Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna ( wa pili kutoka kulia) akielezea majukumu ya kampuni hiyo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Taasisi zilizopo chini yake.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akielezea fursa za uwekezaji katika sekta ya gesi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna (kushoto) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Pan African Energy Nchini Patrick Rutabanzibwa (kulia) wakinukuu maelekezo kutoka kwa Wiziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) kufanya kazi katika mtindo wa kisasa ili nishati ya umeme iweze kuwa ya uhakika kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na Kampuni ya Pan African Energy kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilichoshirikisha pia watendaji kutoka wizara ya nishati na madini, TANESCO, TPDC na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema mahitaji ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika ni makubwa, hivyo hakuna sababu ya kuwepo kwa upungufu wa nishati ya umeme nchini wakati kuna gesi ya uhakika.
Alifafanua kuwa haiwezekani shirika la TPDC likadai kuwa kuna gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme, wakati kuna upungufu wa umeme nchini.
Alisema serikali ina mpango wa kuhakikisha kuwa wananchi wote hasa waishio vijijini wanaunganishwa na umeme wa uhakika kupitia Wakala wa Nishati Nchini (REA) hivyo ni jukumu la mashirika hayo kuhakikisha yanabuni miradi na kukaribisha wawekezaji mbalimbali katika uzalishaji wa umeme wa uhakika ili wananchi wote waweze kuunganishwa na huduma ya umeme.
Alisisitiza kuwa amekwishawaalika wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa Megawati 1000 za umeme kwa ajili ya kuingizwa kwenye gridi ya taifa, hivyo ni vyema shirika la TPDC likahakikisha gesi ya uhakika inapatikana ili umeme uweze kuzalishwa mara moja.
“ Lengo la serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 Megawati 10,000 zinazalishwa, hivyo sekta ya nishati kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kutoka kwenye kundi la nchi masikini duniani na kuingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati, kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, inavyofafanua,”alisema Profesa Muhongo.
Wakati huo huo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni ya Pan Afrian Energy kuhakikisha inatatua changamoto zote inazozikabili kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kukutana naye Juni 01 mwaka huu kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kampuni hiyo katika kuzalisha gesi ya uhakika.
Alisisitiza kuwa kutakuwepo na utaratibu wa kukutana na kampuni hiyo kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo, na serikali ipo tayari kutoa msaada pale kampuni itakapokwama.
Aidha, Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kuajiri vijana wa kitanzania wanaomaliza masomo ndani na nje ya nchi baada ya kupata ufadhili kutoka serikalini.
“ Kwa sasa tuna vijana wengi waliohitimu mafunzo kwa ngazi ya shahada za uzamili katika masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kama Norway, Uingereza na China, hivyo ni vyema wakapata ajira katika kampuni ya Pan African Energy, ili nao waweze kufaidika na elimu na uwepo wa uwekezaji katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna, akielezea mafanikio ya uwekezaji kupitia kampuni yake, alieleza kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutoa ajira 87 kwa watanzania na kuboresha huduma za jamii kama vile kutoa huduma ya umeme bure katika eneo la Kilwa kilipo kituo chake za kuzalisha gesi.
Aliendelea kusema kuwa kampuni ya Pan African Energy imejenga zahanati pamoja na kutoa mafunzo kwa waajiriwa wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inakuwa na wataalam wazawa.
No comments:
Post a Comment