Monday, May 30, 2016

DKT.SHEIN AENDELEA KUSISITIZA AMANI PEMBA.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
 MAKAMO mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Zanziba Dkt.Ali
Mohamed Shein (Pichani)amewapongeza wanachama na viongozi katika wilaya ya
Micheweni kwa kukiamini na kukiweka madarakani chama hicho katika
Uchaguzi Mkuu wa Marudio mwaka huu.

Dkt.Shein alisema kwamba ushindi uliopatikana katika uchaguzi huo
umetokana na nguvu na nia za dhati za wananchi waliamua kwa pamoja
kuichagua CCM kwa kura nyingi ili iendelee kuongoza dola.

Akizungumza  na mamia ya wafuasi wa CCM wakiwemo Mabalozi,wenyeviti na
Makatibu wa matawi na maskani za Wilaya ya Micheweni Kichamanhuko
katika ukumbi wa Chuo cha Kiislamu Pemba, alisema baada ya kumalizika
kwa uchaguzi mkuu wa marudio kwa sasa CCM inaendelea na utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi wapate
maendeleo endelevu.

Dkt.Shein alisema serikali ya awamu ya saba itendelea kutafuta
ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza ama kupunguza  changamoto mbali mbali
zilizopo katika nyanja za Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa kwa lengo la
kuhakikisha Zanzibar inakuwa miongoni mwa nchi yenye uchumi wa kati.

“ Nawapongeza sana wanachama wenzangu wa CCM mlioniamini na kunipa
tena dhamana ya uongozi nakuahidini kwamba sitowaangusha bali
nitaendelea kuwatumikia kama nilivyowahi kuahidi katika mikutano yangu
ya Kampeni zilizopita.

Pia nakukumbusheni jambo moja ambalo ni muhimu sana na tunatakiwa
kulizingatia ambalo ni kulinda na kutunza amani na utulivu wa nchi
yetu, kwani kufanya hivyo ndiyo siri ya mafanikio yetu.”, alisisitiza
Dkt.Shein na kuongeza kwamba licha ya kuwepo changamoto za kisiasa
katika kisiwa cha Pemba bado wafuasi wa CCM wanatakiwa kuwa
wavumilivu.

Alisema Zanzibar ili iweze kuvuka katika migogoro na vurugu zisizokuwa
za lazima ni lazima iwe na kiongozi wa ngazi ya Urais anayejali utu na
ubinadamu wa watu wengine na mwenye maono na uvumilivu mpana wa
kisiasa na vigezo ambavyo anavyo yeye rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Aidha Dkt. Shein amekerwa na kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na
watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CUF kwa kuwatenga na kuwagomea
wafuasi wa CCM katika shughuli mbali mbali za kijamii kisiwani humo.

Alisema kwamba vitendo vya kuwabagua hadi kufikia hatua ya kuwachomea
nyumba za kuishi havionyeshi sifa mbaya tu bali vinaidhalilisha jamii
nzima ya Zanzibar na Serikali yake na kujenga taswira mbaya katika
nchi zingine duniani.

Akizungumzua vipaumbele vya serikali ya awamu ya saba iliyopo
madarakani kwa sasa ni kuimarisha dhana ya utawala bora, uwajibikaji
na uwazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na uadilifu katika
utekelezaji wa malengo ya serikali.

Alisema katika kuweka mipango na mikakati ya kuelekea Zanzibar kutoka
katika kundi la nchi zinazoendelea na kwenda katika nchi zenye uchumi
wa kati ni lazima serikali kupambana vikali vita vya rushwa na
ubadhilifu wa mali za umma.

Alieleza kwamba baadhi ya ahadi alizotoa katika kampeni za Uchaguzi
zilizopita za kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma wa kima cha
chini alisema ahadi hiyo imeanza kutekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wa ahadi ya posho la shilingi 20,000 kwa wazee wenye  umri
wa kuanzia miaka 70 ambao wamewahi kuwa watumishi wa umma ama
hawakufanya kazi serikalini nalo limeanza kutekelezwa kwa baadhi ya
maeneo ambayo taratibu zake zimekamilika.

Alisema jambo pekee la kulinda hadhi na heshima ya zanzibar ni Amani
na utulivu wa kudumu kwani nchi itastawi kimaendeleo endapo hali hiyo
itatawala nchini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema chama
hicho kima imani kubwa na kasi ya utendaji wa Dkt.Shein na wataendelea
kumuunga mkono ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa miongoni mwa nchi
zilizoimarika kiuchumi katika ukanda wa Afika Mashariki na Kati.

Vuai aliwasihi viongozi mbali mbali waliochaguliwa katika Uchaguzi
Mkuu wa Marudio kuwa wabunifu katika utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi
ya CCM kwa vitendo ili wananchi waendelee kukiunga mkono chama hicho.

Pamoja na hayo, Vuai amewapongeza wanachama wa CCM Pemba kwa ujasiri
wao toka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992,
wameendelea kuwa waaminifu kwa kukiunga chama hicho bila ya woga.

“ Licha ya vikwazo, vitisho na wakati mgumu wa kutengwa na kunyanyaswa
na wapinzani lakini mmeendelea kuwa waaminifu kwa CCM nasi
tunakuahidini kwamba tutakuwa nanyi daima katika kusimamia na kulinda
hadhi ya CCM.”, alifafanua Vuai.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema CCM ni chama kilichotokana na vyama
vikuu vya ukombozi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara hivyo kina
historia na asili ya amani kwa miaka mingi na kinaendelea kusimamia
utu na maisha ya watu kwa misingi ya haki na uadilifu.

Aidha aliwasihi wananchi wa Pemba hasa wafuasi wa CCM kuendelea kuwa
watulivu wenye subira juu ya changamoto za kisiasa wanazokumbana nazo
huku wakisubiri serikali na chama kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa
kutatua changamoto hizo.

No comments: