Na Jumbe Ismaill, Singida
NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto amesema asilimia 15 ya wanawake wamegundulika kuwa wamekeketwa na kwamba takwimu hizo zinaonyesha pia kuwa ukeketaji huo umekithiri katika mikoa minane hapa nchini.
Naibu Waziri huyo,Dk.Hamisi Kigwangala ametoa takwimu hizo alipokuwa akifunga kongamano la siku ya kupinga vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake lililofanyika mjini hapa.
Alifafanua naibu waziri huyo kuwa takwimu hizo zinaonyesha kwamba ukeketaji huo umekithiri katika mikoa ya Manyara,Dodoma,Arusha,Singida pamoja na mkoa wa Mara na kwamba ukubwa wa tatizo hilo katika mikoa hiyo linatokana na imani na mila potofu.
“Kwa mujibu wa utafiti wa kidemografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa asilimia 15 ya wanawake wamekeketwa na kwamba takwimu hizo zinaonyesha ukeketaji umekithiri katika mikoa ya Manyara asilimia 71”alisema.
Aliitaja mikoa na asilimia zake kuwa ni mkoa wa Dodoma asilimia 64,Arusha asilimia 59,Singida asilimia 51 na Mara asilimia 40 huku akiweka bayana kuwa takwimu hizo zinaonyesha pia ukubwa wa tatizzo la ukeketaji katika mikoa ya Dar-es-Salaam,Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila mbali mbali kuhamia katika mikoa hiyo.
“Serikali inapinga,kulaani na kukemea tabia ya kuendelezwa kwa vitendo hivi vya ukatili unaomdhalilisha mtoto wa kike kwani unamsababishia madhara makubwa kiafya,kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo”alisisitiza Dk.Kigwangala.
Katika kuhakikisha kuwa suala la udhalilishaji kwa wanawake na watoto wa kike linazuiwa na kutokomezwa kabisa nchini,Dk.Kigwangala alibainisha kuwa serikali imesaini na kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda,maazimio na makubaliano mbali mbali yanayohusu haki na maendeleo ya watoto na wanawake.
Hata hivyo Naibu waziri huyo aliitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni pamoja na mkataba wa kimataifa wa Haki za mtoto wa mwaka 1989,Mkataba wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake wa mwaka 1989,mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za watu wa mwaka 1982 na itifaki yake ya nyongeza inayohusu wanawake wa Afrika wa mwaka 2003 inayopinga mila zenye kuleta madhara kwa binadamu kama vile ukeketaji.
Akitoa salamu za shukurani mara baada ya hotuba ya mgeni huyo,Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA,Edda Sanga aliweka wazi kwamba suala la harakati za ukeketaji ni harakati ambazo zimeweza kuleta machungu mengi katika jamii,jambo ambalo linahitaji msukumu mkubwa wa serikali.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo licha ya machungu yanayotokana na vitendo vya ukeketaji kunakosababisha vilio vya watu kutoka sehemu mbalimbali,lakini vilio peke yake havitasaidia chochote na kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuchukua hatua za kuhakikisha mila na desturi zilizopitwa na wakati zinatoweka kabisa nchini.
“Mheshimiwa Naibu waziri tulilia hapa machozi jana lakini kama unavyojua mheshimiwa waziri machozi hayatoshi ni lazima tuchukua hatua na hatua ndizo hizo ambazo umetuahidi hapa,jamani naomba tumpigie makofi mheshimiwa waziri”alisisitiza Sanga.
baadhi ya wanaharakati wa mapambano dhidi ya kupinga vitndo vya ukeketaji kutoka katika mikoa mitano ya Tanzania Bara waliohudhuria kongamano la siku mbili lililofaanyika mjini Singida.
No comments:
Post a Comment