Tuesday, September 22, 2015

WANAOWAFICHA WATOTO WALEMAVU NCHINI WASHUGHULIKIWE

(Meneja msaidizi wa kituo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation Centre,Sophia Moshi akibadilishana mawazo na meneja mkuu wa kituo hicho,Claus Heim).
 
Mahmoud Ahmad, Arusha
SERIKALI imeombwa kuchukua hatua kali kwa baadhi ya wazazi nchini wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemavu hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakose mahitaji ya msingi kama elimu na afya.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na uongozi wa chuo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation Centre  huku wakiiomba serikali iviangalie vituo vya kulea watoto walemavu kwa kuvipatia ruzuku .

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili chuoni hapo,meneja wa chuo hicho,Claus Heim alisema kwamba serikali inapaswa kuhakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemevu majumbani.

Alisema kwamba serikali inapaswa kuweka sheria kali na kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwapa fursa watoto wenye ulemavu nchini kupata huduma za msingi kama elimu,afya,chakula  pamoja malazi.

“Hawa wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu nchini je wanachukuliwa hatua gani?kila mtoto ana haki ya elimu na afya lakini nani anawajibika”alihoji Heim ambaye ni raia wa nchini ujerumani

Hatahivyo,meneja msaidizi wa kituo hicho,Sophia Moshi kwa upande wake alisema kwamba ni wajibu wa serikali kuhakikisha inavipatia ruzuku vyuo vya ulemavu nchini ili viweze kujiendesha kwa kuwa vinakabiliwa na changamoto lukuki.

Alisema kwamba mtoto mwenye ulemavu ana uwezo kama mtoto mwingine na hivyo kuitaka jamii kuwathamini watoto wenye mahitaji maalumu badala ya kuwanyanyapaa.

Mbali na kauli hiyo Moshi alisema kwamba chuo chao kimejipanga kujenga shule ya sekondari kwa lengo la kuongeza mapato ya kuendesha chuo hicho badala ya kutegemea wafadhili ,kusajili kituo cha afya kwa ajili ya matibabu ya mguu kifundo(club foot) sanjari na kusajili chuo cha ufundi chuoni hapo.

Chuo hicho kilianzishwa mnamo mwaka 1988 na kinasimamiwa na kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) Dayosisi ya Meru  ,kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 74 walemavu ambao ni wasichana na wavulana ambapo nchi ya ujerumani ndiye mfadhili mkuu kwa sasa.

No comments: