Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya saratani Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Jumuiya hiyo Mpendae ikiwa ni maadhimisho ya siku ya saratani duniani, kushotoni kwake ni Mkurugenzi wa Utumishi na uendeshaji Wizaraya ya Afya.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya saratani Zanzibar kwenye maadhimisho ya siku ya saratani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Utumishi na uendeshaji Wizaraya ya Afya Zanzibar ndugu Omar Mwinyi Kondo akizungumza na waandishi katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani yaliyofanyika Ofisi ya Jumuiya Mpendae, (kulia).
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani ndugu Omar Mwinyi Kondo (kati) mwenye suti na baadhi ya viongozi na waandishi wa habari waliohudhuria.
PICHA NA MAKAME MSHENGA/MAELEZO ZANZIBAR.
NA RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi ya Saratani Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani ameitanabahisha jamii kwamba maradhi ya saratani yamekuwa janga linalosumbua dunia nzima kwa sasa na kila mmoja anawajibu wa kusaidia katika kukabiliana na maradhi hayo sugu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Jumuiya hiyo Mpendae nje kidogo ya Mjini Zanzibar, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya saratani duniani, Dkt. Marijani amesema mtu anaweza kujikinga na maradhi hayo iwapo hatua za mapema zitachukuliwa.
Amezitaja hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi katika kukabiliana na saratani kuwa ni kujenga mwamko wa kuchunguza afya mara kwa mara ili kugundua mapema iwapo mtu anazo dalili za maradhi hayo.
Amesema hatua nyengine ni kuacha kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku, ulevi wa kupindukia, kupunguza matumizi ya mafuta kwenye chakula, kutumia zaidi vyakula vya matunda na mbogamboga na kujenga tabia ya kufanya mazoezi kila siku.
Dkt. marijani amewakumbusha wananchi kuwa saratani ni uvimbe mpya kwenye mwili na baada ya muda mfupi huzalisha chembechembe zinazosababisha athari kubwa na kama haikuwahiwa mapema inasababisha donda kubwa na kuwa halitibiki tena.
“Saratani inaweza kuzuilika iwapo itawahiwa mapema, tuongezeni nguvu kukabiliana nayo vyenginevyo inaweza kuathiri wananchi wengi kwani gharama ya matibabu yake ni kubwa na wagonjwa wengi hushindwa na kupoteza maisha,” alisisitiza Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Amesema saratani ya matiti na shingo ya kizazi ndizo zinaongoza kwa wanawake Zanzibar na saratani ya tenzi dume inaongoza kwa upande wa wanaume.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya maradhi ya Saratani Zanzibar, ambae ni Daktari bingwa wa uchunguzi wa saratani, amewaeleza waandishi wa habari kwamba mpaka hivi sasa hakuna takwimu rasmi za wagonjwa wa maradhi hayo Zanzibar lakini Hospitali ya Ocean Road ya Dar es salaam imekuwa ikipokea wagonjwa 1,000 kila mwaka kutoka Zanzibar mbali na wagonwa wengine wanaopelekwa nje ya nchi na wanaobakia majumbani kupatiwa dawa mbadala.
Amesema kutokana na kadhia hiyo mwaka 2013 ilianzishwa Jumuiya ya kupambana na saratani Zanzibar ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii juu ya njia za kujikinga na kuishauri serikali njia zinazofaa kupunguza ongezeko la maradhi hayo.
Ameitaka Serikali kuongeza wataalamu na dawa za kupunguza maumivu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja na hospitali nyengine za Zanzibar kwani zimekuwa hazitoshi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji Wizara ya Afya Ndugu Omar Mwinyi Kondo amewapongeza wanachama wa Jumuiya hiyo kwa juhudi kubwa wanayochukua kuelimisha jamii kujikinga na saratani.
Amewahakikishia viongozi wa Jumuiya hiyo kwamba Serikali itaanzisha utaratibu rasmi wa kuwasajili wagonjwa wa saratani na kuongeza huduma za matibabu Hospitali kuu ya Mnazimmoja hasa dawa za kupunguza maumivu na wataalamu.
ujumbe wa mwaka huu katika siku ya saratani duniani ni mimi na wewe tunaweza kujikinga na saratani.
No comments:
Post a Comment