Tuesday, May 3, 2016

BASATA YAADHIMISHA SIKU YA MUZIKI WA JAZZ DUNIANI

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaongoza zaidi ya wasanii na wadau wa Sanaa mia moja katika maadhimisho ya siku ya Jazz duniani yaliyofanyika makao makuu ya Baraza hilo yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

Maazimisho hayo ambayo yameazimishwa kwa mara ya kwanza nchini yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Bendi ya muziki wa Jazz huku wataalam na wasanii wakongwe wakiwasilisha mada mbalimbali katika kongamano maalum lililobeba mijadala na hoja mbalimbali kuhusu muziki huo.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Msanii Mkongwe John Kitime alisema kuwa muziki wa jazz una historia ya aina yake duniani hasa katika kujenga diplomasia baina ya mataifa, kuunganisha tamaduni mbalimbali duniani na kushiriki katika ukombozi dhidi ya ukandamizaji na utumwa.

“Sifa kubwa ya muziki huu wa jazz ni namna ulivyopokelewa na kuvuka mipaka katika tamaduni mbalimbali. Ni muziki unaoeleza hisia na matukio ya kweli yanayotokea. Ni aina ya muziki ambao ni urithi wa Dunia kwani una mchango wa pekee” alisema Kitime.

Awali akielezea historia ya muziki huu, Mtaalam wa muziki ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA Kurwijira Mareges alieleza kwamba muziki wa jazz una mizizi yake barani Afrika kabla baadaye kupitia biashara ya utumwa haujasambaa sehemu mbalimbali duniani na kugeuka urithi wa Dunia nzima.

“Watumwa waliotoka Afrika ndiyo waliusambaza muziki wa jazz duniani. Walitoka nao Afrika ukachanganywa na tamaduni za Marekani na baadaye kuzalika jazz tunayoisikia leo. Waliutumia muziki huu katika kujiliwaza, kutetea haki zao, kupinga dhuluma na manyanyaso yaliyotokana na utumwa” alisisitiza Mareges.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bw. Maximilan Chami alisema shirika hilo limetenga siku maalum kwa ajili ya kuadhimisha muziki wa jazz kutokana na mchango wake katika diplomasia ya utamaduni (cultural diplomacy), kutetea usawa miongoni mwa jamii na kuwa alama ya urithi wa tamaduni mbalimbali duniani.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza aliwapongeza wasanii na wadau wa Sanaa kwa kujitokeza kwa wingi katika kuadhimisha siku hiyo huku akisisitiza kwamba BASATA kwa kushirikiana na wadau litaendelea kuadhimisha tukio hilo muhimu kila mwaka na kuahidi kuboresha zaidi.

“Nawapongeza sana kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya. Huu ni mwanzo mzuri. Tunaahidi kuendelea kuadhimisha siku hii kila mwaka na kwa ubora zaidi” alisema Mngereza.

Siku ya muziki wa jazz duniani imekuwa ikiazimishwa kila mwaka tarehe 30 mwezi Aprili kutokana na muziki huu kutambuliwa rasmi na Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama urithi wa dunia na ni kwa mara ya kwanza imeazimishwa nchini Tanzania.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza akizungumza na wadau wa Sanaa kwenye maadhimisho ya Siku ya Muziki wa Jazz duniani yaliyofanyika mapema wiki hii katika Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba jijinI Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Msanii mkongwe John Kitime na Mkuu wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA Kurwijira Mareges.
Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Maximilan Chami akitoa elimu kwa wasanii na wadau wa Sanaa kuhusu maadhimisho ya siku ya Muziki wa Jazz duniani yaliyofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko ofisi za Baraza hilo Ilala Sharif Shamba. Kushoto kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza.
Msanii mkongwe na mchambuzi wa masuala ya Sanaa John Kitime akifafanua juu ya kwa nini bendi nyingi nchini zilitumia jina la jazz wakati akiwasilisha mada kwenye maadhimisho ya siku ya muziki wa Jazz duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Wengine kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Mwakilishi kutoka UNESCO Maximilan Chami na Afisa Habari wa BASATA Aristides Kwizela
Msanii Mkongwe wa muziki wa reggae na mchambuzi wa masuala ya Sanaa Innocent Nganyagwa (Katikati) akiimba sambamba na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza (Kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA Kurwijira Mareges kwenye maadhimisho ya siku ya Muziki wa Jazz duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Msanii na Mtaalam wa Sanaa za Maonesho Kwama Bhalanga akichangia moja ya mada kwenye kongamano lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya muziki wa Jazz duniani.
Sehemu ya wasanii na wadau wa Sanaa waliohudhuria kwenye maadhimisho ya siku ya muziki wa Jazz yaliyofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

No comments: