Thursday, September 10, 2015

LISHE DUNI YACHANGIA VIFO VYA WATOTO NA KIMAMA WAJAWAZITO

 
Na Woinde Shizza,Arusha.
Lishe duni kwa kinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano imekua chanzo cha vifo vya watoto wadogo pamoja na kinamama hao hali ambayo  hali ambayo inazorotesha maendeleo ya kiafya na kitaaluma hivyo watanzania wametakiwa kutumia lishe bora yenye vitamin na virutubisho ili kujenga jamii yenye afya bora kwa ustawi wa nchi.

Hayo yameelezwa na Naibu waziri wa Afya Dokta Kebwe S.Kebwe akitoa takwimu za vifo vya watoto na kinamama vinavyosababishwa na lishe duni amewataka kinamama kuzingatia lishe bora hasa katika kabla ya ujauzito na baada ya kujifungua katika siku 1000 za kuzaliwa kwa mtoto ili aweze kukua vizuri kiafya  hususan afya ya akili na kufaulu kitaaluma.


Kebwe amesema kuwa Mtoto aliyezaliwa na uzito pungufu (chini ya kilo 2.5) ana uwezekano wa kufa katika mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa, mara nne kuliko mtoto aliyezaliwa na uzito wa wastani au zaidi.Mtoto mwenye uzito mdogo sana ana uwezekano wa kufa kutokana na ugonjwa wa kuambukizwa mara nane kuliko mtoto aliye na hali nzuri ya lishe.


“Lishe duni inahatarisha maisha ya watoto wa Tanzania kama ilivyo katika nchi zinazoendelea.Tafiti zinaonyesha kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya kiwango cha udumavu na vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka 5, katika ngazi ya mikoa nchini” Kebwe

Naibu Waziri wa Afya Dokta Kebwe S.Kebwe amesema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa Masuala ya Lishe ulioandaliwa na Taasisi ya GAIN (Global Alliance for Improved Nutrition)  unaondelea jijini Arusha huku akiwaagiza maafisa afya walioko katika Halmashauri kufanya kazi zao za kuwaelimisha wananchi na kuwashauri juu ya masuala ya lishe badala ya kupangiwa majukumu mengine na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Mfalme wa 3 wa Lesotho ambaye pia ni Balozi wa  lishe barani Afrika  Mfalme Letsie wamesema kuwa lishe bora ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi hivyo amezitaka nchi za kiafrika kuweka vipaumbele katika masuala ya lishe kwani yanachangia katika ukuaji wa uchumi.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema kuwa takribani watu bilioni 1 duniani wanakabiliwa na matatizo ya lishe kwa mujibu wa Takwimu za shirika la Afya duniani idadi ambayo ni kubwa hivyo Tanzania na nchi nyingine zina jukumu la kuhamasisha lishe bora na matumizi ya vitamin na virutubisho katika kila mlo.

Mkutano wa Masuala ya Lishe umefanyika jijini Arusha ukikutanisha wataalamu wa lishe kutoka karibu kwenye kila pembe ya dunia ili kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza njaa na tatizo la lishe duni .

No comments: