Friday, April 15, 2016

UTAFITI WABAINI WATANZANIA HUTUMIA MUDA MWINGI KWENYE SHUGHULI ZISIZO ZA UZALISHAJI

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ms. Mary Kawar alipohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa serikali, wadau wa takwimu, mashirika ya umma na binafsi pamoja na wananchi walioshiriki katika uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akionyesha vitabu vya ripoti ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee Hall Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na baadhi ya washiriki waliohudhuria katika uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).

Na Veronica Kazimoto

Watu wenye umri wa miaka mitano na zaidi wanatumia asilimia 71 ya muda wao mwingi kufanya shughuli zisizo za uzalishaji kama vile kujihudumia, kulala na starehe.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014/2015 Jijini Dar es Salaam uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Waziri Mhagama alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilikiona kiashiria hiki cha matumizi ya muda ndio maana iliamua kuingia madarakani na kauli mbiu ya HAPA KAZI TU.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha watu wenye uwezo wa kufanyakazi hutumia asilimia 71 ya muda wao kwenye shughuli zisizo za uzalishaji na asilimia 18.5 ya muda hutumika katika shughuli za uzalishaji huku asilimia 10.6 hutumika katika shughuli za nyumbani zisizokuwa na malipo” Amesema Waziri Mhagama.

Amefafanua kuwa nchi haiwezi kupiga hatua katika maendeleo zaidi ya kuhimiza na kuhamasisha nguvu itumike zaidi katika uzalishaji.

Aidha, Mhagama amesema kuwa katika utafiti huo, wanaume walitumia asilimia 23.8 ya muda wao katika uzalishaji ikilinganishwa na wanawake ambao walitumia asilimia 13.5 katika uzalishaji na asilimia 16.5 ya muda wao waliitumia katika shughuli za nyumbani zisizokuwa na malipo huku wanaume wakitumia asilimia 4.4 kwa shughuli za nyumbani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema matokeo ya utafiti huu ni ya muhimu sana katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya wananchi hususani vijana na watoto ambao ni Taifa la kesho. 

“Ninalisemea hili kwa kuwa utafiti huu umeonesha kuwa bado watoto wetu wanatumikishwa katika kazi hatarishi katika maisha yao.” Amesema Dkt.Chuwa.

Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea na juhudi za kukusanya taarifa na kutumia mifumo ya kisasa inayotumia teknolojia kwa lengo la kupunguza gharama za kukusanya takwimu nchini.

Utafiti huu wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi ni wa tano kufanyika tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 1965, 1990/91, 2000/1, 2006/7 na huu wa 2014/15.

No comments: