Sunday, December 20, 2015

Rais Magufuli atuma salamu za Rambirambi kufuatia kifo cha Askofu Nkalanga



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
      IKULU,
 1 BARABARA YA BARACK OBAMA,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu Plasdus Gervas Nkalanga (OSB) kilichotokea Ijumaa tarehe 18 Desemba, 2015 katika hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho, Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

Mhashamu Askofu Nkalanga aliyekua Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba alistaafu uaskofu mwaka 1974 na kujiunga na watawa wabenediktini wamonaki ambapo aliamua kwenda kuishi katika Abasia ya Hanga iliyopo katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.  

Katika salamu zake Rais Magufuli amesema  Askofu Nkalanga aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96 atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kuhimiza imani na uchapakazi kazi katika kipindi chote cha miaka 54 ya uaskofu wake na utawa wake akiwa katika Abasia ya Hanga.

Amesema Marehemu Askofu Nkalanga ambaye baada ya kustaafu aliamua kuingia katika utawa akianzia katika ngazi ya chini kabisa ya Unovisi hadi alipofunga nadhili za milele za utawa mwaka 2009, ameacha mfano mzuri unaohimiza jamii kuishi kwa upendo, unyenyekevu na kutokata tamaa. 

"Kupitia kwako Baba Askofu Ngalalekumtwa napenda kuwapa pole nyingi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Abate wa Abasia ya Hanga, watawa na waumini wote wa kanisa Katoliki kwa kupoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla" amesema Rais Magufuli.

Rais John Pombe Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu Mhashamu Askofu Mstaafu Plasdus Gervas Nkalanga mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU



20 Desemba, 2015

No comments: