Thursday, April 14, 2016

BALOZI SEIF ALI IDD MGENI RASMI KATIKA UZINDUZI WA 4G YA ZANTEL ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokelewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin, wakati wa hafla ya kuzindua Mtandao mpya wa Teknolojia ya kisasa wa 4G hapo katika viwanja vya Mnara wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Michenzani Mjini Zanzibar. Nyuma ya Balozi Seif ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Aman Karume na kulia ni Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifurahia jambo na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Balozi Ali Karume kwenye hafla ya uzinduzi wa mtandao Zantel wa 4G.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin akiteta na Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo kwenye hafla hiyo fupi.
Warembo wa Kampuni ya Zantel wakifuatilia tukio la uzinduzi wa mtandao wa 4G kwenye simu zao za mikononi zitakazowawezesha kupata huduma mbali mbali ikiwemo kuonanan na yule watakayempigia.
Balozi Seif akipokea zawadi maalum kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin mara baada ya kuzindua mtandao wa 4G wa Kampuni hiyo.Nyuma ya Balozi Seif ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Amaan Karume. Picha no:-808 ni:- Balozi Seif Wa Tatu kutoka Kushoto akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Zantel, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wageni wengine walioalikwa kwenye uzinduzi wa Mtandao wa 4G.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Ujenzi Balozi Ali Karume na Katibu Mkuu wake Dr. Juma Malik na kushoto ya Balozi ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin, Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipando Nd. Khamis Mussa Pamoja na Afisa muandamizi wa Kampuni ya Zantel hapa Zanzibar Ndugu Baucha. Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Viongozi na Watendaji wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel wanapaswa kuongeza kasi ya utendaji ili waendelee kuwa watoa huduma bora hapa Nchini licha ya kasoro ndogo ndogo zinazoweza kurekebishwa kwa wakati muwafaka.

Alisema Zantel kwa kipindi cha miaka Minane mfululizo imekuwa ikitunukiwa zawadi ya mlipa kodi bora katika kundi la walipa kodi wakubwa, zawadi ambayo hutolewa kila mwaka na Mamlaka ya Kodi Tanzania { TRA }.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma mpya ya mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne { 4G } kwa upande wa Zanzibar iliyofanyika katika Bustani ya Mnara wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Michenzani Mjini Zanzibar.

Alisema ushindi huo ni fahari kubwa kwa Zantel pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye hisa zake ambayo ilipata changamoto kubwa na hatimae kufanikiwa kupata kibali cha kuanzishwa kwa Kampuni hiyo mwaka 1999.

Balozi Seif alieleza kwamba kodi zinazolipwa na Zantel zilizofikia zaidi ya shilingi Bilioni 18 kwa mwaka 2015 pekee zinasaidia Taifa katika kuweka urari wa nakisi ya Bajeti yake.

Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba yapo matatizo yanayolalamikiwa na Wananchi kuhusu kukatika kwa mawasiliano kwa baadhi ya wakati jambo ambalo huleta usumbufu unaochangia baadhi ya wanandoa kutoaminiana.

Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umekusudia kuimarisha zaidi huduma zake ili kuhakikisha unapatikana mtandao wa kasi utakaorahisisha ukuaji wa teknolojia hapa Zanzibar.

Alisema matumizi ya teknolojia hiyo mpya ya mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne { 4G } utasaidia watumiaji kupata huduma zenye ubora na uhakika pamoja na kuwepo kwa ongezeko la kasi la matumizi ya mtandao kama vile huduma za skype, You Tube na mitandao mengine ya Kijamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/4/2016.

No comments: