RAIS wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara, mnamo tarehe 14 Oktoba, 1999, aliaga
dunia katika hospitali ya mtakatifu Thomas
Jijini London
nchini Uingereza.
Katika uhai wake, alikuwa ni Mmalenga.
Aliandika barua ya Kiserikali kwa mtindo
wa utenzi, pia alijibiwa barua hiyo kwa mtindo
wa utenzi na Nguli/Karii, Hayati Saadani
Abdul Kandoro aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mnamo mwaka 1964.
Nukuu ya Hayati Saadani A. Kandoro “Huu ni utenzi ulioandikwa kwa njia ya barua iliyotungwa na Muheshimiwa
Mtukufu mwalimu J.K. Nyerere President
wa TANU na Serikali. Aliniletea barua hiyo ili kunizungumza jinsi ya watu
wanaopenda kujisaidia katika shughuli za maendeleo na jinsi ya kuwapa moyo
dhidi ya adui wa jamii katika shughuli za vijiji”.
Picha ya Hayati Mw. J.K. Nyerere
SHEIKH KANDORO, SIKIA!
1.
Sheria husaidia,
Kuijenga
Tanzania,
Siyo kazi
ya sheria,
Nchi kutuharibia.
2.
Kila
nchi ina nia,
Inayoikusudia,
Vile vile
ina njia,
Itakayoipitia.
3.
Tanzania
tuna nia,
Ya kujenga
ujamia,
Na njia ya kupitia,
Ni wote kusaidia.
4.
Kijiji
cha turadhia,
Kisima
kujipatia,
La magambo
limelia,
Watu wakahudhuria.
5.
Wakakubali
kwa nia,
Kisima
kujichimbia,
Aliyewakatalia,
Kukuye wakamlia.
6.
Akenda
kushtakia,
Kwa hakimu
wa sheria,
Kwamba
wamemuonea
Kuku wake kalmia.
7.
Hakimu
akasikia,
Akaita
jumuia,
Wakaja akawambia,
Nyinyi wavunja
sheria.
8. Basi
nawahukumia,
Faini shilingi mia,
Na sabini za
fidia,
Au jela
kuingia.
9.
Hakimu
wakamwambia,
Itatushinda
fidia,
Hata na
faini pia,
Heri
jela kuingia.
10.
Wakafungwa
kwa sheria,
Na maji
wakamwachia,
Mwenye kuku
kuumia,
Pamwe na Hakimu pia.
11.
Huko
ni kusaidia,
Adui wa jumuia,
Nasi kazi
ya sheria,
Ila ya maharamia.
12. Kazi hasa ya sheria,
Kusaidia raia,
Sina nia
kuwavunjia,
Wanapojisaidia.
“JIBU LA SHEIKH S.A. KANDORO
ALIYEKUWA AREA COMMISSIONER BAGAMOYO, KWA SHAIRI LA MHESHIMIWA MWALIMU
J.K.NYERERE, RAIS WA JAMHURI YA TANZANIA”
“Huu ni utenzi niliandika kama barua ya kumjibu Mheshimiwa Mtukufu
Mwalimu J.K. Nyerere President wa TANU kujibu utenzi wake alioniandikia juu ya
wanaoharibu maendeleo ya kijiji katika kazi za jamii”.
Picha ya Hayati sheikh S. A Kandoro
1.
Labeka
Mheshimiwa,
Julius msifiwa,
Kambarage muelewa,
Bwana nakuitikia.
2.
Nakuitikia
sheria,
Kwamba inasaidia,
Kuijenga Tanzania,
Na ni nguzo ya Dunia
3.
Kutoheshimu
sheria,
Huleta wingi udhia,
Amani ikapotea,
Nchi
zikaangamia.
4.
Ni
msumeno sheria,
Mithali hii natia,
Haitaki kubabia,
Pendelea liso njia.
5.
La
mgambo likilia,
Watu wote hudhuria,
Kisima kujichimbia.
Hilo lataka sheria.
6.
Kuna
wavivu wa nia,
La mgambo likilia,
Nao anajikalia,
Huendi kuhudhuria.
7.
Mfano
huo hatia,
Wengine huufatia,
Na wao hujikalia,
Kazi zetu husinzia.
8.
Kimila
nimesikia,
Waweza kumsikia,
Kuku wake kujilia,
Lakini sio sheria.
9.
Kwa
kuwa sio sheria,
Mvivu hujishitakia,
Na walao huumia,
Pia hutozwa fidia.
10.
Twazidi
kukulilia,
Ifanywe hasa sheria,
By Law kuitia,
Yaweza kusaidia.
11.
Yaweza
kusaidia,
Kuku tukijilia,
Pasiwepo hata njia,
Mvivu kukimbilia.
12.
Kuku
tumejilia,
Pasiwe na kuponyea,
Hakimu kumuendea,
Kwamba alipwe fidia.
13.
Mkazo
twaukazia,
Bila nyuma kurudi,
Twataka kuendelea,
Kuinua Tanzania.
14.
Taifa
kuitikia,
Kazi kuzishangilia,
Ndilo tunalolilia,
Ndipo tunakazania.
15.
Ndipo
tuna kazania,
Na tena tuna kania,
Kuishangaza dunia,
Lengo letu kutimia.
16.
Bila
nguvu kuzitia,
Mkazo wa kisheria,
Unafaa kufatia,
Kazi zitaendelea.
Utii wa Sheria bila kushurutishwa:
Nukuu ya S .A . Kandoro , Mashairi
ya Saadan,
(Jina la Ushairi ; Staharaki kwa
tendo ),
(UK. 162-166)
Mnukuu; Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo;
Idara ya Maendeleo ya Utamaduni; Sehemu ya Lugha.
Hajjati S . Kitogo na C. Mhongole
No comments:
Post a Comment