Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO.
Wanadamu wameumbwa kwa hulka
na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni mwao, jamii wanamoishi,
taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza nia na azma yao ya kuwasiliana.Ili mawasiliano hayo yakamilike
ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.
Ujumbe huo ili uweze
kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha ujumbe huo kwa mlengwa
ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti (redio) na picha (TV) pamoja
na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.Vyombo hivyo vya habari
vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha jamii inapata ujumbe kwa wakati
ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa
na kiutamaduni.
Vyombo vya habari hakika
vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili kufikisha ujumbe unaohusu mambo
mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
Tunapoelekea siku ya maadhimisho
ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3,
maadhimisho hayo mwaka huu yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari
wote duniani wataungana kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza
majukumu yao na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za
ufanisi zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni
mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika suala la uwepo wa vyombo vya
habari.
Ni dhahiri vyombo vya
habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia Serikali kutoa taarifa
mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.Ukilinganisha na nchi
nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya
habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi zaidi katika tasnia hiyo.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye mwenye dhamana ya habari
nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari
nchini.“Tulipofika ni pazuri
ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa ukiangalia idadi ya vyombo
vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa habari wanavyoanadika na wanavyofikisha
ujumbe kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji” alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape
amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa
habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu
yao ya kiundishi wa habari.Kwa mujibu wa takwimu
za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambacho ni chombo kilichoanzishwa
kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji nchini hadi sasa kuna jumla
ya vituo kadhaa vya radio na televisheni vilivyosajiliwa.
Idadi ya vituo vya redio
vilivyosajiliwa nchini hadi sasa ni 123 ambavyo ni sawa na asilimia 43.4 katika
ukanda wa Afrika Mashariki huku miongoni mwa vituo hivyo vinamilikiwa na
makampuni binafsi, taasisi na mashirirka ya dini, jamii na Serikali ambayo inayomiliki
kituo kimoja cha TBC Taifa inayoendeshwa chini ya Shirika la Taifa la
Utangazaji (TBC), nchini Kenya vipo vituo vya redio 118 sawa na asilimia 41.7,
Uganda 37 sawa na asilimia 13.1, Rwanda vituo vitatu sawa na asilimia 1.1 wakati
Burundi ina vituo vya redio viwili ambavyo ni sawa na asilimia 0.7.
Kwa upande wa vituo vya
televisheni, Uganda inaongoza kwa kuwa na vituo vingi ambavyo idadi yake ni 44
sawa na asilimia 53.6, ikifuatiwa na Tanzania yenye vituo 24 sawa na asilimia
29.3, Kenya vituo 10 sawa na asilimia 12.2, Rwanda vituo vitatu ambavyo ni sawa
na asilimia 3.7 na Burundi ikiwa na kituo kimoja cha televisheni ambacho ni sawa
na asilimia 1.2
Kwa kuzingatia maslahi
ya wananchi na wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe, TCRA imekuwa
ikihimiza juu ya ufanisi wa ushindani na uchumi, kulinda maslahi ya walaji,
kulinda uwezo wa fedha na ufanisi wa wagavi.
Pia inahimiza
upatikanaji wa huduma zinazosimamiwa kisheria kwa walaji wakiwemo wenye kipato
cha chini na walaji wa vijijini na wa pembezoni, kukuza mwamko, maarifa na
uelewa wa jamii kuhusu sekta zinazosimamiwa ikiwemo kuzingatia haja ya kulinda
na kuhifadhi mazingira, haki na wajibu wa walaji na wagavi wanaosimamiwa.
Katika kuonesha
Tanzania inavyosimamia uhuru wa vyombo vya habari, TCRA ina jukumu lingine la
kusimamia malalamiko na migogoro inayoweza kujitokeza miongoni mwa wateja wake
wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wananchi na kupatia ufumbuzi changamoto
hizo.
Aidha, hadi Aprili 22,
2016, Tanzania imekuwa ndio nchi inayoongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na idadi
kubwa ya magazeti yaliyosajiliwa ambapo idadi yake ni 881 licha ya magazeti na
majarida mengi kusajiliwa, mengi huchapishwa mara chache na mengine kutokuchapishwa
na kusambazwa baada ya kusajiliwa.
Kwa idadi ya magazeti
nchi za Uganda, Rwanda na Burundi yapo magazeti matano yanayotumika katika nchi
hizo wakati Kenya ina magazeti saba ambayo husomwa na kufikisha ujumbe kwa
walengwa katika mataifa hayo.
Wingi huo wa vyombo vya
habari nchini imekuwa ishara njema ya kujali uhuru wa kuanzishwa kwa vyombo vya
habari kwa makampuni binafsi, taasisi na mashirika ya dini pamoja na jamii
mbalimbali ili kuweza kuwa ndio namna yao ya kupata taarifa.
Katika ulimwengu wa
leo, uhuru wa habari ni suala la msingi na lina umuhimu mkubwa katika
kutekeleza haki za binadamu katika kutafuta, kupata, kupokea na kutoa habari ambazo
ni muhimu kwa nchi katika kujiletea maendeleo endelevu.
Kauli mbiu ya
maadhimisho hayo mwaka huu inawahimiza wanahabari na watu wote kutambua “Kupata
Habari ni Uhuru wa Kimsingi: Hii ni haki yako!” ikilinganishwa na kauli mbiu ya
mwaka uliyopita ambayo ilisema “Achia uwandishi habari ustawi! Kuelekea
upashaji habari bora, usawa wa jinsia na usalama wa vyombo vya habari katika
enzi ya dijitali”.
Kwa mujibu wa taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Aprili 8, 2016 imebainisha kuwa katika maadhimisho ya Siku
ya vyombo vya habari duniani mwaka huu, mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka
Azerbaijan Khadija Ismayilova amechaguliwa kupokea tuzo ya uandishi wa habari
za uchunguzi ijulikanayo “Guillermo Cano” inayotolewa na Shirika hilo.
Tuzo hiyo ina thamani
ya Dola za Kimarekani 25,000, na imepoewa jina hilo kwa heshima ya Guillermo
Cano Isaza, mwandishi wa habari wa Colombia aliyefariki Desemba 17, 1986 akiwa
kazini.Jukumu la kuenzi na
kutoa tuzo ya heshima kwa waandishi wa habari duniani linafadhiliwa na taasisi
ya Cano Foundation kutoka nchini Colombia na Helsingin Sanomat Foundation kutoka
nchini Finland.
Msaidizi wa Mkurugenzi
Mkuu wa Mawasiliano na Habari UNESCO Frank La Rue anasema "Uhuru wa vyombo
vya habari ni muhimu kwa taarifa muhimu na uwazi ni ambao ni mahitaji ya jamii
ya kidemokrasia. Lakini leo tunaona ongezeko la ghasia na vitisho dhidi ya
waandishi ambayo mimi napendekeza nchi zote duniani kuanzisha utaratibu wa
habari na ulinzi kwa ajili ya usalama wa waandishi wa habari"
Moja ya changamoto za
kuweka utaratibu wa usalama wa waandishi wa habari ni idadi ndogo ya mifano ya
taratibu zilizopo ambayo inaweza kuwa somo ili wengine waweze kujifunza
kutokana na taratibu zilizopo.
Masuala muhimu ya kuzingatiwa
wakati wa kuanzisha utaratibu huo ni pamoja na kuwepo kwa makundi matatu ambayo
ni wigo wa utaratibu, ushirikishwaji wa wadau muhimu pamoja na taasisi kubuni na kutathmini hatua ambayo itasaidia kufikia
malengo ya kumlinda mwandishi wa habari.
Akizungumzia maandalizi
ya maadhimisho kitaifa ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari nchini ambayo
yanafanikia jijini Mwanza Mei 2 na 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya maadhimisho hayo Andrew Marawiti amesema kuwa yanaendelea vizuri
kulingana na ratiba ilivyopangwa.
Katika maadhimisho
hayo, Marawiti amesema kuwa Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Othman Chande ambapo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho
hayo mada mbalimbali zitawasilishwa na watoaKuhusu ratiba ya siku mbili za
maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa zitawasilishwa zikiandamana na
majadiliano kwa washiriki wote.
Miongoni mwa washiriki
wanaotarajiwa kuwepo katika maadhimisho hayo ni wadau mbalimbali wa habari
wakiwemo viongozi wa Serikali, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini,
wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi
wa habari na wananchi.
Kulingana na takwimu
zilizopo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Mzee Willie Mbunga amesema kuwa
Tanzania ina vyombo vingi vya habari ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya
nyuma ambapo kulikuwa vyombo vichache vya habari ambavyo ni redio Tanzania Dar
es salaam, Tanganyika Standard, Mambo Leo, Uhuru, Mzalendo na Ngurumo.
Aidha, amesema kuwa changamoto
ya baadhi ya watu kujisahau na kuweka pembeni maadili ya uandishi wa habari ni
suala ambalo si la kufumbiwa macho, ni vema litiliwe maanani ili kukiokoa
kizazi cha sasa na kijacho katika kujenga jamii inayojali na kusimamia maadili
ya taaluma na ya jamii.
Katika upashanaji
habari, dunia sasa imekuwa sawa na kijiji hasa katika kipindi hiki cha sayansi
na teknolojia ambapo mawasiliano ndio imekuwa nguzo ya kila kitu.
Awali makala haya
yameonesha kuwa ujumbe katika jamii ulifikishwa kwa njia ya redio, magazeti na TV,
zaidi ya vyombo hivyo, mitandao ya kijamii kwa sasa imekuwa nguzo mahiri na
vyanzo vikuu vya habari kwa waandishi wa habari na wananchi.
Miongoni mwa mitandao
hiyo ya kijamii ni pamoja na blog ya Serikali, Michuzi, fullshangwe, bayana,
milardayo, mwamba wa habari, businessmagnetblogs, mpekuzi, moh Dewji na
mitandao mingine.
Mwandishi wa habari
Majid Mjengwa ambaye pia ni mwanzilishi na mmiliki wa blog ya mjengwa anasema
“Mitandao ya kijamii imekuwa ni eneo la upashanaji habari linalofanya kazi kama
vyombo vingine vya habari”.
Ili kufikisha ujumbe
kwa jamii, Mjengwa amesema kuwa watu wote wanaofanya kazi katika mitandao ya
kijamii wanapaswa kufuata maadili ya taaluma ya habari pamoja na sheria na
taratibu za nchi husika ili kuondoa mgongano wa maslahi katika kufikisha ujumbe
kwa jamii.
Ni dhahiri haki na
wajibu ni vitu ambavyo haviachani, hivyo ni jukumu la kila mdau wa habari
nchini wakiwemo Serikali, waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na
wananchi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na maadili ya jamii.
Hatua hiyo itasaidia
kuimarisha na kuhakikisha wadau hao wanakuwa sehemu ya kujenga uhuru wa vyombo
vya habari ambavyo vitakuwa chachu ya kujenga taifa imara lenye uchumi bora kwa
manufaa ya Watanzania ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment