Muonekano wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro unaojengwa njia za
kutua na kuruka ndege na kukarabatiwa jengo la abiria. Ujenzi huo unafanywa na kampuni ya
NACO kutoka Uholanzi.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa
kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akielekea kukagua ujenzi
wa njia za kuruka na kutua ndege mara baada ya kukagua hanga la uwanja huo. Katikati ni
Mkurugenzi wa Via Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni Muwekezaji wa Hanga hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na
Mkurugenzi wa Via Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni Muwekezaji wa Hanga katika
Uwanja wa Ndege wa KIA.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Arusha, Eng. John Kalupale (wa pili
kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa (kushoto) kuhusu ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa Km 26
unavyoendelea.
Muonekano wa moja ya makalvati makubwa yaliyojengwa katika barabara ya Kia-Mererani
yenye urefu wa Km 26.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa
Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani Km 26.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akikagua
karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA mkoani Manyara.
Serikali imeitaka kampuni ya KADCO inayoendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), kuongeza mapato na kuimarisha ulinzi ili kulinda hadhi ya uwanja
huo, kuchangia pato la serikali na kudhibiti hujuma dhidi ya watu wasio waaminifu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo
wakati akikagua utendaji wa uwanja huo na mradi wa ujenzi wa njia za kurukia ndege
na jengo la abiria unaondelea katika uwanja huo.
Prof. Mbarawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa KADCO Bw. Bakari Mururusi,
kuhakikisha kuwa uwanja huo kuanzia mwaka huu wa fedha unazalisha mapato
yanayowiana na hadhi yake na kuchangia kikamilifu mapato ya Serikali na kuachana na
utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea.
“Siridhiki na kiasi cha bilioni 18 mnazozalisha kwa mwaka, nawataka kuanzia sasa
mkusanye mapato ya kutosha na kudhibiti vitendo vya hujuma ili kuupa hadhi
inayostahili uwanja huu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amemtaka Muwekezaji wa Hanga (garage) la Uwanja huo kujiandaa kuondoka
kutokana na kutowekeza kikamilifu katika kipindi cha miaka 10 alichokodishiwa na
kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kukabidhi hanga hilo kwa Shirika la Ndege nchini
(ATCL), ifikapo Julai mwaka huu ili lifanye kazi kwa faida na madhumuni
yaliyokusudiwa.
“Nia ya Rais ni kufufua ATCL liwe na hadhi inayoshatahili hivyo hanga hili tutawapa
ATCL na kuwasimamia ili wafanye kazi kikamilifu na kuleta mapato kwa Serikali”,
amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amemweleza Mkurugenzi wa Kampuni ya Via Aviation inayomiliki
hanga hilo kwa miaka 10 kuwa Serikali hairidhishwi na mapato yanayotokana na hanga
hilo hivyo imejipanga kuitumia kuleta faida zaidi kwa Serikali katika mkakati wake wa
kukuza uchumi.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani
yenye urefu wa Km 26 inayojengwa na Kampuni ya Chicco kwa gharama ya shilingi
bilioni 32.2 na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa
wakati.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara,
Eng. Yohani Kasaini amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa licha ya barabara hiyo
kupita katika ukanda wa tambarare jumla ya makalavati makubwa 6 na madogo 85
yanajengwa ili kukabiliana na changamoto ya mafuriko na hivyo kuiwezesha barabara
hiyo kupitika wakati wote wa mwaka.
Barabara ya Kia-Mererani ina umuhimu wa kipekee kiuchumi kwani inapita katika
ukanda wenye rasilimali zenye madini ya Tanzanite, eneo zuri la kilimo, ufugaji, utalii na
misitu hivyo kukamilika kwake kutapunguza gharama za usafiri na kuvutia watalii wengi
kuja nchini.
Serikali iko katika mkakati wa kuimarisha uwanja wa ndege wa KIA kwa kukarabati
jengo la abiria na njia za kutulia na kurukia ndege ambapo kampuni ya NACO kutoka
Uholanzi inajenga uwanja huo ili kuuwezesha kufanya kazi kisasa, kuruhusu ndege
nyingi kutua na kuongeza mapato ya uwanja huo na Serikali kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa taasisi zilizo chini ya
wizara hiyo mkoani Manyara kufanyakaz kwa umoja, uwazi, uadilifu ili kuiwezesha
lengo la wizara hiyo la kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa kufikia uchumi wa
kati 2025 kutimia kwa wakati.
No comments:
Post a Comment