Thursday, September 3, 2015

Mashehe wa Tanzania waliotekwa nchini Congo DRC waachiwa huru

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya kuachiwa huru kwa Mashekhe wa Tanzania waliotekwa nchini Congo DRC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji Kombo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (kulia) wakimsikiliza Balozi Mulamula wakati akizungumza na Waandishi wa Habari. 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Bi. Zuhura Bundala (kulia), Afisa Mambo ya Nje, Bw. Elisha Suku (katikati) na Bw. Rewben Mchome nao wakifuatilia mkutano huo na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Balozi Silima naye akizungumza wakati wa mkutano kati ya Katibu Mkuu na waandishi wa habari.
Mwandishi wa Habari wa Kituo Televisheni cha Azam Bw. Jamali Hashim akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (katikati) akielezea jambo katika mkutano huo na waandishi wa Habari huku Balozi Mulamula akisikiliza. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bw. Innocent Shiyo.
Mkutano ukiendelea Picha na Reginald Philip ===============================
MASHEHE WALIOTEKWA NCHINI DRC WAACHIWA HURU
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimefanikisha jitihada za kuachiwa huru mashehe kutoka Tanzania waliokuwa wanashikiliwa mateka na moja ya vikundi vya uasi huko Kivu Kaskazini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu taarifa za kuachiliwa huru kwa Mashehe hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa taarifa za awali zinaeleza kwamba mashehe hao ambao walikwenda nchini DRC kwa ajili ya kuhubiri dini wameachiliwa huru na watekaji jana tarehe 01 Septemba, 2015.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Congo, Mhe. Anthony Cheche, Mashehe hao kwa sasa wamepelekwa Mjini Goma ambako taratibu za kukutana nao na kupata undani wao zitafanyika kabla ya taratibu za kuwarejesha nchini kufanyika.
“Tumepokea taarifa hizo njema za kuachiliwa huru kwa mashehe hao jana kutoka kwa Balozi wetu nchini Congo na leo Balozi Cheche anatokea Kinshasa kwenda Goma waliko Mashehe hao ambapo tutajua idadi yao kamili na masuala mengine ya muhimu kutoka kwao yatajulikana kabla ya kuanza taratibu za kuwarejesha nchini” alisema Balozi Mulamula.
Aidha, Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Serikali ya Congo kwa ushirikiano wa hali ya juu waliouonesha hadi kufanisha Mashehe hao kuachiliwa huru wakiwa salama.
Katika hatua nyingine, Balozi Mulamula alitoa rai kwa Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kidini, kibiashara au kutafuta maisha wafuate taratibu ikiwemo kutumia Wizara au Balozi zetu zilizopo katika maeneo wanayokwenda au karibu na maeneo hayo ili kuziwezesha Balozi na Serikali kwa ujumla kuwasaidia pale wanapopatwa na matatizo mbalimbali.
“Napenda kutoa rai kwa Watanzania wote wanaokwenda nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali kuwasiliana na Balozi zetu kwa kutoa taarifa zao ili wasaidiwe pale wanapopatwa na matatizo kwani ni jukumu la Balozi kulinda maslahi ya Tanzania na raia wake katika nchi wanayoiwakilisha, tumieni Wizara na Balozi zetu kwani ni jukumu letu”, alisisitiza Balozi Mulamula.
Kwenye mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji Kombo alisema kuwa Serikali ya Zanzibar imefurahishwa na taarifa za kuachiliwa huru kwa mashehe hao ambao wanatokea Taasisi ya dini ya Tablighi ya Zanzibar.
“Tukio la kutekwa kwa mashehe hao lilikuwa la kushtusha na kufadhaisha, hata hivyo Serikali ya Jamhuri na ile ya Zanzibar zililichukua kwa uzito mkubwa kwa kuwa hawa ni Watanzania wenzetu na tunashukuru jitihada hizo zimezaa matunda kwa wenzetu hao kuachiliwa huru” alisema Balozi Silima.

No comments: