Thursday, March 24, 2016

Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kuendelea kuwezesha miradi ya Umeme

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na watendaji kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Mwakilishi wa Shirika hilo nchini, Emmanuel Baudran (katikati) na kushoto ni Dennis Munuve kutoka Shirika hilo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ( wa kwanza kulia) akiwa katika kikao na watendaji kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.

Na Teresia Mhagama,

Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) limesema kuwa limeshatoa jumla ya Euro milioni 321 kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa ambazo ni sawa na wastani wa Euro milioni 50 kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo nchini na kwamba mpango wake ni kuongeza kiwango hicho ifikapo mwakani.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Tanzania, Emmanuel Baudran wakati alipofika Wizara ya Nishati na Madini ili kuzungumza masuala mbalimbali na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.

Baudran alieleza kuwa fedha hizo ambazo zimetolewa kupitia mkopo wenye masharti nafuu zimeelekezwa katika Sekta za Maji, Nishati na Miundombinu ya usafirishaji.

Alisema kuwa kwa mwaka ujao Shirika hilo linaweza kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa nchini kutoka Euro milioni 50 hadi Euro milioni 100 kwa mwaka kupitia mikopo ya masharti nafuu huku kipaumbele kikiwa ni Sekta hizo za Nishati, Maji, na miundombinu ya usafirishaji na kwamba Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na Shirika hilo.

Aliongeza kuwa katika miezi ijayo AFD itajikita katika utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa gridi ya Taifa ya umeme, uboreshaji wa vituo 10 vya kupooza umeme pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka Geita mpaka Nyakanazi (220 KV) ikiwa ni hatua ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupanua gridi ya Taifa kwa upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania (North-West grid extension) ambayo itaunganisha mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alilishukuru Shirika hilo la AFD kwa ushirikiano wanaouonesha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini na kueleza kuwa juhudi hizo zitapelekea kutimiza lengo la Serikali la kuwa na umeme wa kutosha, unaotabirika, na wa bei nafuu ambao utapunguza mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali.

Profesa Muhongo alisema kuwa Shirika hilo pia linaweza kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia, makaa ya mawe, maji na nishati jadidifu kama vile jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari na bayomasi au kuendelea kuisaidia Tanesco na wawekezaji binafsi katika miradi hiyo ya uzalishaji umeme.

Aidha Profesa Muhongo alisema kuwa Shirika hilo pia linaweza kuiwezesha Serikali katika uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji umeme ambapo alisema kuwa kwa sasa Serikali imeamua kujenga miundombinu yenye uwezo mkubwa wa usafirishaji umeme wa kilovolti 400 na kuachana na miundombinu ya 220 KV kwani zoezi la ubadilishaji wa miundombinu hiyo kutoka 200kv hadi 400kv hugharimu fedha nyingi.

Aliongeza kuwa Serikali pia imeweka mkazo katika usambazaji umeme vijijini ili kuongeza kiwango cha watu wanaopata umeme katika maeneo hayo ambayo sasa imefikia asilimia 21 na kwamba hilo litawezekana endapo Taasisi mbalimbali za kifedha kama AFD zikiamua kufadhili miradi hiyo.

“Tunatafuta misaada ya kifedha ili kuongeza upatikanaji wa umeme vijijini hasa katika huduma za kijamii kama mashule na vituo vya afya,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Vilevile Profesa Muhongo aliliomba Shirika hilo kuangalia namna ya kuwawezesha au kushirikiana na wawekezaji wa miradi midogo ya umeme (chini ya megawati 20) ili kuweza kuzalisha umeme au katika hatua ya upembuzi yakinifu ambapo miradi mingi kati ya hiyo ipo nje ya gridi ya Taifa.

Ili Tanzania iweze kufikia Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali imejikita katika kuhakikisha kwamba idadi wananchi waliofikiwa na huduma ya umeme inaongezeka hadi kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka huo.

No comments: