Thursday, March 31, 2016

Wakandarasi wasiolipa mishahara, madeni kutopewa kipaumbele REA III.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika moja ya kikao na wakandarasi wanaosambaza  Umeme Vijijini vilivyoanza tarehe 29 Machi na kumalizika tarehe 31 mwezi huu.Wa Tatu kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi kutoka REA, Mhandisi Bengie Msofe. Wengine ni watendaji kutoka kampuni ya Angelique International inayosambaza umeme mkoani Arusha, Wizara na REA.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na kampuni  ya Engineering & Construction inayosambaza umeme vijijini mkoani Kagera katika wilaya za Ngara, Biharamulo, Misenyi, Karagwe, Kyerwa, Bukoba vijijini na Muleba kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya na anayemfuatia ni Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Mhandisi Amos Maganga.Wengine ni watendaji kutoka kampuni hiyo, Wizara na REA.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa kwanza kushoto), Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Mhandisi Amos Maganga (wa pili kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya (wa Tatu kushoto) wakiwa katika moja ya vikao vilivyojumuisha wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini vilivyoanza tarehe 29  Machi na kumalizika tarehe 31 Machi, mwaka huu.

Na Teresia Mhagama
Imeelezwa kuwa wakandarasi wenye tuhuma za kutolipa mishahara wafanyakazi wao, kuomba rushwa  kwa wateja wanaotaka kuunganishiwa umeme na kutolipa fedha za watoa huduma waliokuwa wakifanya nao kazi katika usambazaji  umeme vijijini Awamu ya Pili, hawatapewa kazi husika katika miradi ya REA Awamu ya Tatu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kampuni mbalimbali zinazotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili inayotarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

“Kampuni zitakazopewa kipaumbele ni zile zilizofanya vizuri katika miradi ya REA Awamu ya Pili na kuonekana kuleta ushindani kwa kampuni nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kufanya kazi waliyopewa kwa bidii na kutokuwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo rushwa,” alisema Profesa Muhongo.

Awali Meneja Operesheni wa  kampuni ya Engineering & Construction, Julius Kateti  inayosambaza umeme vijijini mkoani Kagera katika wilaya za Ngara, Biharamulo, Misenyi, Karagwe, Kyerwa, Bukoba vijijini na Muleba alimweleza Profesa Muhongo kuwa kazi ya usambazaji umeme katika mkoa huo imehusisha vijiji 451 na wanatarajia kuunganisha wateja 30,000 kabla ya muda wa ukomo uliowekwa na Serikali.

Alisema kuwa katika wilaya za Ngara na Biharamulo jumla ya wateja 4385 wa njia moja ya umeme waliunganishwa kati ya wateja 4554 na wateja 49 wa njia tatu za umeme waliunganishwa ambapo jumla ya transfoma 47 zilifungwa na kwamba kwa wilaya za  Ngara na Biharamulo wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo Aprili 20 mwaka huu na kuukabidhi mradi huo kwa Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO).

Aidha alisema kuwa katika wilaya ya  Karagwe jumla ya transfoma 82 zilifungwa na wateja wa njia moja ya umeme wapatao 3507 waliunganishwa kati ya wateja 5480 na wateja 95 wa njia tatu ya umeme wameunganishwa ambapo wanatarajia kukamilisha kazi mwezi Mei mwaka huu.

“Mheshimiwa Waziri,  kwa upande wa wilaya ya Kyerwa tumeshafunga transfoma 63 ambapo lengo la awali lilikuwa ni kufunga transfoma 53, na kwa wilaya hii wateja 2044 wa njia moja ya umeme wameunganishiwa umeme kati ya wateja 3228 na wateja 30 wa njia tatu za umeme waliunganishwa na tunatarajia kuendelea kuunganisha wateja hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu,” alisema Kateti.

Vilevile alisema kuwa  katika wilaya ya Misenyi jumla ya transfoma 52 zimefungwa ambapo wateja 1345 wa njia moja waliunganishwa  kati ya wateja 4308 na wateja waliounganishwa kwa njia tatu za umeme ni 17 huku wakitarajia kukamilisha kazi mwezi Juni mwaka huu.

Aliongeza kuwa kwa upande wa wilaya za Muleba na Bukoba Vijijini jumla ya transfoma 118 zimefungwa  ambapo wateja 5649 wa njia moja ya umeme waliunganishwa na huduma hiyo kati ya wateja 12,703 huku wateja waliounganishwa katika njia tatu za umeme wakifikia 22 na wanatarajia kukamilisha kazi mwezi Mei mwaka huu.

Kwa upande wa  kampuni ya JV State Grid, Meneja Mradi wa kampuni hiyo Mhandisi  A. Mwaipaja alisema kuwa kampuni hiyo inasambaza umeme vijijini katika wilaya za Rungwe, Kyela na  Ileje mkoani Mbeya ambapo kazi ya  kusambaza umeme katika wilaya hizo  imekamilika kwa asilimi 92 hadi kufikia katikati mwa mwezi Machi mwaka huu na wateja wapya 2,244 wameunganishwa katika vijiji 65 na kufunga transfoma 90 kati ya 133 wanazopaswa kufunga.

Aidha katika wilaya ya Mbarali mkoani humo, JV State imeshakamilisha kazi kwa asilimia 92  hadi kufikia tarehe 15 Machi, 2016 ambapo wateja wapya 1724 kati ya 4505 katika vijiji 27 wameunganishwa na transfoma 35 kati ya 56 zimefungwa.

Alisema kuwa  kampuni hiyo pia inafanya kazi ya kusambaza umeme vijijini katika mkoa wa Kigoma katika wilaya Sita za  Kigoma Vijijini,  Buhigwe, Kasulu, Kibondo, Kakonko na Uvinza ambapo kazi imekamilika kwa asilimia 93 hadi kufikia Machi 2016 na jumla ya vijiji 63 na wateja  2,647 kati ya 8773 wameunganishwa na umeme katika wilaya hizo.  

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini,  Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini kujiepusha na masuala ya rushwa katika utekelezaji wa miradi hiyo hasa katika zoezi la  uunganishaji umeme kwa wateja. 
  

No comments: