Thursday, May 19, 2016

DAWASCO kugharamia gharama za uunganishwaji wa maji kwa wateja wake

Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO

Maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya viumbe vyote pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote, ubora wa afya na mazingira kwa ujumla vinategemea kuwepo kwa maji yakutosha na yenye ubora unaotakiwa.

Maji yana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya jamii kwa kuwa hutumika kwa matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha umeme,kupika, kuoga na kufua nguo, katika ujenzi na kusaidia maisha ya viumbe hai, matumizi ya viwandani pamoja na kilimo hivyo usimamizi na utunzaji wake lazima uzingatiwe.

Serikali ina malengo ya kuwapatia maji wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani, Kibaha pamoja na Bagamoyo kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.Hakika aja ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Hii imethibitika kuwa kweli Serikali ya Awamu ya Tano inajali watu wake hasa wa hali ya chini kama Rais John Pombe Magufuli ambavyo hupenda kuwaita wanyonge. Watu wengi wanahitaji kuwa na maji ya bomba lakini uwezo wa kuunganisha ulikuwa mgumu kwani gharama wengi waliiona kuwa ni kubwa sana.

Kwa kulitambua hilo Serikali imeamua kuingia gharama za kuwaunganishia maji wateja wake na wenyewe watalipia kidogo kidogo gharama hizo. Hili ni jambo la kuungwa mkono sana.Hapa tunamsikia mkazi wa Mbweni, Jijini Dar es Salaam, Bi Fatuma Iddi akisema,“Kwa kweli serikali hii imetukumbuka, mimi nilishapoteza matumaini ya kupata maji kwangu kwani sikuwa na uwezo wa kulipa malaki hayo kwa ajili ya kuunganishiwa. Lakini kwa kulipia kwa awamu hilo nitalimudu. Heko Mhe. Rais Magufuli kwa kutujali hasa sisi wanyonge.”

Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Mkoa wa Dar es Saalam zinaeleza kuwa Mkoa unapata maji kutoka katika mito na visima ambapo eneo kubwa la Mji huo linahudumiwa na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA) na kwa maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka kwenye visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watu binafsi.

Aidha, vyanzo vikuu vya maji yanayopatikana katika Mji wa Dar es Salaam ni mitambo ya Ruvu Juu ambao kwa siku unazalisha jumla ya lita milioni 82, Ruvu Chini unazalisha lita milioni 270, Mtoni unazalisha lita milioni 9 na visima virefu 106 ambavyo vinazalisha jumla ya lita milioni 106 kwa siku.Vyanzo vyote hivi huzalisha wastani wa jumla ya lita milioni 371 kwa siku zinazotosheleza asilimia 75 ya mahitaji ya wananchi.Mahitaji ya maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam yamefikia Lita milioni 450 kwa siku yakijumuisha matumizi ya nyumbani, matumizi ya Viwanda, Kilimo, Mifugo, na usafi wa Jiji kwa siku.

Hata hivyo mtandao wa DAWASA unapoteza takribani Lita 128,000 sawa na asilimia 48 kwa siku kutokana na ubovu wa mitambo, uchakavu wa mabomba na matumizi yasiyo halali lakini hali hii inaendelea kudhibitiwa na DAWASA kwa kukarabati miundombinu yake, kuwawekea wateja mita za kupima kiasi cha maji wanayotumia, kuelimisha wananchi na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaopatikana na makosa ya uharibifu wa miundombinu au wizi wa maji, kuongeza matanki ya kuhifadhia maji na kufunga mabomba mapya kwenda maeneo yasiyokuwa na huduma na kuchimba visima virefu.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa maji yanayozalishwa bado hayatoshelezi wakazi wa Mji huu lakini Serikali inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wananchi wake kuondokana na adha hii ya ukosefu wa maji safi na salama.Katika kutekeleza kauli mbiu ya “Hapa kazi tu” ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kuwa ifikapo Juni mwaka huu wateja 400,000 wa Mkoani Dar es Salaam wawe wamepatiwa huduma ya maji safi na salama.

Ili kutekeleza agizo hilo, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam imeamua kugharamia uunganishaji wa huduma hiyo kwa wakazi wake ambapo gharama hiyo ilikua ikilipwa na mteja mwenyewe.Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa zoezi hili la kugharamia uunganishaji wa huduma ya maji kwa wateja ni kwa kipindi maalumu cha miezi miwili ambayo ni Mei na Juni ambapo mteja atawajibika kurudisha gharama za uunganishaji kidogo kidogo kila mwezi kwa muda wa miezi kumi na mbili.

“Fursa hii itasaidia hata kwa wananchi wenye kipato cha chini kuweza kuunganishiwa huduma ya maji hivyo nawasihi wananchi wa sehemu husika kujitokeza kwa wingi kupatiwa huduma hii,”alisema Mhandisi Luhemeja.Naye Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo Bi. Everada Balati ametoa rai kwa wananchi kutopuuzia fursa hii kama walivyopuuzia fursa zingine zilizopita kwa kuwa hii ni ya tofauti na anaamini kuwa watu wengi wataweza kuimudu.

“Huduma hii ni ya haraka kwakua haichukui zaidi ya wiki kukamilika,mteja wetu atalipia kulingana na urefu wa sehemu ambayo atafikishiwa huduma hiyo”,alisema Bi. Balati.Bi. Balati amesisitiza kuwa malipo haya hayatakuwa na riba bali mteja atahitajika kulipia gharama za uvutaji wa bomba kama zilivyoainishwa na utaratibu wa malipo utaunganishwa pamoja na bili ya kawaida ya maji inayopelekwa kwa mteja kila mwezi.

Wakazi wa Dar wanashauriwa kuitumia fursa hii nzuri iliyotolewa na DAWASCO ili kuweza kupata huduma ya maji safi kwa urahisi kwa kuwa gharama za uunganishwaji zilikua zikiwashinda wananchi wengi sasa unaunganishiwa na kulipia gharama hizo kidogo kidogo kwa muda wa miezi 12.

Kusema ukweli hii ni fursa kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani na imekuja kipindi muafaka ambapo mtambo mkubwa wa maji wa Bagamoyo unakaribia kuanza rasmi. Hii itaondoa adha ya wakazi wa jiji ambao walilazimika kuamka usiku wa manane ili kupata maji pindi yanapotolewa kwa mgao. Pia itaondoa kero ya kuuziwa maji yasiyo salama ambayo watu wengi wamekuwa wakinunua bila kujua maji hayo yanapatikana wapi na yako safi na salama kiasi gani.

Falsafa au kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu imetafsiriwa kwa vitendo. Hii inajibu kauli mbiu jingine iliyokuwa inasema Maisha Bora kwa kila mtanzania. Haya kwa hakika yatakuwa maisha bora kwa kila mtanzania kwani hakuna ambaye siku hupia bila kutumia maji, iwe mtoto, mkubwa na hata kikongwe anahitaji maji. Ndio maana watu husema ya kuwa Maji ni Uhai.

DAWASCO zoezi hili mlikamilishe kwa wakati kama mnavyosema kuwa litadumu kwa miezi miwili yaani Mei na Juni. Uondoaji wa kero ya maji utasaidia nguvu nyingine na muda uliokuwa unatumika kwa ajili ya kutafuta maji, kutumika kwa shughuli nyingine za uzalishaji mali.

No comments: