Msimamizi wa
mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu
kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela akiangalia maendeleo ya kisima kimoja
kati ya viwili vinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa
(DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
Wataalam
kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) wakiendelea kuchimba
kisima chenye urefu wa mita 130 katika shule ya Msingi Mbagala majimatitu,
Temeke jijini Dar es salaam. Msimamizi
wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala
majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela na Mhandisi Elizabeth Kingu, Katibu
Tawala Msaidizi Huduma za Maji (kushoto) wakiangalia maendeleo ya moja ya
kisima kinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika
shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
Na. Aron Msigwa –Dar es salaam.
Walimu na
wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Majimatitu iliyoko Temeke jijini Dar es
salaam watanufaika na huduma ya maji safi kufuatia Serikali kutoa kiasi cha
shilingi milioni 24.5 kwa lengo la kufanikisha mradi wa uchimbaji wa visima
viwili kwa lengo la kuboresha taaluma na mazingira ya shule hiyo.
Akizungumzia
uchimbaji wa visima hivyo leo jijini Dar es salaam msimamizi wa mradi huo kutoka Mamlaka ya Maji Safi
na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Abel Chibelela amesema kuwa kuchimbwa kwa
visima hivyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali kuitaka DAWASA kutafuta vyanzo
vya maji katika shule hiyo ili kuwaondolea adha ya uhaba wa Maji.
Amesema shule
hiyo imekuwa na tatizo hilo kufuatia kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 6000
inayozidi uwezo wa miundombinu iliyopo sasa ikiwemo kisima kinachotumiwa na
wanafunzi hao kinachozalisha lita 8000 kwa siku wakati mahitaji halisi ya maji ni
Lita 40,000 kwa siku.
Amesema
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima
na Mabwawa ( DDCA) ilipewa jukumu la kuchimba visima viwili vya shule hiyo kwa thamani ya shilingi
milioni 24.5 zikiwa ni gharama za uchimbaji, usafishaji wa visima hivyo na
gharama za vipimo vya maabara ili kuangalia ubora wa maji hayo.
" Kazi ya
uchimbaji wa visima hivi vyenye urefu wa mita 130 na 140 imeanza rasmi na
itachukua siku 14, tunafanya haraka ili tuweze kujua wingi wa maji yaliyopo na
ubora wake kama inafaa kwa matumizi ya binadamu"
Pia amesema
DAWASA itasimamia ujenzi wa minara mirefu ya matenki na kuongeza matenki
makubwa yatakayokidhi mahitaji ya shule hiyo yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita
20 kwa kila shule.
Kwa upande
wake Mtaalamu kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) ambayo
ndiyo iliyopewa jukumu la kuchimba visima hivyo na DAWASA Bw. Nungwe Gwaga
akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo amesema kuwa wao kama wataalam wa
kuchimba visima walifanya utafiti katika eneo hilo na kujiridhisha kuwa eneo la
shule ya Msingi Mbagala Maji Matitu lina Maji ya kutosha.
" Sisi
kama wataalam tulifanya utafiti (Physical Survey) katika eneo hili ili kujua
kama kuna maji na miamba inayopita pale pamoja na umbali wake, sisi
tumejiridhisha tutachimba mita 130 ambazo tayari zimetupa majibu ya kuwepo kwa
Maji "
Mwalimu Mkuu wa
Shule hiyo Bw. Abdul Mgomi akifafanua kuhusu visima hivyo amesema vitawezesha shule
yake kuondokana na adha ya uhaba wa huduma ya maji inayowakabili wanafunzi
shuleni hapo kufuatia mwitikio wa wazazi kuwaandikisha watoto wao shuleni hapo
kwa mwaka 2016.
Amesema kwa
sasa shule hiyo inatumia kisima kidogo chenye uwezo wa kuzalisha lita 8000 kwa
siku ikilinganishwa na mahitaji halisi ya lita 32000 kwa wanafunzi 6000
wanaosoma shuleni hapo.
Mwalimu Mgomi
ameshukuru jitihada zilizofanywa na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa
na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo Mhe. Said Mecki Sadiki kwa kuwezesha upatikanaji
wa fedha za kuchimbia visima hivyo.
Ameeleza kuwa
mara baada ya visima hivyo kukamilika
uongozi wa shule utaweka utaratibu wa matumizi ya maji hayo kwa shule na
ziada itakayopatikana na maji itauzwa kwa majirani wanaoishi kuzunguka shule
hiyo ili mradi uweze kujiendesha wenyewe.
Aidha, amesema
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuifanyia kazi
changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa kujenga mapya 10 ili
kukidhi mahitaji ya wanafunzi 6000 waliopo shuleni hapo pamoja na ujenzi wa shule
nyingine 2 zitakazoondoa kabisa tatizo la mrundikano wa wanafunzi.
Naye mmoja wa
Wazazi na Mjumbe wa Kamati ya Miradi ya shule hiyo Bi.Happiness Mgulambwa
akizungumza katika eneo vinapochimbwa visima hivyo ameishukuru Serikali kwa
kusikia kilio cha wazazi na wanafunzi hao kwa kuamua kuwachimbia visima hivyo
huku akiongeza kuwa upatikanaji wa
huduma ya maji shuleni hapo utaongeza ufanisi kwa walimu na wanafunzi.
Amesema wao
kama Wazazi kupitia kamati ya miradi ya shule hiyo waliiomba Serikali kuwasaidia
kupata maji kwa wanafunzi shule hiyo ili
kuondoa kero ya maji jambo ambalo lilikubaliwa.
" Kweli
wanafunzi wa shule hii walikua wanapata shida,uhaba wa maji hapa shuleni
uliwalazimu kuja na maji kwenye madumu jambo liliowafanya wakati mwingine
kufika wamechoka na hata kuchafuka, tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya
tano kwa kutusaidia" Amesema Bi.Mgulambwa.
MIWISHO.
No comments:
Post a Comment