Tuesday, October 20, 2015

TUZO ZA UANDISHI MAHIRI 2015 ZAJA

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Baraza zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam.

KAMATI za maandalizi ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) iliyopo chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) imezindua rasmi tuzo hizo ambazo zimeongezewa makundi mawili ya kushindania.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Baraza zilizoko Mwenge Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, amesema makundi mapya ya kushindaniwa katika shindano la mwaka huu, ni habari za kodi na ukusanyaji mapato, na habari za manunuzi ya umma.

Amesema kwa maana hiyo, tuzo zitakazotolewa katika shindano safari hii zitakuwa 22.

Mukajanga ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mandalizi ya Tuzo, ametaja makundi mengine kuwa ni habari za uchumi na biashara; mazingira; afya; michezo; ukimwi; utawala bora; michezo; jinsia; sayansi/teknolojia.

Makundi mengine ni habari za afya ya mama na mtoto; uchunguzi; elimu; watu wenye ulemavu; utalii na uhifadhi; katuni bora; kilimo; afya ya uzazi kwa vijana; gesi; mafuta; na uchimbaji wa madini.

Amesema makundi mawili mapya yamelenga kuhamasisha waandishi wa habari kuandika habari zinazohusu umuhimu wa kulipa na kukusanya kodi na tuzo ya masuala ya manunuzi ya umma kuwaongezea ari waandishi kupenda kufuatilia namna serikali na asasi zake zinavyopata huduma mbalimbali.

“Haya ni masuala yanayohimiza uwajibikaji katika sekta ya umma. Ni maeneo ambayo waandishi wengi bado hawajayachangamkia katika kuyachunguza, labda hawajui ni maeneo yanayoigharimu serikali fedha nyingi za wananchi,” amesema Mukajanga.

Kuhusu uwasilishaji kazi, waandishi wametakiwa kupeleka kazi zao kuanzia hiyo jana Oktoba 16 mpaka Februari 15 mwakani. Kazi zote zipelekwe ofisi kuu za MCT.

Mukajanga amesema kilele cha shindano kitakuwa Aprili 29, 2016 watakapokabidhiwa washindi tuzo zao zikiwemo vyeti, fedha taslimu vifaa vya kufanyia kazi kwa waandishi wa habari.

Katika hatua nyingine, Mukajanga amewataka waandishi wa habari kuwa makini katika kazi zao hasa kipindi cha uchaguzi ambao kura itapigwa Oktoba 25 (Jumapili wiki ijayo).

Meneja Udhibiti na Viwango MCT, Pili Mtambalike ambaye alihudhuria mkutano huo wa waandishi wa habari, amesema vipengele vya kushindaniwa hubadilika kila mwaka kutokana na kupata mawazo ya kuimarisha utoaji wa tuzo kwa waandishi mahiri.




“Kumekuwa na kudorora kwa baadhi ya vipengele hasa ‘habari za uchunguzi na ufuatiliaji’ kutopata waandishi wengi. Miaka iliyopita baadhi ya vipengele tulipokea kazi tano hata nne wakati nyingine zinakuja hata 1,000 na kuendelea. Waandishi leteni kazi za aina zote,” amesema Mtambalike. 

No comments: