NA BASHIR YAKUB
Ni kawaida watu kukopeshana fedha katika shughuli za kibinadamu za kila siku hasa zile za uzalishaji. Ni kutokana na hili baadhi ya watu hujikuta wameingia katika faraka ambazo hata hivyo zinatatulika kisheria. Kwa wale ambao madeni yao hutokana na taasisi za fedha kama benki hawa huwa sio rahisi kwao kukwepa kutokana na utaratibu makini wa utoaji wa fedha wa taasisi hizo. Tatizo kubwa la kutolipana na kuleteana dharau huhusisha wadeni binafsi yaani mtu na mtu. Ni katika madeni haya ya watu binafsi ambamo msemo maarufu wa deni halifungi husikika. Ni kawaida kukuta mtu amekopeshwa na hataki kurejesha akijiamini kuwa deni halifungi. Yumkini wapambe nao husikika wakisema, asikutishe huyo deni halifungi. Kwa makala haya tutapata kujua ikiwa ni kweli deni linafunga au halifungi.
1.KESI YA MADAI.
Kesi za madai ni zile kesi zote ambazo si za jinai. Kesi za madai hazihusishi kudaiana pesa tu kama wengi wanavyojua. Hata masuala ya talaka, kudai fidia, mikataba, madai ya vitu kama nyumba, magari n.k navyo huingia katika kesi za madai. Kwa hiyo tunapojiuliza swali la ikiwa deni linafunga au halifungi tunaongelea hivi vyote. Hata hivyo tutajielekeza zaidi katika kudaiana fedha.
2. JE INARUHUSIWA KUPELEKA KESI YA MADAI POLISI ?.
Unayo haki ya kufungua shauri ikiwa kuna mtu unamdai lakini kwa sharti kuwa shauri lifunguliwe pahala stahiki. Wapo ambao hupeleka kesi za namna hii polisi japo huko si mahali pa kesi za namna hii. Polisi hujitahidi kuzitafutia ufumbuzi ambapo wakati mwingine hufanikiwa na wakati mwingine hushindwa. Ukweli ni kuwa kisheria polisi hawana ruhusa ya kushughulikia kesi za madai hasa hizi za kudaiana hela na hata mali. Ni basi tu wanaamua kuzishugulikia lakini si kazi yao kisheria. Madhara utakayoyapata utakapomfungulia kesi mdai wako polisi ni pamoja na kupoteza mda bila kupata ulichokitaka. Hii ni kwasababu mdaiwa atakapokataa kutoa ushirikiano wowote, polisi hawana la kumfanya.
Hawawezi kumfunga kwasababu hairuhusiwi. Hawawezi kumpeleka mahakamani kwasababu hawaruhusiwi kupeleka kesi za madai mahakamani. Kwahiyo mdaiwa uliyempeleka polisi akiamua kukomaa hawana la kufanya utakuwa umepoteza muda na gharama.
Basi ieleweke kuwa kesi za madai kama haya hutakiwa kufunguliwa mahakamani. Yaweza kufunguliwa mahakama yoyote kutegemea na kiwango cha fedha unachodai. Waweza kufungua mahakama ya mwanzo, ya wilaya na hata mahakama kuu. Usipeleke kesi ya namna hii polisi labda kama unalenga kumtisha mdeni na si kupata haki.
3. JE DENI HALIFUNGI KISHERIA ?
Hapana, deni linafunga, Ikiwa utashitakiwa kwa kudaiwa fedha na hukumu ikatolewa kuwa unatakiwa kulipa hizo fedha basi unatakiwa uzilipe. Ikiwa hauna basi itaangaliwa kama una mali kama nyumba, gari au mali yoyote ambayo inaweza kukamatwa ili kulipia deni. Ikiwa hauna nyumba , gari au mali nyingine yoyote inayoweza kufidia deni basi itatakiwa ukamatwe ufungwe kwa ajili ya deni hilo. Kifungu cha 44 ( 1 ) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai kinasema kuwa mdaiwa anaweza kukamatwa katika muda na siku yoyote , na haraka kufikishwa mahakamani , na kuwa mahakama inaweza kutoa amri ya kuwekwa kizuizini/kufungwa. Kwa hiyo deni linafunga labda mdai asiamue kuchukua hatua.
4. JE UKIFUNGWA DENI LINAISHA ?.
Hapana ukifungwa deni haliishi. Kifungu cha 46 ( 2 ) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai kinasema kuwa mdaiwa aliyeondolewa katika kifungo kwasababu yoyote ile, iwe kwa kumaliza muda, ugonjwa au vinginevyo hatahesabika kuwa ameondolewa katika deni kutokana na kuachiwa huko. Hii ina maana unatumikia kifungo kikiisha deni linabaki palepale.
Kifungo hakifuti au kusimama badala ya deni isipokuwa ni adhabu ya ukorofi. Ni kutokana na mtazamo huo wa sheria unaolazimisha kutakiwa kulipa deni hata baada ya kutumikia kifungo. Ukishindwa mara nyingine tena kulipa mdai anayo haki ya kukurudisha tena mahakamani ambapo unaweza kufungwa tena. Msimamo wa sheria ni mpaka ulipe tu.
5. KULIPIWA DENI UKIWA JELA.
Muda wowote mdaiwa akiwa jela anatumikia adhabu yake ya deni anaweza kuondolewa na kufutiwa adhabu hiyo iwapo kiwango cha deni analodaiwa kitalipwa. Mahakama iliyotoa amri ya kufungwa ndiyo itakayotoa amri ya kuachiwa baada ya deni kulipwa katika ukamilifu wake.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment