugonjwa wa homa ya Ini kwa kuwa virusi vinaingiliana,”  amesema Dk . Masue .

Mkakati wa MHN.
Kwa upande wake Daktari John Rwegasha amesema katika kipindi cha Julai mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  kutaanzishwa mradi wa miaka mitano ambao unalenga kupima na kutibu watu ambao watagundulika kuwa na homa sugu ya ini  na kwamba hata baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi wataendelea kupatiwa matibabu bure.

 “ Kuna muongozo wa tiba wa  Shirika la Afya Duniani-WHO- ambao umetolewa mwaka jana hivyo tunataka kuangalia matumizi ya huo muongozo kwenye nchi zetu za Dunia ya tatu , kuna watu wametusaidia tulikuwa hatuna uwezo wa dawa. Awali tulikuwa tunaazima dawa kwenye mradi wa HIV hivyo kupitia mradi huo tutakuwa na dawa pamoja na vitenganishi vya kimaabara,” amesema Dk Rwegasha.

“Kati  ya watu 100, wanane wanatembea na ugonjwa huo bila kufahamu baada ya miaka 20 mtu anapata matatizo ya ini na kusababisha ini kushindwa kufanya kazi na  tumbo kuvimba   hivyo natumia fursa hii kuwaambia wananchi wajitokeze kupima mapema ili waweze kupatiwa  matibabu,” amesema.

Virusi vinavyoenea:
Kwa mujibu wa watalaam , asilimia kubwa ya Virusi vya HEPATITIS B vipo kwenye damu , mbegu za kiume  , ute wa mwanamke na hedhi ya mwanamke  na kwamba  maambukizi yake hayana tofauti na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Dalili za ugonjwa huo:
-Kichefuchefu
-Kukosa hamu ya kula
-Macho kua ya njano
-Mkojo kuwa wa njano
-Kupata choo chenye rangi ya njano ambayo imepauka
-Mwili mzima kuishiwa nguvu.
Hata hivyo dalili hizo si zote zinaenda pamoja , kuna wengine huwa hawana dalili hizo  kabisa.

No comments: