Mkuu wa Matengenezo wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini
Tumaini Ndosi (aliyepanda juu) akitoa ufafanuzi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba kuhusu moja ya mita inayosoma
kiwango cha ujazo wa maji yanayosafirishwa kutoka kwenye Pampu za kusukumia
maji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo
Futakamba (kulia) akizungumza jambo na Meneja wa Mtambo wa kuzalisha maji
wa Ruvu Chini, Emmanuel Makusa (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO
Muhandisi Cyprian Luhemeja mara baada ya kukagua mitambo na pampu za
kusukumia Maji za Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Eneo la ndani la Mtambo wa kuzalisha maji likiwa limekamilika
mara baada ya kufungwa pampu mpya zenye uwezo wa kusukuma maji Lita milioni
270 kwa siku kuja jijini Dar es salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo
Futakamba (katikati) akieleza namna wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa
wa Pwani watakavyonufaika na huduma ya Maji mara baada kukamilika kwa
ujenzi wa bomba la kusafirishia Maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini kuja
jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na
Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Archard Mutalemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa
DAWASCO Muhandisi Cyprian Luhemeja.
Sehemu ya maungio ya Mabomba yanayoingiza maji ndani ya Mtambo
huo kutoka mto Ruvu, chini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es
salaam (DAWASCO) Muhandisi Cyprian Luhemeja akitoa ufafanuzi kwa waandishi
namna DAWASCO ilivyojipanga kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Dar es salaam
kwa kuwafikishia huduma ya Maji Safi kufuatia kukamilika ujenzi wa bomba la
Maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Moja ya maungio ya Bomba kubwa la kusafirishia Maji kutoka
mtambo wa Maji wa Maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo Pwani lililoko eneo la
Tegeta jijini Dar es salaam likiwa limekamilika.
Sehemu ya ndani ya Matenki yanayopokea maji kutoka mtambo wa
Ruvu Chini yaliyoko eneo la Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es salaam.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo
Futakamba akibonyeza moja ya mashine inayoongoza pampu za kusukuma Maji
kwenda jijini Dar es salaam kutoka Mtambo wa kuzalisha Maji wa Ruvu Chini
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya majaribio ya mtambo huo
mara baada kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirisha maji lenye urefu
wa kilometa 55.9.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Hatimaye moja ya Pampu kubwa katika mtambo wa kuzalisha Maji kwenye chanzo
cha maji cha Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani imewashwa kwa majaribio
kufuatia kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba kubwa la kusafirishia maji
lenye urefu wa kilometa 55.9 kutoka chanzo hicho kwenda jijini Dar es
salaam.
Majaribio hayo ni sehemu ya awali ya kupitisha maji yenye msukumo mkubwa
kwenye bomba hilo kuelekea kwenye matenki makubwa ya kuhifadhia maji
yaliyoko eneo la Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya kuwasha Pampu hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji
na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamaba amesema kuwa majaribio hayo
ambayo yameonyesha mafanikio yatawawezesha wakazi wa jiji hilo na maeneo ya
mkoa wa Pwani kupata huduma ya uhakika ya Maji kufikia mwishoni mwa mwezi
Machi mwaka huu.
Amesema mradi huo utakuwa suluhisho la tatizo la maji la muda mrefu kwa kuwa
kiwango cha maji kitakachozalishwa kwa siku kitafikia lita milioni 270 ambazo
zitaongezwa kwenye msukumo wa lita milioni 182 zilizokuwa zikizalishwa hapo
awali kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo.
“Hii ni faraja kwa Serikali na wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa wa
Pwani, sasa tutapata lita Zaidi ya milioni 270 kwa siku haya ni mafanikio
makubwa, kulingana na mahitaji tuliyokuwa nayo tutahakikisha tunayasambaza
maji haya ili kukidhi mahitaji ya wananchi” Amesema Muhandisi Futakamba.
Muhandis Futakamba amewataka wahandisi na watendaji wanaosimamia uendeshaji
wa mitambo hiyo kuwa mahili na makini katika utekelezaji wa majukumu yao
ili kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi na kwa maslahi ya umma.
Ameiagiza DAWASA na DAWASCO kuendelea kuwajengea uwezo kielimu Wahandisi wa
ndani wanaohusika na utunzaji wa miundombinu hiyo ili miradi ya maji
wanayoisimamia iweze kudumu na kuwa endelevu kupitia matengenezo na huduma
mbalimbali watakazozifanya.
“Ninyi kama wahandisi na wasimamizi wa miradi na mitambo hii mikubwa
hakikisheni mnajenga uwezo wenu wa ndani ili muweze kuiendesha na
kuidhibiti mitambo hii pia kuwa na uelewa wa ndani wa mifumo yote
iliyotumiwa wakati wa uwekaji wake na mabadiliko ya teknolojia” Amesisitiza.
Pia amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wanatunza mitambo na
miundombinu yote ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea
kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA)
Muhandisi Archard Mutalemwa akizungumza mara baada ya kukagua mitambo ya
kuzalisha Maji ya Ruvu Chini amesema kuwa kukamilika kwa bomba hilo ni
mwendelezo wa juhudi za Serikali kupitia DAWASA za kuhakikisha wananchi
wanafikiwa na huduma ya maji Safi.
Amesema DAWASA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha
inaendeleza na kusimamia miradi ya maji ikishirikiana na wadau mbalimbali
wa maendeleo na kuhakikisha inawawezesha wakazi wa jiji la Dar es salaam na
maeneo ya mkoa wa Pwani yanapata huduma ya Maji Safi kupitia miradi iliyo
chini yake.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam
(DAWASCO) Muhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza mara baada ya kuwashwa kwa
mtambo huo amesema kuwa DAWASCO imejipanga kuhakikisha inawasambazia huduma
ya maji wakazi wengi zaidi wa jiji hilo ambao walikua na miundombinu lakini
hawapati huduma hiyo pamoja na kuunganisha wateja wapya kwa gharama nafuu.
“Naishukuru Serikali kwa kuwezesha mafanikio haya sisi kama DAWASCO
tumejipanga na tutahakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi, yapo
maeneo mengi yaliyokuwa na changamoto ya huduma hiyo hata yale ambayo
yalikua yameunganishwa tayari katikati ya jiji nay ale yaliyo pembezoni mwa
jiji tutahakikisha tutayafikia” Amesisitiza.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kudhibiti wa wizi wa maji amesema
DAWASCO imeanzisha maeneo 25 (DMA) ambayo yamefungwa mita kubwa katika
wilaya za jiji hilo ili kuwawezesha Mameneja wa Zoni husika kuweza kubaini
wizi , upotevu wa maji, ubovu wa mita na tatizo la usomaji na kisha
kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kuhujumu miundombinu hiyo.
Aidha, amesema DAWASCO imeandaa mpango wa kuziondoa mita zote ambazo
zimefikia umri wa miaka 10 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa mradi wa ujenzi wa bomba kubwa la kusafirishia maji kutoka
mtambo wa Ruvu Chini wenye urefu wa kilometa 55.9 umejengwa na Kampuni ya
JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zote
zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment