Friday, April 22, 2016

MUOGELEAJI WA TANZANIA HILAL HILAL ATWAA MEDALI YA SHABA DUBAI.

 Muogeleaji nyota wa kiume wa Tanzania, Hilal Hilal (wa kwanza kulia) akiwa kwenye jukwaa mara baada ya kupokea medali yake ya Shaba katika mashindano ya Kanda ya Nne ya Cana. 
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinanchoshiriki katika mashindano ya Cana Kanda  ya nne. kutoka kulia ni Amani Doggart, Catherine Mason, Hilal Hilal na Smriti Gokarn.

Na Mwandishi wetu
Muogeleaji wa Tanzania, Hilal Hilal ametwaa medali ya Shaba katika mashindano ya kuogea ya Cana Kanda ya Nne yanayoendelea nchini Mauritius.

Hilal ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa katika mchezo huo, amemaliza katika nafasi ya tatu katika staili ya butterfly kwa kutumia muda wa sekunde 26.70 katika mashindano hayo magumu yaliyoshirikisha nchi za Uganda, Kenya, Rwanda Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudani Kusini na Sudan.

Nafasi ya kwanza ilichukuliwa na muogeleaji kutoka Zambia,  Ralph Goveia  aliyetumia muda wa 25.11 na kupata medali ya dhahabu huku  Tom Donker wa Zambia pia akimaliza katika nafasi ya pili kwa kutumia muda wa 25.66 na kupata medali ya fedha.

Hilal pia alishiriki katika mashindano ya mita 50 ya staili ya backstroke na kumaliza katika nafasi ya saba kati ya waogeleaji 13 kwa waogeleaji wenye umri zaidi ya miaka 17.  Hilal alitumia muda wa 29.91 katika mashindano hayo ambapo Mzambia Tom Donker alishinda medali ya dhahabu kwa kutumia muda wa sekunde 27.40.

Mbali ya Hilal, muogeleaji mwingine wa Tanzania Catherine Mason alimaliza  katika nafasi ya nne katika mashindano ya mita 50 butterfly kwa kutumia muda wa 31.89 kwa wasichana wenye umri wa zaidi ya miaka 17. Catherine pia alimaliza katika nafasi ya nne katika mashindano ya mita 50 ya staili ya backstroke kwa kutumia muda wa  34.13.

Pia muogeleaji wa klabu maarufu ya Dar Swim Club (DSC) , Smriti Gokarn alishika nafasi ya 14 kati ya waogeaji 18 katika mashindano ya mita 200 ya backstroke kwa kutumia muda wa 3.21.30.

Muogeleaji huyo pia alishika nafasi ya tisa kwa kumia muda wa 2.31.31 katika mashindano ya freestyle mita 200 na katika mita 50 butterfly alimaliza katika nafasi ya 11 kwa kutumia muda wa 34.28. Pia alimaliza katika nafasi ya 11 katika mita 50 kwa upande wa staili ya backstroke kwa kutumia muda wa 36.43.

Naye Amani Doggart alianza kwa kushika nafasi ya 14 katika staili ya butterfly kwa kutumia muda wa 38.54 na baadaye kumaliza wa Saba katika staili ya backstroke  kwa kutumia muda wa 37.41 katika mashindano ya mita 50.

No comments: