Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kaskazini, Elias
Kayandabila akisisitiza jambo kabla ya ufunguzi wa masanduku
yenye bahasha za ahadi ya bei za madini yaliyopigwa mnada
katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini
Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016. Katikati ni Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
Zena Kongoi na kushoto ni mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni
ya Sky Associates Faisal Juma Shahbhai inayomiliki mgodi wa Tanzanite
One kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na
Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo
akiangalia maombi ya ahadi za bei ya madini yaliyopigwa mnada
katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini
Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016. Wanaoshuhudia
ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Uchumi na Biashara, Salim
Salim (Wa Pili kushoto), Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Uthamini
wa Madini na Huduma za Kimaabara katika Wakala wa Ukaguzi
wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika na wa
kwanza kulia ni Mthamini Almas wa Serikali, Edward
Rweyemamu.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almas na
Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo
akionesha masanduku yenye bahasha za ahadi ya bei za madini
yaliyopigwa mnada katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya
Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili,
2016. Wanaoshuhudia ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Uchumi
na Biashara, Salim Salim (katikati) na kulia ni Mkurugenzi wa
Uthamini wa Madini na Huduma za Kimaabara katika Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika.
Wadau mbalimbali walioshiriki Maonesho ya Tano ya Kimataifa
ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21
wakimsikiliza Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya
Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard
Kalugendo (hayupo pichani) wakati akitangaza matokeo ya
mnada wa madini uliofanyika katika Maonesho hayo.
Wadau mbalimbali wakishuhudia, Mkurugenzi wa Kitengo cha
Uthaminishaji Madini ya Almas na Vito, katika Wizara ya Nishati
na Madini, Archard Kalugendo akifungua masanduku yenye
bahasha za ahadi ya bei za madini yaliyopigwa mnada katika
Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha
kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016.
Na Teresia Mhagama na Asteria Muhozya, Arusha
Serikali imepata jumla ya shilingi bilioni 1.6 ikiwa ni mapato
yaliyopatikana katika mnada wa madini uliofanyika wakati wa
Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha
katika Hoteli ya Mt.Meru kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili mwaka
huu.
Hayo yameelezwa hivi karibuni jijini Arusha na Mkurugenzi wa
Kitengo cha Uthaminishaji Madini ya Almasi na Vito (TANSORT)
katika Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo, wakati
akitangaza matokeo ya mnada huo.
Katika maonesho hayo, kulikuwa na Tenda Tatu; Tenda ya
Kwanza ilikuwa ya Serikali ikihusisha madini mbalimbali
yaliyokuwa yakishikiliwa na Kamishna wa Madini ambapo jumla
ya shilingi za kitanzania bilioni 1.3 zilipatikana kutokana na mauzo
ya madini hayo.
Tenda ya pili ilikuwa ni madini ya Tanzanite ghafi yaliyozalishwa
na mgodi wa TanzaniteOne unaomilikiwa kwa ubia kati ya
kampuni ya Sky Associates na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO).
“Napenda kushukuru mgodi wa TanzaniteOne kwani wametuletea
madini ya Tanzanite ambayo ni ghafi yenye thamani kubwa
ambapo madini yote kutoka mgodi huu yamenunuliwa kwa
thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni Tano (5),” alisema
Kalugendo.
Kalugendo alisema kuwa tenda ya tatu ya mnada huo ilikuwa ya
kampuni ya El-Hilal inayochimba madini ya Almas nchini.
Alifafanua kuwa, kampuni mbili zilizojitokeza katika tenda hiyo
hazikufikia kiwango cha chini cha bei iliyowekwa na Serikali hivyo
kupelekea madini hayo kutokuuzwa katika mnada huo.
“ Hii ni kusema kwamba madini yote ya Tanzanite yaliyoletwa na
mgodi wa TanzaniteOne na Tanzanite iliyoletwa na Serikali
katika kifurushi cha kwanza pamoja na dhahabu yote iliyokuwa
katika kifurushi hicho yameuzwa,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kuwa, fedha yote iliyopatikana kutokana na mauzo ya
madini yaliyokuwa yakishikiliwa na Kamishna wa Madini,
inaingizwa katika mfuko wa Serikali na kwamba madini ghafi
yaliyouzwa kutoka TanzaniteOne yatalipiwa mrabaha serikalini
wa shilingi milioni 245,686,000 ili madini hayo yaweze
kusafirishwa popote.
Aidha, Kalugendo alisisitiza kuwa mapato hayo ni ya mnada tu
hivyo mauzo ya jumla ya maonesho hayo yatatangazwa baada ya
kujumuisha matokeo ya mauzo yote yaliyofanyika katika
Maonesho husika.
Pia, Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini na Huduma za
Kimaabara kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA), Mhandisi Gilay Shamika, akiwa katika Mnada wa Madini
yaliyo chini ya Kamishna wa Madini, alitoa wito kwa
wafanyabiashara kufuata sheria, taratibu na kanuni za biashara
ya Madini ili kutotaifishiwa Madini yao mara wanapokamatwa bila
kuwa na vibali husika.
‘Madini haya unayoyaona yakipigwa mnada, yalikamatwa na
kutaifishwa pindi yakitoroshwa nje ya nchi bila wahusika kuwa na
vibali vya usafirishaji. Ni vema wafanyabiashara kufuata taratibu
kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010,’’ Alisema
Shamika.
Naye kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na
Biashara, Salim Salim aliwashukuru wadau wote walioshiriki na
kudhamini maonesho hayo ambayo ni muhimu katika uendelezaji
wa Sekta ya Madini nchini.
No comments:
Post a Comment