Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar wa kwanza kutoka kulia akiwa katika kikao cha kwanza
na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Ofisi hiyo mara baada ya
kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuiongoza Wizara
hiyo.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim akielezea faraja kwa niaba ya
watendaji wa ofisi hiyo wakati viongozi wa Taasisi za Ofisi hiyo walipokutana
kwa mara ya kwanza na Waziri wao Mh. Mohammed Aboud Mohammed ofisini vuga Mjini
Zanzibar.
Waziri Aboud akiwaagiza wasaidizi
wake kuwasimamia vyema watendaji wao katia kutekeleza majukumu yao
yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na kazi ya utendaji wa Serikali wa kipindi
cha Pili cha Awamu ya Saba.Picha na – OMPR – ZNZ.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi
zilizo chini ya Ofisi hiyo wakajenga tabia ya kukubali kukosolewa na
wafanyakazi walio chini yao zinapotokea hitilafu za kiutendaji wakati wanapotekeleza
majukumu yao ya kazi.
Mh. Aboud alisema hayo katika kikao cha kwanza alipokutana
na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Ofisi hiyo mara baada ya
kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kushika wadhifa wa kuiongoza Wizara hiyo
Kikao kilichofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Wananchi walio wengi wameanza kujenga
matumaini yanayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa kipindi
cha Pili cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na
Dr. Ali Mohammed Shein.Mh. Aboud alieleza kwamba Miaka mitano ijayo itakuwa
ya kasi katika utendaji wa Serikali kuu iliyojikita zaidi kuimarisha uchumi na
kusimamia Maendeleo kwa kutegemea rasilmali
na vianzio vyake vya mapato.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alielezea matumaini yake kutokana na umakini wa Viongozi walioanza
kukabidhiwa majukumu ya kusimamia Taasisi za Umma katika maeneo mbali mbali.
Akizungumzia suala la udhibiti na matumizi sahihi ya
fedha pamoja na Vifaa vya Serikali Mh. Aboud aliwakumbusha Viongozi wa Taasisi
hizo kuhakikisha kwamba suala hilo wanalisimamia kwa nguvu zao zote kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za kazi.
Alisema udhibiti na usimamizi wa matumizi sahihi ya
fedha za Serikali ni kitu cha msingi kinachopaswa kushirikisha watendaji na
viongozi wa ngazi zote za Taasisi na mashirika ya Umma.
Kuhusu mvua za masika zinazoendelea kunyesha sehemu
mbali mbali hapa Nchini Waziri Aboud aliwaagiza Viongozi na Watendaji wa
Kamisheni ya Maafa Zanzibar iliyo chini ya Ofisi hiyo kuendelea kutoa tahadhari
kwa umma ili kusaidia kupunguza hitilafu zinazoweza kusababisha athari kutokana
na mvua hizo.
Alisema athari za maafa zinazotokana na mvua hizo
bado zipo ikiwemo uharibifu wa nyumba zilizojengwa mabondeni na vianzio vya
maji sambamba na kuendelea kwa maradhi ya maambukizo mambo ambayo viongozi na Wananchi
wote wanapaswa kushirikiana katika kukabiliana nayo.
Mapema Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim alisema kwamba watendaji wa Ofisi hiyo
wamepata faraja kubwa kutokana na imani ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Moh’d Shein
kwa kumteuwa tena Mh. Aboud kushika wadhifa huo.
Nd. Ahmad alisema watendaji wanaamini kwamba kasi ya
utendaji kwa Taasisi na mashirikia yaliyo chini ya Ofisi hiyo itaongezeka
kutokana na uhusiano na maingiliano ya muda wa miaka mitanoyaliyopo kati ya
Kiongozi huyo na watendaji hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment