Thursday, March 31, 2016

SERIKALI KUIWEZESHA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI KUHAKIKI RASILIMALI NA MADENI YA VIONGOZI WA UMMA

Na Mwandishi wetu.
SERIKALI imesema kuwa italipa kipaumbele suala la uhakiki wa mali za viongozi wa umma  kwa kuiwezesha Sekretarieti ya Maadili ya viongozi kufanya kazi zake  kwa ukamilifu kwa mujibu wa Sheria ya  Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imetembelea ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma kujua majukumu, mafanikio na changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo  ili wakifika bungeni waweze kuisemea.

“Suala la uhakiki wa rasilimali na madeni ya viongozi tutahakikisha linapewa kipaumbele katika Awamu hii ya tano ya  uongozi,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, Serikali itajitahidi kuongeza jitihada ili uhakiki  wa rasilimali na madeni ya viongozi wa Umma ufanyike,  pamoja na kuiongezea Taasisi hiyo bajeti ya kutosha.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukum u ya ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Mhe  Salome Kaganda amesema viongozi wengi wanarejesha fomu za raslimali na madeni, ila wapo wachache wanaoshindwa kurejesha fomu hizo.
Amesema, “Tangu mwaka 2005/06 hadi mwaka 2014/15 tumesambaza  fomu 78,786, lakini fomu zilizorejeshwa ni 60,948 ambazo ni sawa na asilimia 77 ya fomu zote zilizosambazwa.”

Aidha Kamishna huyo amewaambia  wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge kuwa tangu mwaka 2013 hadi 2015 Sekretarieti yake haikufanya uhakiki wa rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma kutokana na  ufinyu wa bajeti.
Kwa upande wao baadhi ya Wajumbe wa kamati wamesema kuwa wataishauri serikali kuiongezea Sekretarieti bajeti ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sharia.

Pia wamependekeza kufanyiwa maboresho Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ili iwe na nguvu zaidi na kuwaruhusu kuwafikisha mahakamani viongozi wanaokiuka sharia hiyo.

Sekretarieti ya Maadil  ilianza kufanya kazi rasmi mwezi Julai, 1996 ikiwa na jukumu la msingi la kujenga na kukuza uadilifu miongoni mwa Viongozi wa Umma kwa kusimamia utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma Na 13 ya mwaka 1995.

No comments: