Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuzingatia thamani ya fedha kwa kila mradi wa ujenzi wa nyumba wanaoutekeleza nchini.
Ametoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ghorofa saba katika eneo la Sida Ada Estate linalojegwa na Wakala huo jijini Dar es Salaam.
Amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Arch.Elius Mwakalinga kuhakikisha kuwa wapangaji wote wanaoishi kwenye nyumba za Wakala huo kulipa kodi zote kwa wakati na watakaoshindwa wahame mara moja.
“Natoa mwezi mmoja kwa watumishi ambao hawajalipa watafute sehemu nyingine ya kukaa, ili wakala apangishe nyumba hizo kwa anaeweza kulipa kwa wakati “,amesema Profesa Mbarawa.
Amewataka watumishi wote wa TBA kufanya kazi kwa malengo yanayopimika ili kuweza kuleta tija na kuongeza pato la Wakala.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Arch.Elius Mwakalinga amemhakikishia Waziri kuwa Wakala unaendelea kutoa huduma ya matengenzo na ujenzi wa nyumba na ofisi za Serikali katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara.
Aidha, ametaja baadhi ya changamoto zinazokabili Wakala huo ni mahitaji makubwa ya nyumba kwa watumishi wa umma kuliko uwezo wa Wakala ambapo kwa sasa mahitaji ya nyumba za watumishi wa Umma ni takribani laki nne.
Ameongeza kuwa kasi ya mabadiliko ya teknolojia hailingani na uwezo wa wakala hivyo ameomba Waziri Profesa Mbarawa kuuwezesha Wakala huo kimtaji na kimafunzo ili uweze kushindana na soko na kuboresha sekta ya ujenzi wa nyumba nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Eng. Jospeh Nyamhanga amesisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo wa Wakala kufanyakazi kimazoea na badala yake kuwa na mtazamo wa kibiashara ili kuweza kujitegemea kama lengo la kuanzishwa kwa wakala huo. Aidha ameongeza kuwa atahakikisha kuwa Wakala huo unapata magari kwa kuongeza tija katika utendaji kazi.
Wakala wa majengo umetumia kiasi cha takribani Bilioni 5 kwa ujenzi wa jengo la ghorofa saba lililojengwa katika eneo la Sida Ada Estate ambapo ujenzi huo umekamilika kwa asilimia tisini na tano.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiongea na Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania - TBA (hawapo pichani) wakati alipotembelea Ofisi za Wakala huo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiongea na Wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania –TBA kutoka mkoa wa Pwani na Dar es salaam katika mkutano wa Wakala huo uliofanyika Karimjee jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga (kulia), akiongea na wafanyakazi wa TBA kutoka mkoa wa Pwani na Dar es salaam katika mkutano wa Wakala huo uliofanyika jijini Dar es salaam. Katikati ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifuatilia.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga (kushoto), akizungumza na wafanyakazi wa Wakala huo (hawapo pichani) kwenye mkutano wa wafanyakazi wa Wakala huo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Huku Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga wakisikiliza.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga (kulia), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa mara baada ya Waziri huyo kukagua mradi wa jengo la ghorofa saba eneo la Sida Eda Estate jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment