Thursday, January 14, 2016

KATIBU MKUU NISHATI NA MADINI AFANYA ZIARA GST NA CHUO CHA MADINI

Na Veronica Simba – Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).

Ziara hiyo iliyofanyika jana Januari 13, 2016 mjini Dodoma, ziliko Taasisi hizo, ililenga kujitambulisha kwa viongozi na watumishi pamoja na kujionea kazi na huduma mbalimbali wanazotoa kwa wananchi.

Katibu Mkuu alikutana na viongozi wa GST na wa Chuo cha Madini ambapo alipokea taarifa ya utendaji, kisha akakutana na wafanyakazi wote wa Taasisi hizo na kuzungumza nao kuhusu majukumu yao na changamoto walizonazo kiutendaji.

Baada ya kukutana na Wafanyakazi, Katibu Mkuu Ntalikwa alitembelea majengo mbalimbali ya Wakala kujionea kazi zinazofanyika ambapo ni pamoja na Maabara mpya ya kisasa ya Uhandisi wa Kijiolojia, Chumba chenye mitambo na mashine za kisasa zinazohifadhi data mbalimbali, chumba maalum kinachohifadhi nyaraka na machapisho mbalimbali pamoja na Maabara ya kuchenjua Madini (Mineral processing Laboratory).

Ziara ya Katibu Mkuu Ntalikwa katika Ofisi za GST na MRI ni mwanzo wa ziara anayofanya kutembelea Mashirika na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ili kujitambulisha na kujionea kazi na huduma wanazotoa. Profesa Ntalikwa ataendelea na ziara mjini Dodoma kwa kutembelea Ofisi za Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Ofisi za Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).
Mtumishi katika Maabara ya Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Kamana Camilius (mwenye Koti la Bluu) akimweleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (wa pili kutoka Kulia) namna Maabara hiyo inavyofanya kazi. Wengine pichani ni Viongozi wa GST.
Mtumishi katika Maabara mpya ya kisasa ya Uhandisi wa Kijiolojia inayomilikiwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Godson Kamihanda (wa pili kutoka Kushoto) akimweleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (katikati) namna Maabara hiyo inavyofanya kazi. Wengine pichani ni Viongozi wa GST.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (mbele) akikagua Jengo jipya la Ofisi ya Madini – Dodoma. Pamoja naye pichani ni Viongozi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST). Jengo hilo lipo jirani na Ofisi za GST.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akisaini Kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Chuo cha Madini Dodoma (MRI) alipotembelea Chuoni hapo hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akisalimiana na Watumishi wa Chuo cha Madini Dodoma (MRI) alipowasili ofisini kwao kuwatembelea na kuzungumza nao hivi karibuni. Kulia kwa Katibu Mkuu ni Mkuu wa Chuo, Ofolo Ngowi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (mwenye suti ya Bluu – katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wafanayakazi wa Chuo cha Madini Dodoma, alipowatembelea na kuzungumza nao hivi karibuni. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo, Profesa Abdulkarim Mruma na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo, Ofolo Ngowi.
Mkuu wa Maabara ya Madini inayomilikiwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Heri Issa (wa pili kutoka Kulia) akimweleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Ntalikwa (katikati) namna Maabara hiyo inavyofanya kazi. Wengine pichani ni viongozi na watumishi wa GST.

No comments: