Na Rahma Khamis /Miza Othman -Maelezo Zanzibar.
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) wamewataka Viongozi wa Mashirika ya Vyama vya Michezo Tanzania kusaidiana na wanamichezo mbalimbali ili kufikia hadhi ya kimataifa .
Hayo yameelezwa na na Katibu mtendaji wa TOC Jamal Nassor Adi huko Kituo cha Utengamano Welezo Zanzibar wakati alipokua akifungua Mkutano mkuu wa mwaka wa Kamisheni ya Wachezaji Tanzania . Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuhamasisha na kuamsha ari kwa Wachezaji ili kuweza kurejesha hadhi ya Michezo Tanzania.
Katibu Jamal amefahamisha kuwa wachezaji ndio wahusika wakuu wa michezo hivyo ni lazima kushirikishwa na kupatiwa elimu ili kuweza kufahamu wajibu wao katika michezo na kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Akizungumzia suala la dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo, Katibu Jamal amesema ni vyema wachezaji kuzifahamu na kujiepusha nazo kwani kitendo hicho kinaweza kupelekea nchi kupigwa marufuku kushiriki michezo ya Kimataifa. Nae Katibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania Filbert Bayi amesema kuwa michezo ni chanzo cha kujipatia ajira kwa vijana hivyo ni vyema michezo iendelezwe ili kuleta maendeleo kwa wachezaji wenyewe na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema katika kuimarisha michezo Nchini suala la kuteuliwa wawakilishi wenye uwezo ni jambo muhimu na amewashauri washiriki wa mkutano huo kusaidia ili kupunguza malalamiko.
Mwenyekiti wa Kamsheni ya Wachezaji Tanzania (KAWATA) Ramadhani Zimbwe ameahidi kupambana na rushwa kwa viongozi na watendaji wa michezo nchini kwani vitendo hivyo vinarudisha nyuma ufanisi wa michezo.
Amesema rushwa ni adui wa haki na mara nyingi hupelekea mtu mwenye uwezo wa kifedha kupata haki asiyostahiki na kumuacha mwenye haki hiyo kuikosa kutokana na kukosa fedha.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya wachezaji Tanzania (KAWATA) Ramadhan Zimbwe akizungumza na Wanamichezo mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi akizungumza na wana Michezo mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka waliohudhuria katika Mkutano huo wakisikiliza maelezo kwa Mgeni Rasmi Katibu Mkuu msaidizi Jamali Nassor Adi hayupo pichani.
Mgeni Rasmi Jamal Nassor Adi akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa kamisheni ya Wachezaji Tanzania (KAWATA) katika Ukumbi wa Kituo cha Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.
Washiriki wa Kamisheni ya Wachezaji waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Mwaka.
Wajumbe wakiwa katika picha ya Pamoja.
PICHA NA ABDALLA OMAR –HABARI MAELEZO.
No comments:
Post a Comment