Tuesday, February 9, 2016

Serikali kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya wawekezaji wa Umeme- Profesa Muhongo

Na Teresia Mhagama, Mtera

Imeelezwa kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutafuta fedha  kwa   ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ambayo wananchi  wameamua kuiendeleza  ikiwemo miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama maji,upepo, jua, nishati  jadidifu, makaa ya mawe na mawimbi ya bahari. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa kikao chake na wazalishaji wa umeme wa maji na wale wanaotaka kuzalisha umeme huo chini ya megawati 20 kilichofanyika katika Kituo cha Kuzalishia Umeme cha Mtera. 

“Serikali lazima iwe Msemaji wa wawekezaji hawa ili kuhakikisha wanapata fedha na teknolojia za kuendesha miradi yao na hii itapelekea Taifa kuwa na nishati ya kutosha kwani wawekezaji hawa sasa watakuwa na uwezo wa  kuzalisha umeme,” alisema Profesa Muhongo. 

Ili kufanikisha suala, Profesa Muhongo  aliwataka wadau hao wanaotaka kuzalisha umeme wa maji chini ya megawati 20 kuhakikisha kuwa wanaandika na kuwasilisha wizarani mapendekezo yanayochanganua  miradi  wanayotaka  kuanzisha kabla ya mwisho wa mwezi huu ili litengenezwe kalabrasha moja litakalotumika katika kuombea fedha kwa wafadhili mbalimbali na Taasisi za Kifedha. 

“Ifikapo tarehe 28 mwezi huu mchanganuo wa mapendekezo yenu yawe yamemfikia Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati ili serikali iangalie namna ya kutafuta fedha zitakazowawezehsa  kuendeleza miradi yenu ya  umeme badala ya  mtu mmoja mmoja kuanza kuzunguka na maombi yake binafsi  ya kutafuta fedha kutoka Taasisi mbalimbali jambo linalochelewesha upatikanaji wa fedha hizo, “ alisema Profesa Muhongo. 

Profesa Muhongo alisema kuwa tayari serikali imeshaanza majadiliano na Taasisi za kifedha kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB),  Benki ya Dunia  (WB) na nchi wahisani kwa ajili ya kupata fedha za kuendeshea miradi mbalimbali ikiwemo ya Nishati ambapo alisema kuwa suala hilo litafanyika kwa ufanisi endapo miradi yote inayoombewa fedha itajumuishwa katika kalabrasha moja litakaloainisha miradi yote  inayohitaji kuendelezwa. 

Waziri wa Nishati na Madini alisema kuwa kwa sasa serikali inazalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia (50%), maji (35%), na mafuta mazito (15%) na kueleza kuwa Tanzania bado ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme ambavyo vinahitaji wawekezaji makini ikiwemo upepo, joto ardhi,makaa ya mawe na jua ili nchi iwe na umeme wa uhakika, unaotabirika na wa bei nafuu. 

“ Ndugu zangu tunapaswa kutekeleza miradi hii ya nishati kwa kasi kubwa kwani Tanzania ni nchi mwananchama wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Nishati Endelevu kwa Wote (SE4ALL) ambao unaelekeza kwamba ifikapo mwaka 2030 kila mtu anapaswa kuwa na nishati ya umeme na sisi Tanzania ndio tuliwakilisha nchi za Afrika  kutengeneza Mpango huo, “ alisema Profesa Muhongo. 

Alisema kuwa Mpango huo wa SE4ALL malengo yake makuu ni upatikanaji wa nishati kwa wote ifikapo mwaka 2030, ongezeko la maradufu la utumiaji wa nishati jadidifu na matumizi bora ya ya nishati. 

Profesa Muhongo alisema kuwa tayari ameshatia saini Mpango huo ambao utawezesha Tanzania kufaidika na fedha zitakazotolewa ili kuendeleza miradi ya nishati na kusema kuwa tayari Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kufaidika na Mpango huo wa SE4ALL na kutaka wawekezaji zaidi waendelee kujitokeza ili kuendeleza miradi ya umeme nchini. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao wa umeme wa maji na wale wanaotaka kuanzisha miradi hiyo ikiwemo kutoa msaada wa kitaalam ili kuongeza kiwango cha nishati ya  umeme nchini. 

“TANESCO itaendelea kutoa ushirikiano kwenu na naomba tuendelee kushirikiana ili kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika uendelezaji wa miradi hii na ninaomba mjitokeze zaidi na kuwekeza katika maeneo  mbalimbali ikiwemo Kigoma, Liwale na Loliondo sehemu ambazo bado changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo ni kubwa.,”alisema Mhandisi Mramba. 

Naye  Mkurugenzi wa Maendeleo ya Masoko  na Teknolojia, kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA),Mhandisi Gissima Nyamohanga) alisema kuwa mpaka sasa Wakala huo umeshatoa Dola za Marekani milioni 3.1 kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa wajasiriamali  wanaotaka kuwekeza katika miradi ya nishati nchini. 
  
Pia Wakala huo umetoa Dola za Marekani milioni 5.4 kwa kampuni za   zilizoanza kuzalisha umeme ili waweze kuunganisha  umeme huo kwa wananchi.

No comments: