Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo Benki Kuu, Bw. Bernard Dadi (kushoto)
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam wakati wa kutangaza rasmi mabenki kufanya kazi kwa muda wa nyongeza
kuwawezesha wateja wa bandari na wadau wengine kufanya malipo hadi saa 2 usiku
kwa siku za kazi na saa 8 kwa siku za mwisho wa wiki na sikukuu. Wengine ni Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es
Salaam, Bw. Hebel Mhanga (wa pili kushoto), Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya
Uchukuzi, Bw. Gabriel Migire (wa pili kulia) na Kamishna wa Forodha wa TRA, Bw.
Tiagi Kabisi (kulia). Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi bandari hiyo.
Kaimu
Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Hebel Mhanga (kulia) akielezea
jambo kwa kundi la waandishi wa habari waliotembelea bandari
hiyo kuona maendeleo ya utekelezwaji wa miradi inayotekelezwa chini ya
mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Inatarajiwa kuwa baada ya kukamilika, miradi
hiyo itaongeza uwezo na ufanisi wa bandari hiyo.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Hebel Mhanga (kulia)
akiteta jambo na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo Benki Kuu, Bw. Bernard Dadi mwishoni
mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza rasmi mabenki kufanya kazi
kwa muda wa nyongeza kuwawezesha wateja wa bandari na wadau wengine kufanya
malipo hadi saa 2 usiku kwa siku za kazi na saa 8 kwa siku za mwisho wa wiki na
sikukuu. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza
ufanisi bandari hiyo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeelezea
kuridhishwa kwake na uamuzi wa serikali kuruhusu rasmi nyongeza ya muda wa
kufanya kazi kwa benki hapa nchini na kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza
ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hii inakuja baada ya serikali kupitia Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kuruhusu kutumika kwa mfumo wa huduma baina ya taasisi za
kibenki (TISS) hadi saa 2 usiku na hivyo kuwezesha wateja kufanya malipo na kuendelea
na taratibu nyingine katika bandari hiyo bila tatizo.
Mfumo huo umeunganishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na Wizara ya Fedha ili kuwezesha malipo mbalimbali kama kodi kuweza kulipwa
katika muda huo wa nyongeza.
Kaimu Meneja wa bandari hiyo, Bw. Hebel Mhango amesema jijini
Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa mfumo huo utaisaidia mamlaka hiyo na wadau
wengine kwa kiwango kikubwa kwa kuwa utasaidia kuendana na mpango ulioanzishwa
bandarini wa kufanya kazi kwa saa 24.
Aliwakumbusha watumiaji wa bandari hasa wakala wa mizigo kuwa
mfumo huo mpya unalenga kuwasaidia kuokoa muda, gharama na hivyo kuongeza
ufanisi katika biashara zao.
“Tunaomba sasa wadau wengine wajitahidi kuendana na kasi ya
bandari kwa kufanya pia kazi kwa muda wa saa 24. Tutaendelea kuhamasisha wadau
wetu kuhusiana na mfumo huu mpya,” alisema.
Akizungumza awali, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Bw.
Gabriel Migire alisema serikali imeamua kuongezamuda wa utendaji kazi kwa
mabenki ili kuruhusu wateja na wadau kulipia kodi zao hadi saa 2 usiku.
Alisema mbali na utekelezaji wa mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa (BRN) katika sekta ya uchukuzi, hatua hiyo pia itarahisisha ukusanyaji wa
mapato ya serikali na huduma ya mizigo.
Kwa mujibu wa takwimu, muda wa miezi sita ya majaribio iliyopita,
mfumo huo umeonyesha mafanikio makubwa.
“Miezi 6 ya kipindi cha majaribio ya mfumo huu, jumla ya
miamala 7,727 yenye thamani ya Tshs 382 bilioni ilifanyika,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kutekeleza miradi ya BRN katika
kuifanya bandari kuwa kivutio cha nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
“Wadau wote wa bandari watumie fursa hii kuleta ufanisi
katika kazi zao,” alisema.
Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo BoT, Bw. Bernard Dadi alisema
benki hiyo imeruhusu malipo kufanyika hadi saa 2 usiku kwa siku za kazi na
kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana mwisho wa wiki na siku za sikukuu.
“Ni vyema benki zikazingatia muda huu mpya badala ya ule
zamani ambapo malipo kama hayo yalirusiwa kufanyika hadi saa 7 mchana,”
alisema.
Kamishna wa Forodha wa TRA, Bw. Tiagi Kabisi alisema mamlaka
hiyo inakubaliana na muda huo wa nyongeza kwani utasaidia katika ukusanyaji wa
mapato ya serikali.
“TRA pia imeongeza masaa ya kuhudumia wateja wake ili
kuendana na kasi ya maboresho ya bandari yanayoendelea,” alisema.
No comments:
Post a Comment