Sunday, September 13, 2015

LAFARGE TANZANIA YAKABIDHI MRADI WA MAJI KWA KIJIJI CHA SONGWE VIWANDANI, MBEYA

  Afisa Mtendaji Mkuu wa Lafarge Tanzania (Mbeya Cement), Catherine Langreney na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Sabi wakikata utepe kuzindua mradi wa maji uliojengwa na kampuni hiyo kwa ajili ya kuwaondelea tatizo la uhaba wa maji safi na salama wananchi wa kijiji cha Songwe Viwandani mkoani Mbeya katika hafla iliyofanyika kijijini hapo mwishoni mwa wiki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Lafarge Tanzania (Mbeya Cement), Catherine Langreney na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Sabi wakimbebesha ndoo ya maji mmoja ya wananchi aliyekuwepo katika uzinduzi wa mradi wa maji uliojengwa na kampuni hiyo kwa ajili ya kuwaondelea tatizo la uhaba wa maji safi na salama wananchi wa kijiji cha Songwe Viwandani mkoani Mbeya katika hafla iliyofanyika kijijini hapo mwishoni mwa wiki.
Mmoja ya wananchi akitoa shukrani mara baada ya kuzinduliwa mradi wa maji uliojengwa na Lafarge Tanzania (Mbeya Cement) kwa ajili ya kuwaondelea tatizo la uhaba wa maji safi na salama wananchi wa kijiji cha Songwe Viwandani mkoani Mbeya katika hafla iliyofanyika kijijini hapo mwishoni mwa wiki.
---Lafarge Tanzania leo imekabidhi mradi wa maji uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 10 kwa kijiji cha Songwe Viwandani mkoani Mbeya. Mradi huu unatarajiwa kuwanufaisha familia zaidi ya 200 na unahusisha tanki la kuhifadhi maji pamoja na vifaa mbalimbali vya kusaidia upatikanaji maji safi ya kunywa kwa kijiji hiki. 

Akiongea katika hafla fupi wakati wa kukabidhi mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Lafarge Tanzania, Catherine Langreney amesema kwamba Lafarge Tanzania imedhamiria kusaidia jamii ipate maji safi kwa kuwapatia suluhisho la kudumu la tatizo la maji ikiwa ni sehemu ya mpango wake kusaidia jamii. 

 “Lafarge Tanzania inatambua kwamba maji ni kati ya mahitaji muhimu na kiungo muhimu kwa maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi. Kuwapatia wananchi suluhisho la kudumu la matatizo yao kunadhiirisha azma yetu kuisaidia jamii ambayo imezunguka eneo letu la biashara,” alisema Langreney na kuongeza kwamba upatikanaji wa maji safi ni muhimu kwa afya ya jamii na ni muhimu kwa mazingira pamoja na maendeleo kiuchumi. 

Langreney alisisitiza kwamba upatikanaji maji kwenye kijiji hicho utaboresha hali ya usafi na afya na kuwaletea maisha bora wananchi wa kijiji cha Songwe Viwandani. “Kabla ya mradi huu watu walikuwa wanavuka barabara kuu iendayo Tunduma kuja kuchota maji katika nyumba za kiwanda cha Lafarge Tanzania jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya jamii hii.” 

Akizindua mradi huo kama mgeni rasmi, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Bw. Nyirembe Sabi aliwashukuru Lafarge Tanzania kwa jitihada zao kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza kwamba hii inadhiirisha dhamira thabiti ya kiwanda hicho kusaidia jamii na mfano wa kuigwa na makampuni mengine. 

“Jamii pamoja na mazingira yaliyoizunguka vinahitaji maji ili kuweza kustawi, nafurahi kwamba mradi huu utaipatia jamii rasilimali hii muhimu na niwashukuru Lafarge Tanzania kwa jitihada zao,” 

alisema Nyirembe. Mkuu huyo wa wilaya pia aliainisha azma ya serikali kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi kwa kusaidia mipango kama ambayo inaboresha maisha ya jamii. 

Mbali na msaada huo, Lafarge Tanzania pia imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili kuwapatia wananchi wa Songwe makazi bora na ya gharama nafuu.

No comments: