Friday, February 12, 2016

makala: Kwanini mazungumzo ya amani nchini Syria yameshidikana

Na Nizar Visram 

HATIMAYE mazungumzo ya amani kuhusu Syria yaliyokuwa yakifanyika jijini Geneva yamesitishwa bila mafanikio. Msuluhishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Bw Staffan de Mistura kuanzia tarehe 31 Januari mwaka huu alikutana na pande zinazopigana – upande wa serikali ya Rais Bashar Assad na upande wa waasi kutoka makundi mbalimbali. 

Kulikuwepo na waasi waliounda kile walichokiita kamati kuu ya mazungumzo (High Negotiations Committee - HNC) inayoungwa mkono na Saudia. Kamati hii inaongozwa na Riad Hijab. Wao walimwambia Mistura kuwa hawatashiriki mazungumzo mpaka serikali ya Syria itakapositisha mabomu yake na kuruhusu misaada ifikishwe kwa “raia waliokuwa wamezingirwa na majeshi ya Syria” 

Kikundi cha Wakurdi wa Syria walizuiliwa na Uturuki kwa sababu inawahesabu kama magaidi. Wakurdi hawa wana nia ya baadae kuungana na Wakurdi wenzao walioko Iraq na Uturuki ili kuunda taifa lao la Kurdistan. Hii ndio sababu ya kimsingi kuchukiwa na utawala wa Uturuki

Upande wa serikali uliongozwa na Balozi al-Jaafari ukajibu kwa kusema hilo halina tatizo, kwani pande zote zinapaswa zikubaliane  kama raia wa Syria. Jaafari ni balozi wa Syria huko UN. Yeye alisema Mistura ameshindwa kutoa orodha ya wapinzani watakaoshiriki katika mazungumzo. Hivyo kuna uwezekano mazungumzo haya yakashidikana kama ilivyokuwa wakati wa mazungumzo ya mwaka 2014
Mazungumzo yalichelewa kuanza kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wapinzani wa rais Bashar al-Assad.  Bw Mistura alishinikizwa na Marekani pamoja na Saudia, Uturuki na Qatar ambao walilazimisha kuwa HNC peke yao watambuliwe badala ya kuwaachia Wasyria wajiamulie wenyewe. Hii HNC iliundwa na utawala wa Saudia ili kuwakilisha wapinzani wote wa rais Assad

Wakamweka Riad Hijab kama kiongozi wa HNC. Huyu aliwahi kuwa waziri mkuu wa rais Assad. Inasemekana alishawishiwa na nchi za magharibi kujiunga na upinzani, baada ya kupewa sanduku la minoti kutoka majasusi wa Ufaransa

Msemaji mkuu wa HNC ni Mohammed Alloush, ambaye anaongoza kikundi cha Jaysh al-Islam, Hawa ni wafuasi wa madhehebu ya Wahabi ambao wanashirikiana kwa karibu na Al Qaeda kupitia kikundi cha Jabat al-Nusra pamoja na ISIL/Daesh

Kabla ya mazungumzo ya Geneva kuanza inaripotiwa kuwa ni kikundi hiki ndicho kilichoripua kwa mabomu msikiti wa Shia ulio karibu na Damascus. 

Watu 72 waliuawa. Halafu Marekani inadai kuwa eti Alloush na wenzake ni wapinzani wenye siasa ya wastani (moderate) Si ajabu upande wa serikali ya Syria na Urusi ulipinga kikundi hiki kushiriki mazungumzo ya Geneva
Haya ni mapigano ambayo yamekuwa yanaendelea kwa muda wa takriban miaka mitano sasa. Tayari watu zaidi ya 300,000 wamepoteza maisha yao na takriban milioni 9 hawana mahali pa kuishi. Watu milioni 4 wamekimbilia nchi za jirani kama Jordan na Lebanon. 

Sasa tunaona wengi wao wakiishia Ulaya ambako wanakamatwa na kupigwa. Wenyeji wa huko wamesema hata wapigwe risasi ili kuwazuia wasiingie. Nchi za Ulaya (NATO) ndizo zilizosababisha janga hili la Syria kama ilivyo huko Iraq, Libya, Afghanistan na Somalia. Wao ndio waliosababisha mamilioni ya wakimbizi na sasa wanasema hawahusiki kuwasaidia 
Ni vizuri tukaelewa kuwa hivi si vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ni vita vilivyoanzishwa na mataifa ya kigeni – Marekani (NATO) wakishirikiana na Saudia, Qatar, Jordan, Uturuki na Israel. 

Ndio maana wapiganaji zaidi ya 20,000 wameajiriwa kutoka zaidi ya nchi 60 ili kwenda “kuigomboa” Syria. Wengi wao ndio hawa ISIL au Daesh ambao wanashikilia maeneo kadha nchini Syria 
Mara nyingi huwa tunaambiwa kuwa ugomvi wa Syria unatokana na tofauti za kidini au kimadhehebu.  Ni kweli kuwa wakazi wa nchi hii wanafuata imani tofauti, lakini kwa muda wa karne nyingi watu hao wamekuwa wakiishi kwa amani bila ya migogoro. 

Sasa ghafla tunaambiwa, kwa mfano, eti Waislamu wa madhehebu ya Sunni na Washia hawapendani, au Waislamu wanawachukia Wakristo
Tuchue mfano mmoja ili kuonesha mahusiano yalivyo baina ya Waislamu na Wakristo
Mwaka jana ujumbe kutoka asasi za kiraia nchini Marekani ulitembelea Syria na ukaonana na watu kadha. Miongoni mwao ni mufti mkuu wa Syria, Sheikh Ahmad Badr Al-Din Hassoun  na Askofu Luca al-Khoury wa kanisa la Greek Orthodox 
Mufti Hassoun alisisitiza umuhimu wa kufikia muwafaka kwa njia ya mazungumzo baina ya wananchi wa Syria wenyewe bila ya kuingiliwa na wageni. Aliwasimulia wageni hao jinsi miaka mitatu iliyopita mwanaye wa miaka 22 alivyouawa. 

Kijana huyo ambaye hakuwahi kubeba silaha maishani mwake alikuwa akirudi nyumbani kutoka chuo kikuu wakati alipopigwa risasi na kuuliwa. Katika mazishi Mufti alitangaza kuwa anawasamehe wauaji hao na badala yake akaomba mshikamano wa wananchi wa Syria. 

Kisha mufti akamtaja Askofu Khoury kama “ndugu yangu”. Ndipo askofu aliposema alishangazwa na uamuzi wa serikali ya Marekani kumpa viza yeye asafiri hadi Marekani wakati wakimkatalia viza Mufti. Akasema: 
“Sisi wote ni viongozi wa kidini. Kwanini tubaguliwe?  Hii ni mbinu za Marekani kuwagawa Wakristo na Waislamu wa Syria. Ni sehemu ya mradi wao wa kuudhibiti utawala wa Syria ili waweze kujenga bomba la gesi litakalopita nchini mwetu”

“Kama serikali ya Syria ingewakubalia Wafaransa wachukue gesi yetu basi rais Hollande wa Ufaransa angemtembelea Rais Assad siku ya pili yake. Kama Syria ingekubali kudhibitiwa na Marekani basi rais Obama angemkumbatia rais  al-Assad na kumuita rais halali”
Askofu Khoury  akaongeza: “Tunashambuliwa na Uturuki kwa msaada wa kifedha kutoka Saudia na Qatar na msaada wa kisiasa kutoka Marekani na Ulaya (hasa Uingereza). 

Ndege zao zisizo na rubani (drone) kila siku zinawasaidia wavamizi kwa kuwaongoza” Viongozi hao wa kidini waliuambia ujumbe kutoka Marekani kuwa cha kufanya ni kuzuia silaha zisiingizwe nchini Syria. Walisema Marekani inapaswa kuwasilisha azimio katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kupiga marufuku uingizaji wa silaha zote nchini Syria na vita vitamalizika katika wiki moja.


Lakini Marekani na wenzake hawatafanya hayo. Badala yake wamekuwa wakiendesha propaganda kadha za kuichafua serikali ya Syria. Kwa mfano, mnamo Disemba na Januari mwaka huu vyombo vya habari vya magharibi vimekuwa vikisambaza “habari”  kuhusu mji mdogo wa Madaya wenye wakazi 9,330, ulio karibu na mji mkuu wa Damascus. 

Walituambia wakazi wa huko wamekuwa wakifa kwa njaa, pamoja na picha kama “ushahidi”. Wanasema eti ni kwa sababu majeshi ya Syria hayaruhusu chakula na madawa kupelekwa huko
Ukweli ni kuwa hizi ni propaganda zinazoendeshwa na wapinzani wa serikali ya Bashar al-Assad. Madaya ni mji mdogo karibu na milima. 

Tarehe 27 Disemba 2015 serikali ya Syria iliandika barua namba 3746 kwa mwakilishi wa UN nchini humo ikiomba msaada wa haraka na dharura, pamoja na madawa na chakula kwa wakazi wa Madaya na kwengineko   
UN ikatuma huko chakula cha msaada, lakini chakula hicho kikavamiwa na majeshi ya waasi na kwa hiyo UN ikashindwa kuendelea kusaidia. Haya yalithibitishwa na mwakilishi wa asasi ya Msalaba Mwekundu ambaye alisema waasi wanachukua chakula na kuwapa wapiganaji wao. Kilichobaki wanakiuza kwa bei ya juu. 

Haya yote yanafunikwa na badala yake tunaambiwa serikali inawaua raia wake kwa kuwapiga mabomu na kuwanyima chakula
Tukaambiwa wananchi wanakufa kwa njaa kwa sababu majeshi ya serikali yanazuia chakula kuingia.  Tukaonyeshwa picha za watu waliokondeana. 

Hizi ni picha za kupandikizwa. Kwa mfano,  picha moja ni ya msichana mwenye njaa eti “kutoka Madaya” (tinyurl.com/j8uzcc2) . Ukweli ni kuwa hii ni picha ya Mariana Mazeh anayeishi Lebanon kusini. Yeye mwenyewe alitangaza katika mtandao wa You Tube akikanusha kuwa anaishi Madaya, (tinyurl.com/z9vpwoa)

Halafu shirika la utangazaji la BBC lilitumia video kutoka Yarmouk ya mwaka 2014, ikidai ni kutoka Madaya. Na Al Jazeera nayo ikaonesha video ya mtu aliye na njaa kali, ikisema ni kutoka Madaya. Kumbe baadae ikagundulika kuwa ni picha ya ombaomba kutoka mitaa ya Ulaya iliyopigwa mnamo 2009 Shirika la VICE News linaloshirikiana na Fox news likasambaza picha za watoto wenye njaa kali eti kutoka Madaya. Baadae walilazimika kukubali kuwa zilikuwa picha feki. 

Picha moja ya msichana mwenye njaa ilipigwa nchini Lebanon na alikuwa na afya ya kutosha Tarehe 10 Januari shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu ambalo linashirikiana kwa karibu na Nyota Nyekundu nchini Syria lilitangaza kuwa habari za watoto wanaokufa kwa njaa huko Madaya hazijaweza kuthibitishwa rasmi. Inakuwaje basi habari, picha na video hizi feki zinasambazwa ulimwenguni kinyume na maadili ya uandishi?


Ni kwa sababu nchini Uingereza kuna asasi iitwayo uchunguzi wa haki za binadamu nchini Syria (Syrian Observatory for Human Rights - SOHR). Kazi yake kuu ni kusambaza hizo habari na picha kwa vyombo vya habari na mtandao wa jamii. Kwa kweli asasi hii ya SOHR inaendeshwa na Rami Abdulrahman mwenye duka la nguo mjini Coventry. Kazi hii anaifanya kutoka nyumbani kwake na ana uhusiano wa karibu na tajiri George Soros
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times huyu Rami anafadhiliwa na nchi za Ulaya pamoja na tajiri wa Marekani aitwaye George Soros. 

Pia ana uhusianao wa karibu na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza ambaye huwa anamtembelea mara kwa mara ofisini kwake. Hivi ndivyo ulimwengu unavyopatiwa “habari” kutoka Syria 
Sasa baada ya mazungumzo ya amani kukumbwa na matatizo, Bw Mistura ameamua kuwa mkutano mwengine ufanyike tarehe 25 mwezi huu. Hata hivyo alisema kuna haja kubwa ya maandalizi kufanyika kabla ya kuwakutanisha wajumbe wa pande mbili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani naye amesema kuna haja ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Huu ni msimamo tofauti na ule wa zamani walipokuwa wakisema wanataka serikali ya “mpito” bila ya Assad. 

Sasa wameacha kusema Assad ni lazima aachie madaraka, na badala yake anaweza kushiriki katika uchaguzi ili wananchi wa Syria wajiamulie utawala wanaoutaka.

nizar1941@gmail.com
0713-562181

No comments: