Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifunua pazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unaguja.
Balozi Seif pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr. Omar Dadi Shajak wa kwanza kutoka kulia na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hijja nyuma yake wakifurahia na kupiga kofi mara tu baada ya Balozi Seif kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana hapo Kidimni.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr. Shajak wa pili kutoka kushoto akimpatia maelezo Balozi Seif wa kwanza kutoka kushoto jinsi ya ujenzi wa kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana utakavyoendelea hapo Kidimni.Wa Pili kutoka kulia ni Mkandarasi wa ujenzi huo kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Nd. Mbwana Bakari juma.
Baadhi ya wananchi walioshiriki hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni Wilaya ya Kati.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr. Omar Dadi Shajak akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana hapo Kidimni Wilaya ya Kati.
Balozi Seif akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana ikiwa ni shamra shamra za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika sasa katika kuona Wananchi wanalazimika ipasavyo kutoa mashirikiano ili kusaidia kufanikisha ile azma ya Serikali Kuu ya kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya Nchini.
Amesema kuwa kukosekana ushirikiano katika kutoa ushahidi Mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya ambako kunawahusu zaidi Wananchi walio karibu na wahusika hao inapelekea kufutwa kwa kesi na hivyo kudumaza juhudi za Serikali katika vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo.
Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unaguja ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964.
Amesema suala la Dawa za kulevya hivi sasa limekuwa janga la Dunia kwa vile ni la muda mrefu na kuathiri watu wengi hasa Vijana. Hivyo udhibiti wa matumizi yake unahitaji maamuzi magumu ya Serikali pamoja na ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Dunia kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi walioanzisha nyumba hizo pamoja na Vijana wanaoishi kwenye nyumba hizo kujitahidi kutoshawishika kurudi nyuma kwa kujiingiza tena katika janga la matumizi ya dawa za kulevya.
Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr.Omar Dadi Shajak alisema ujenzi wa kituo hicho unagharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Nne na Milioni Mia Mbili { 4,200,000,000/- } hadi kukamilika kwake.
Dr. Shajak alisema Kituo hicho cha aina yake ndani ya ukanda wa Mwambao wa Afrika Mashariki kitakuwa na uwezo wa kuhudumia Vijana wapato 200 wake kwa waume kwa wakati mmoja ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na mafunzo ya kazi za amali, michezo na huduma nyengine za kurekebisha tabia.
Dr. Omar Dadi Shajak amewafahamisha kwamba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya tayari imeshaandaa zawadi kwa Mtu au Kikundi kitakachojitolea kutoa Taarifa ya kukamatwa kwa wahusika wa dawa za kulevya.
Ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya hapo Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja chenye eneo la ukubwa wa Eka Tatu kinajengwa na Kampuni ya Kizalendo ya Al – Hilal General Trading Cooperation Limited chini ya Mkandarasi Mbwana Bakari Juma kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 5/1/2016.
No comments:
Post a Comment