Tuesday, April 12, 2016

WASHTAKIWA WA TUMBILI WASOTEA DHAMANA

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

HATMA ya dhamana kwa washtakiwa saba wa makosa ya uhujumu uchumi wakiwamo wafanyabiashara raia wa Uholanzi waliokamatwa Machi 23 mwaka huu wakijaribu kusafirisha wanyama hai 61 aina ya Tumbili sasa kujulikana Alhamisi (Aprili 14).

Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji wa mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi ,Aishiel Sumari wakati akitoa uamuzi mdogo juu ya hoja zilizotolewa na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Majura Magafu dhidi ya upande wa Jamhuri kuhusu maombi ya dhamana kwa washtakiwa.
 
Hoja za upande wa utetezi zilitokana na upande wa Jamhuri kuwasilisha mahakamani hapo hati zuio la dhamana kwa washtakiwa wote saba iliyotoka kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

Maombi matatu ya dhamana yaliwasilishwa mahakamani hapo ambayo ni ombi la tatu la raia wa Uholanzi ,Artem Vardanian ,Eduard Vardanyan na Idd Misanya ,ombi nne la ,Nyangabo Musika,Martina Nyakanga na Very Anthon huku ombi la tano lilikuwa ni la aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa idara ya wanyamapori nchini Dkt Charles Mulokozi.

Baada ya maombi hayo kuwasilishwa upande wa utetezi uliridhia kuunganishwa kwa maombi hayo ili kuokoa muda wa mahakama katika kusikiliza shauri hilo baada ya maombi hayo kufanana.Akitoa uamuzi huo Jaji Sumari aliuelekeza upande wa jamhuri kupitia kwa wanasheria wa Serikali Wankyo Simon na Robart Rogart kutumia siku ya leo (Jumanne) kuwasilisha hoja kinzani na kwamba upande wa utetezi utawasilisha maombi yao kesho (Jumatano) baada ya kujibiwa na upande wa pili.

Awali akiwasilisha hoja za upande wa utetezi kwa niaba ya mawakili wenzake ,Wakili Majura Magafu alieleza kuwa na pingamizi juu ya upokelewaji wa hati ya zuio la dhamana kwa washtakiwa hao na kwamba imewasilishwa kabla ya maombi ya dhamana ya washtakiwa hao hayajaunganishwa.

“Ni mtazamo wetu kwamba uwasilishwaji wa hati ya zuio la dhamana ulipaswa kufanyika kabla ya kuunganishwa kwa maombi ya dhamana ,certificate (hati ya dhamana) iliyo mbele ya mahakama sio Proper kuwepo”alieleza Magafu.

Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na mwanasheria wa serikali Wankyo Simon huku akieleza mahakama kuwa upande wa utetezi unajaribu kuipotosha mahakama bila ya kutaja kifungu cha sheria kinachoonesha makosa yaliyopo. Washtakiwa wote saba wamerudishwa rumande hadi Aprili 14 ambapo shauri hilo namba 1/2016 litakapofika mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kwa usikilizwaji .

Washitakiwa katika shauri hilo ni Dk.Charles Mulokozi mkurugenzi msaidizi wa wanayamapori,Nyangabo Musika ambaye ni Ofisa mfawidhi anayehusika na matumizi endelevu ya wanyamapori nchini(Cites),Martina Nyakanga ambye ni kaimu mkuu wa kanda kikosi cha KDU Arusha.

Wengine ni ofisa wanyamapori Arusha,Very Gelard Anthony,Idd Misanya mmiliki wa Kampuni ya Birds Traders ya JIjini Arusha na raia wawili wa uholanzi,Artem Vardanian na Eduard Alik Vadanyan ambaye ni meneja wa Hotel ya North Sea.Raia hao wawili wa Uholanzi walikamatwa machi 23 mwaka huu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) wakijiandaa kusafrisha wanyama hai 61 aina ya tumbili kwenda nchini Armenia wanaodaiwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani 7,320 zaidi ya sh,Milioni 15 .

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza April mosi mwaka huu mbele ya hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya mkoa,Joachim Tiganga na kusomewa mashitaka matatu likiwamo la uhujumu uchumi,kula njama na kusafrisha wanyama hai.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya februari mosi ya machi 22 katika miji ya Arusha,Kilimanjaro na Dar es salaam,washitakiwa walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kusafrisha nyara za serikali .Mawakili wa serikali ,Wankyo Simon na Salim Msemo wakiongozwa na wakili mwandamizi Abdallah Chavula,walidai katika shitaka la pili kuwa,mnamo machi 23 mwaka huu washitakiwa hao walikula njama za kusafrisha wanyama hai .

Pia washitakiwa Artem Vardanian na Eduard Alik Vadanyan ambao ni raia wa kigeni,pia wanashitakiwa kwa kosa la kujihusisha na biashara ya ununuzi na usafrishaji wa wanyama hai kwenda nchini Armenia bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori.
Baadhi ya Washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi ya usafirishaji wa wanyama Hai 61 aina ya Tumbili wakiongozwa na asakari Polisi walipokuwa wakiwasili katika mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Moshi.

Washtakiwa katika kesi ya kusafirisha Tumbili raia wa Uholanzi ,Artem Vardanian na ndugu yake Eduard Vardanyan wakisindikizwa na askari Polisi kuingia mahakamani,Nyuma yao ni mshtakiwa mwingine Idd Misanya . Washtakiwa katika kesi ya kusafirisha Tumbili raia wa Uholanzi ,Artem Vardanian na ndugu yake Eduard Vardanyan wakiwa katika viunga vya mahakama kuu kanda ya Moshi ,kulia ni aliyekua Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt Charles Mulokozi. Washtakiwa katika kesi ya kusafirisha Tumbili wakiwa katika mahabusu ya mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, kutoka kulia ni Eduard Vardanyan ,ArtemVardanian na Idd Misanya.

Watuhumiwa katika kesi ya kusafirisha Tumbili wakiwa katika mahabusu ya mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, wakizungumza jambo na wakili Majura Magafu anyewatetea katika shauri hilo.kutoka kulia aliyeshika nondo ni aliyekua Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Wanamapori Dkt Charles Mulokozi, mfanyabiashara raia wa Uholanzi Artem Vardanian na ndugu yake Eduard Vadanyan.

No comments: