Thursday, March 31, 2016

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA SERIKALI KWA UJENZI TB III


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA



Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongezaSerikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kujenga jengo zuri la tatu la abiria (TB III)  litakaloboresha zaidi huduma za usafiri wa anga.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Norman Sigalla (Makete) wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea jengo hilo katika ziara yao ya kukagua miradi ya Serikali mwanzoni mwa wiki.

Jengo hilo linajengwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwa Euro milioni 254 (sh. Bilioni 560) za mkopo kutoka Benki ya HSBC ya Uingereza na CRDB kwa dhamana ya Serikali ya Tanzania na Uholanzi.

Tayari TAA imeshamlipa Mkandarasi wake, Bam International ya Uholanzi, Euro milioni 96 baada ya kukamilisha asilimia 60 ya kazi. Jengo hilo linajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ipo katika hatua za mwisho.

Mwenyekiti Sigalla na Wajumbe wengine wa Kamati hiyo walieleza kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali kujenga jengo hilo linalotarajiwa kukamilika Desemba 2017.

Baada ya kufurahishwa na kazi hiyo nzuri na kushauri uboreshaji zaidi wa utendaji, wabunge waliahidi kuisukuma Serikali iiwezeshe zaidi TAA kifedha ikamilishe miradi yake kwa wakati.

 Walisema hayo baada ya kupokea taarifa za utendaji na miradi ya TAA kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi George Sambali na Mkurugenzi anayesimamia Mradi wa TB III, Mhandisi Mohammed Millanga.
Pia walipokea taarifa ya  Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha aliyeeleza uhaba wa fedha wanazopewa unavyowaathiri katika kuendesha shughuli nyingi za kiwanja hicho ambacho ni kitovu cha mapato ya TAA.

TAA inayosimamia viwanja 58 vya ndege vya Serikali Tanzania Bara, hukusanya zaidi ya sh. Bilioni 67 lakini hupewa sh. Bilioni 17 tu kwa ajili ya kujiendesha huku JNIA ikipata sh. Milioni 700 tu kwa mwezi ukitoa za mishahara.

Taarifa  za watendaji TAA zilionesha maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege inayoendeshwa na kusimamiwa na TAA, jengo la TB III, ukarabati JNIA, changamoto zake kubwa na mipango ya Serikali kuzitatua.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Sambali alieleza dhamira ya TAA kuwa na kiwanja kipya cha ndege nje ya Dar es Salaam au kupanua JNIA kwa kuongeza njia zaidi za kurukia ndege ifikapo 2030.

Hata hivyo, aliwaeleza wabunge changamoto ya TAA kutekeleza dhamira hiyo kuwa ni ulipaji fidia kwa wananchi na reli ya TAZARA kupanua eneo la sasa la JNIA au kupata zaidi ya dola milioni 500 kuanzisha kiwanja kipya nje ya Dar es Salaam.

Wabunge waliitaka TAA kufanya tathmini ya gharama za upanuzi wa JNIA kwa kulipa fidia wananchi na kuhamisha reli ya Tazara au  kujenga kiwanja kipya nje ya Dar es Salaam ili kuangalia uwiano kwa lengo la kuishauri Serikali mapema zaidi kabla ya 2030.

Wabunge walilalamikia ukosefu wa ndege za kutoa huduma na zilizopo kutoza nauli kubwa wakati Serikali inaboresha zaidi miundombinu.

Mhandisi Sambali alieleza ukosefu wa ndege unatokana na ushindani wa kibiashara wa mashirika ya ndege ambapo mengine hayaji kwa kukosa abiria wanaounganisha safari za  nje.

Pia alieleza Serikali kutokuwa na shirika imara la ndege kufuatia ATCL kuwa na ndege moja tu kumefanya asilimia 90 ya abiriawatumie nchi za jirani  kuunganisha safari za nje.

Kufuatia maelezo hayo, wabunge waliitaka Serikali inunue ndege nne ili ATCL  irudi hewani kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Magufuli.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani alisema wamepokea rai ya wabunge akisisitiza dhamira ya Serikali ni kununua ndege.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA UHUSIANO
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)
MACHI 30, 2016

No comments: