Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi ( picha ya Maktaba) ametoa wito kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Ofisi zake kutekeleza kwa vitendo dhana ya uwazi na uwajibikani kama yanavyozishikiza Nchi Wanachama, kwa kile alichosema, utekelezaji wa dhana hiyo haupashwi kuwa jukumu la Serikali peke yake. Ametoa wito huo wakati wa majadiliano ya Ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu iliyowasilishwa siku ya jumatatu mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa wito kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwamo Baraza la Haki za Binadamu kuitekeleza kwa vitendo dhana ya uwazi na uwajibikaji.
Tanzania imesisitiza pia kwamba, haitoshi kwa Mashirika hayo kuzitaka nchi wanachama kwa maana ya serikali kuwajibika na kuwa wazi katika utekelezaji wa majukumu yake ili hali yenyewe yanafanya kinyume.
Wito huo umetolewa siku ya Jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Ripoti ya Mwaka ya Baraza la Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Manongi ambaye alikuwa miongoni mwa Mabalozi kati ya wengi waliochangia Ripoti hiyo iliyowasilishwa na Rais wa Baraza la Haki za Binadamu Bw.Joachim Rucker .Amesema, Tanzania inatoa wito huo kutoka kile kinachoonekana dhahiri kwamba ama Mashirika hayo yamekuwa yakionyesha kuegemea upande mmoja dhidi ya mwingine au kupendelea nchi moja dhidi ya nyingine kitendo ambacho kinakwenda kinyume na kile wanachokihubiri.
Akatoa mfano kwa kusema, wakati Rais wa Baraza la Haki za Binadamu akisisitiza katika ripoti yake umuhimu wa uwajibikaji, Ofisi ya Haki za Binadamu katika mwezi Octoba ikishirikiana na UNICEF na Canada, ilidhamini onyesho la Filamu kuhusu kijana kutoka Geita mwenye alibinisim, pasipo Taasisi hiyo kuujulisha Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania ili hali wakijua Tanzania ilikuwa mlengwa wa filamu hiyo.
“ Akiwasilisha Taarifa yake mbele ya Baraza hili mwanzoni mwa mkutao huu, Raisi wa Baraza la Haki za Binadamu amesisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji. Cha kusikitisha tukio la konyeshwa kwa filamu ambayo maudhui yake yalihusu Tanzania na sisi kama Tanzania hatukujulishwa, hakika inakwenda kinyume kabisha na dhana ambayo Rais wa Baraza la Haki za Binadamu amekizungumza hapa” akasema Balozi Manongi.
Na kuongeza “ ndiyo maana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa wito kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa au Ofisi zake kuonyesha kwa vitendo dhana ya uwazi, uwajibikaji na kutoegemea upande wowote”.
Akabainisha kuwa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa hayapashwi kujionyesha kuwa yanaegemea upande wowote au hata kupendelea baadhi ya nchi wanachama dhidi nchi nyingine na hasa pale ambapo Mashirika hayo binafsi hayajapitia na kujiridhisha juu ya kile ambacho wanataka kukiunga mkono au kutaka kujihusisha nacho.
Akaeleza Zaidi mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania haikupinga na wala haipingi filamu kuhusu kijana wa Geita, filamu iliyolenga katika kuonyesha changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino nchini Tanzania.
“ Tulichopinga na tunachopina ni maelezo yaliyoandikwa na muandaaji wa filamu hiyo, maelezo ambayo yalikuwa na upotoshaji mkubwa. Kwa mfano, baadhi ya maelezo ya filamu hiyo yanasema, hakuna utashi wa kisiasa kutoka Serikali ya Tanzania katika kukabili uovu wanaotendewa watu wenye ualibino.
Kwamba, msukumo kutoa mataifa ya nje ni wa lazima ili kutokomeza uovu huo, kwamba ujinga ni laana kubwa inayowakabili waaafrika na jawabu pekee ni kuwaelimisha, kwamba filamu hiyo ilikuwa ni kuwashawishi watu wa nje ili kuleta mabadiliko ya kweli. Na vilevile filamu hiyo ilikuwa ni kusherehekea roho ya utu na kazi nzuri inayofanywa na watu wa Canada katika kuwasaidia watu wenye ualibino” akasisitiza Balozi Manongi.
Akasema Baloz, Ni kwa kuzingatia upotoshaji huo na mwingine ulioelezwa na muandaaji wa filamu hiyo, haishangazi kuona kwamba Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania haukualikwa kufadhili onyesho la filamu hiyo iliyoonyeshwa Umoja wa Mataifa.
“ Rais wa Baraza la Haki za Binadamu pia amezungumzia wajibu wa Asasi za Kijamii katika uhamasishaji wa haki za Binadamu. Tunakubaliana na pendekezo wake. Wakati tunauga mkono mchango wa Asasi za kijamii, ni lazima basi Asasi hizo nazo zikaonyesha uwajibikaji na uwazi pamoja na kujipambanua katika utekelezaji wa majukumu yao. Uwajibikaji hauwezi kuwa ni jukumu la serikali peke yake” akasisitiza Balozi Manongi.
Akizungumzia Zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino, Mwakilishi huyo wa Tanzania, amesema, Tanzania kwa kutambua changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi pamoja na upatikanaji wa haki za msingi kwa watu wenye ualibino ndiyo maana kwa kushirikiana na Malawi imeamua kuwasilisha mbele ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Azimio kuhusu watu wenye ualibino.
Amesema dhumuni kuu la Azimio hilo na ambalo linatarajiwa kupitishwa wiki hii ni kupanua wigo na ushiriki mpana wa wadau mbalimbali ukiwamo Umoja wa Mataifa katika kuzikabili changamaoto zinazowakabili watu wenye ualibino.
Na kwa sababu hiyo, Balozi Manongi ameziomba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuunga mkono azimio hilo pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania pamoja na Chama cha Watu wenye Ualibino Tanzania (TAS) katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino vikiwamo vitendo vya kikali wanavyofanyiwa na watu wasio na mapenzi mema.
No comments:
Post a Comment