Tuesday, September 22, 2015

CCM NDIO CHAMA KINACHOPENDWA ZAIDI NA WANANCHI

TAKWIMU zinaonyesha kwamba wananchi hawaelewi nafasi rasmi ya Ukawa
22 Septemba, Dar es Salaam: Asilimia 62 ya wananchi wanasema kwamba wanajisikia wapo karibu zaidi na chama cha CCM kuliko vyama vingine. 
 
Aidha, walipoulizwa watawachagua wagombea wa chama gani – bila kutajiwa majina ya wagombea – wananchi 6 kati ya 10 walisema kwamba watawachagua wagombea wa CCM kwa Urais (66%), Ubunge (60%) na Udiwani (60%). Takwimu hizi zinatoa picha kwamba CCM inaungwa mkono, kama ilivyokuwa mwaka 2012.

Chadema ni chama cha pili kinachopendwa kushinda vyama vingine vya upinzani. Lakini wananchi wanaosema kwamba watawachagua wagombea wa Chadema kwa Urais, Ubunge na Udiwani wamepungua kidogo. Ikumbukwe kuwa, inawezekana wananchi wanaopenda zaidi mseto wa Ukawa waliunga mkono vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi au NLD.

Mbali ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa, chama cha ACT-Wazalendo kilitajwa na zaidi ya asilimia moja ya wananchi.

Walipoombwa kutaja moja kwa moja jina la mgombea Urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea wa CCM, John Magufuli. Asilimia 25 walimtaja mgombea wa Chadema (na Ukawa), Edward Lowassa. Asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya wale waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea waliyempendelea. Hata hivyo, takwimu zilikusanywa kabla vyama vingine, kikiwemo ACT-Wazalendo, kuteua wagombea wao wa Urais. Takwimu hizi (zilizokusanywa kati ya Agosti na Septemba) sio utabiri wa matokeo ya uchaguzi. Zinaonyesha tu kwamba mwanzoni mwa kipindi cha kampeni, mgombea Urais wa CCM, John Magufuli, alikuwa anaongoza katika kura za maoni.

Aidha, vigezo muhimu vinavyohusu makundi mbalimbali ya watu (demografia) vilitumika kuchambua ni nani au makundi gani yanayowaunga mkono John Magufuli na Edward Lowassa. Wahojiwa ambao walikuwa vijana zaidi, wasomi zaidi, wanaume na wakazi wa mijini, walimuunga mkono Edward Lowassa. Makundi ya wahojiwa wazee zaidi, waliokuwa na elimu ya msingi tu, wanawake na wakazi wa vijijini walielekea kumuunga mkono zaidi John Magufuli kuliko vijana zaidi, wasomi zaidi, wanaume au wanaoishi mijini.

Hata hivyo, katika makundi yote haya, John Magufuli wa CCM anaonekana kuongoza. Kwa mfano, asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50. Pamoja na hayo, asilimia 57 ya watu wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 76 ya watu wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Magufuli. Upande wa makazi, asilimia 28 ya wakazi wa mijini walimuunga mkono Edward Lowassa tofauti na asilimia 24 ya wakazi wa vijijini. Asilimia 66 ya wakazi wa vijijini na asilimia 61 ya wakazi wa mijini wanamuunga mkono John Magufuli.

Asilimia 26 ya wanaomuunga mkono John Magufuli walidai kwamba ni kwasababu yeye ni mchapakazi, na asilimia 12 ya wanaomuunga mkono Edward Lowassa walisisitiza kwamba anaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini. Izingatiwe kwamba kauli hizi zinafanana karibu neno kwa neno na kauli mbiu za kampeni za wagombea hawa wawili.

Hata hivyo, wananchi hawana taarifa sahihi juu ya nafasi rasmi ya Ukawa kama mseto. Asilimia 49 ya wananchi wanafikiri kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa, kinyume na hali halisi. Asilimia 57 wanafikiri kwamba neno ‘Ukawa’ litakuwepo kwenye karatasi zao za kupigia kura. Hii pia, sio kweli. Bila kampeni na juhudi za kuwaelimisha wapiga kura ili wawe na taarifa sahihi kuhusu jambo hili, hali hii inaweza kuleta wasiwasi siku ya uchaguzi. 

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhutasari wa utafiti mwenye jina la Sema mwananchi, sema | Maoni ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa. Muhtasari huu umetumia takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia simu za mkononi na wenye uwakilishi wa taifa zima. Matokeo yanatokana na Awamu ya 1 ya kuwapigia simu wahojiwa wapya 1,848 iliyoendeshwa kati ya Agosti na Septemba 2015. 
 
Wahojiwa waliteuliwa kwa kutumia njia kama zinavyotumika na asasi za utafiti duniani kote. Unasibu (sampling) huu ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Takwimu hizi zimelinganishwa na zile za awamu za utafiti katika miaka ya nyuma, zikiwemo:
  • Utafiti wa awali wa kwanza wa Sauti za Wananchi 2012
  • Sauti za Wananchi Awamu ya 10 ya Octoba 2013
  • Sauti za Wananchi Awamu ya 24 ya Septemba 2014
  • Awamu za utafiti za Sauti za Wananchi Aprili-Julai 2015
  • Utafiti mpya wa awali ulioendeshwa kati ya Julai na Agosti 2015

Twaweza ilibaini kuwa zoezi jipya la kuwaandikisha wapiga kura lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Asilimia 98 ya wahojiwa waliripoti kwamba wameshajiandikisha chini ya mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR). Hata hivyo, wananchi wengi walikumbwa na changamoto nyingi katika mchakato huo. Asilimia 68 ya wananchi walitaja urefu wa foleni za kujiandikisha kama tatizo kuu.
 
 Asilimia 51 walisema walisubiri au walishuhudia wananchi wengine wakisubiri muda wa zaidi ya masaa sita kabla ya kujiandikisha. Aidha asilimia 37 waliona au wao wenyewe walipa matatizo ya kusukumana kwenye foleni. Mashine za BVR kushindwa kufanya kazi ipasavyo kuliripotiwa na asilimia 26 ya wananchi. Upendeleo kwenye vituo vya kujiandikisha uliripotiwa na asilimia 19. Ukosefu wa uzoefu wa BVR ulilalamikiwa na asilimia 16 ya wananchi.

Pamoja na kujiandikisha kupiga kura, asilimia 99 ya wananchi walisema kwamba wanadhamiria kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hata hivyo, izingatiwe kwamba asilimia 79 ya wahojiwa hawa walidai pia kwamba walipiga kura wakati wa uchaguzi wa 2010 wakati hali halisi inaonesha kuwa waliopiga kura walikuwa asilimia 43 tu. Aidha, ni asilimia 57 tu ya wananchi ndio walioweza kutaja tarehe sahihi ya uchaguzi, yani Oktoba 25. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba mara nyingi kuna tofauti kati ya majibu ya watu wakati wa kura za maoni au tafiti mbalimbali, na vitendo vyao halisi.

Asilimia 64 ya wananchi walisema kwamba wanakumbuka vyema ahadi zilizotolewa na Wabunge wao katika uchaguzi uliopita, na asilimia 86 kati ya hao walisema kwamba mbunge wao hakutekeleza ahadi hizo au alizitekeleza chache.

Aidha, wananchi waliorodhesha changamoto kuu walizoona hapa nchini. Kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, huduma za afya ni changamoto kwa asilimia 59 ya Wananchi, ukosefu wa maji ikitajwa na asilimia 46, elimu duni na asilimia 44, na umaskini, asilimia 39. Hata hivyo, kumekuwa na mabadiliko kadhaa. Watu wachache zaidi walitaja umaskini (wamepungua kutoka asilimia 63 mwaka 2014) na watu wengi zaidi walitaja maji (wameongezeka kutoka asilimia 27 mwaka 2014).

“Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia hapa,” alisema Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza. “Wananchi wanabadilisha mawazo kuhusu vipaumbele vyao. Waliweka kipaumbele kwa afya badala ya umasikini katika kipindi kifupi cha miezi 12.”

“Watu wana hamu kubwa sana ya kupiga kura” aliongeza, “lakini hali hii si kigezo cha kuaminika katika kutabiri wangapi kweli watapiga kura siku ya uchaguzi. Wakijitokeza kwa wingi, itaipa uhalali mkubwa serikali ya awamu ijayo. Wakijitokeza wachache, inaweza kuashiria ama hali ya wananchi kukata tamaa, au hali ya kujiamini kwamba tayari wameshinda, au hali zote mbili kwa pamoja.”

“Kwa pamoja, mambo haya mawili yanatoa picha kwamba huenda wapiga kura wakawa hawana uhakika wamchague nani. Yanaimarisha ujumbe kwamba mashindano haya ndio kwanza yameanza kupamba moto. Wagombea hawana budi kuimarisha mahusiano yao na wapiga kura wakiwa na malengo mawili makuu; Lengo la kwanza ni kunadi ubora wa ilani na sera zao. Lengo la pili ni kuhakikisha kwamba watajitokeza kwa wingi kuwapigia kura siku ya uchaguzi, Oktoba 25.”

2 comments:

Anonymous said...

Sampling means picking items randomly,and probably you may be achieved to pick the favorable items.This will lead you to the wrong data.Furthermore these data seems to be the cooked one.

Anonymous said...

jembe jembe safiiiii