Friday, October 23, 2015

MAALIM SEIF AKUTANA NA MASHEIKH

  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Viongozi wa Taasisi za Kiislamu katika ukumbi wa Baitul-Yamin, Malindi mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Kiislamu Zanzibar wakimsikiliza Maalim Seif.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiitikia dua baada ya mazungumzo yake na viongozi hao wa dini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na viongozi hao wa dini baada ya mazungumzo yao. 
(Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameahidi kushirikiana na taasisi zote za dini nchini sambamba na kuziendeleza madrasa za Kur’an, ili ziendane na wakati uliopo.

Maalim Seif ambaye pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi CUF ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa taasisi za Kiislamu katika ukumbi wa Baitul-Yamin Malindi mjini Zanzibar.

Amesema Serikali atakayoiongoza iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar itashirikiana kwa karibu na taasisi hizo ili kuona kuwa michango yao inasaidia kuchangia juhudi za maendeleo na ustawi wa Zanzibar.

Amewataka viongozi hao wa dini kudhibiti tofauti ndogo ndogo za kimadhehebu, ili zisiwe chanzo cha kuvuruga umoja wa waislamu nchini.

Sambamba na hilo Maalim Seif amesema bado madrasa za Kur’an hazijapewa umuhimu unaostahiki, na kuahidi kulishughulikia suala hilo ili kuzijengea mazingira bora na kuangalia maslahi ya walimu wa madrasa hizo.

Amesema iwapo atachaguliwa kuongoza nchini, Serikali yake itatoa mchango wake katika kuziendeleza madrasa ili ziwe za kisasa kwa kuzipatia mahitaji yote ya msingi yakiwemo vikalio pamoja vifaa vya kusomea.

Amewakumbusha walimu wa madrasa kuweka mbele maendeleo ya watoto kwa kuwajenga kimaadili, ili waweze kuwa raia wema na viongozi bora wa baadae.

Mapema akizungumza kwa niaba ya viongozi wa taasisi hizo za Kiislamu, Sheikh Khamis Yussuf amesema taasisi hizo ziko tayari kuzungumza na kushirikiana na kiongozi yeyote wa serikali kwa lengo kuweka mustakbali mwema wa Zanzibar.

Amewaomba viongozi wa Serikali kutoa ushirikiano katika kuulinda na kuuendeleza utamaduni wa Zanzibar ili usiharibiwe na tamaduni nyengine, na kwamba utamaduni ni rasilimali muhimu kwa taifa.

Wiki iliyopita Maalim Seif alikutana na viongozi wa dini ya kikristo waliopo Zanzibar katika kituo cha utengamano Welezo, kuzungumzia juu ya umuhimu kutunza na kuilinda amani ya Zanzibar. 

No comments: