Kampuni ya Koyo Corporation ya nchini Japan imeonesha nia ya kuwekeza nchini katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini kwenye kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Noria Shoji ambaye alifika wizarani hapo na ujumbe wake ili kujadili fursa za uwekezaji nchini hususan katika ufuaji umeme kwa gesi asilia.
Waziri Muhongo aliueleza ujumbe huo kwamba fursa za uwekezaji kwenye nishati hususan katika uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia ni nyingi na hivyo Serikali inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Koyo Corporation ya Japan, Norio Shoji wakati wa kikao cha kujadili fursa za uwekezaji nchini.
Alisema wawekezaji wanakaribishwa kujenga mitambo ya kufua umeme kwenye maeneo mbalimbali ambapo kuna matoleo ya gesi asilia na huku akiyataja maeneo hayo kuwa ni Mtwara, Lindi, Somangafungu na Mkuranga.
Waziri Muhongo alisema gesi asilia iliyogundulika ni ya kutosha kuzalisha umeme mwingi na hivyo wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye ufuaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia wanakaribishwa.
Awali, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya Koyo, Norio Shoji alisema lengo la ujio wake na ujumbe alioongozana nao, ni kutafuta ukweli wa mambo kuhusiana na masuala ya uwekezaji kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia.
Wajumbe wa mkutano baina ya Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya Koyo Corporation ya Japan ukiongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati).
“Tulikuwa katika mkutano mkubwa nchini Japan na tukaelezwa na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Batilda Burian kwamba Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji katika uzalishaji wa umeme. Sasa tumekuja kujionea hali ilivyo pamoja na kuzungumza na wahusika,” alisema Shoji.
Alisema awali kampuni yake haikuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na uwekezaji nchini na hivyo aliahidi kwamba ifikapo tarehe 1 mwezi Juni mwaka huu, Kampuni yake itawasilisha pendekezo rasmi la uwekezaji wa uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia.
“Nimefurahishwa sana na namna Waziri mwenye dhamana anavyoielezea sekta husika; tumehamasika kuwekeza hapa. Tumedhamiria kwamba ifikapo tarehe 1 mwezi Juni, tutarudi na pendekezo rasmi,” alisema.
Wakizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa na Naibu wake, Dkt. Juliana Pallangyo waliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kunakuwepo na umeme mwingi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na wawakilishi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Baadhi ya wajumbe kutoka kampuni ya Koyo Corporation ya Japan; wa kwanza kulia ni Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji, Norio Shoji, akifuatiwa na Mshauri wa Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji, Serge Edongo na Mkurugenzi Mtendaji, Naoto Umeda.
Ujumbe kutoka kampuni ya Koyo Corporation ya Japan ukiongozwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji, Norio Shoji (wa kwanza kulia).
Baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo waliohudhuria kikao baina ya wizara na kampuni ya Koyo Corporation ya Japan. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akifuatiwa na Katibu Mkuu Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa na Naibu wakeanayeshughulikia masuala ya nishati, Dkt. Juliana Pallangyo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), kushoto kwake ni Katibu Mkuu Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akifuatiwa na Naibu wake anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt Juliana Pallangyo na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile
No comments:
Post a Comment