Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, kushoto, akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya ya mikopo ya simu za mikononi aina ya Huawei ijulikanayo kama 'Jibayportphonishe', uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Micka Mavoa, Mkurugenzi wa Cape View, Kampuni inayoshirikiana na Bayport katika huduma hiyo ambayo mteja akikopa simu atapelekewa hadi mahala anapohitaji ifike. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, imezindua huduma yake mpya ya kukopesha (Smartphone) simu za mikononi aina ya Huawei zenye thamani ya Sh 140,000, ikiwa na lengo la kuwawezesha Watanzania ambao ni watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa kumiliki simu wakati wowote ili ziwakwamuwe katika suala zima la mawasiliano ya simu za mikononi, huduma inayotambulika kama 'Jibayportphonishe'.
Kuanzishwa kwa huduma hiyo ya mikopo ya simu za mikononi kumekuja siku chache baada ya taasisi hiyo pia kuzindua huduma ya bima ya magari, pikipiki na bajaj, ambapo zote kwa pamoja ni mkombozi kwa Watanzania, wakiwamo wale wenye kipato cha chini na cha kati.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba kuanzishwa kwa huduma hiyo kutaifanya jamii iwe katika kiwango kizuri cha mawasiliano, hivyo kukuza pia uchumi wao.
Mkurugenzi wa Cape View, Micka Mavoa, kulia akizungumza jambo.
Alisema kwamba badala ya mtumishi wa umma na wale wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa kuwekeza kidogo kidogo ili wanunuwe simu watakazo, sasa wanaweza kukopeshwa simu hizo na kupelekewa hadi katika maeneo yao wanayopatikana. Alisema simu hizo zitaambatana na ofa ya intaneti MB 500 bure kila mwezi kwa miezi sita kutoka katika Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania, huku mteja akilazimika kulipa Sh 9000 kila mwezi, katika kipindi cha miezi 24.
“Bayport Financial Services ni taasisi ya Watanzania wote wakiwamo wale wenye kipato kikubwa au kidogo, hivyo kwa kuanzishwa kwa huduma hii, mteja wetu anaweza kukopa simu kisha akalipa kidogp kidogo, ukizingatia kwamba wapo watoto wanaosoma mbali na wazazi wao, hivyo naamini kwa fursa hii hata maisha yatakuwa rahisi.
“Baba au mama anaweza kuchukua simu apendazo kwa ajili ya familia yake, ambapo pia akichukua simu yenye malipo kwa kipindi cha miezi 60, atalazimika kukatwa Sh 6000 tu kila mwezi, ikiwa ni huduma rahisi na nzuri kwao, hivyo Bayport tunaamini wateja wetu na Watanzania kwa ujumla wataendelea kutuunga mkono ili tuwahudumie na kuwakwamua zaidi,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Cape View, Micka Mavoa, alisema kwamba huduma hiyo mpya ni muhimu kwa Watanzania wote bila kuangalia kipato chao, ukizingatia kwamba wanaweza kufikishiwa simu hadi majumbani kwao baada ya mkopo wao kufanikiwa.“Kwa kushirikiana na Bayport Financial Services, tunaamini kwa kiasi kikubwa tutafanikiwa kwenye huduma hii, ukizingatia simu hizi ni nzuri na zitakuwa na waranti ya mwaka mmoja ili kuona wateja wetu na Watanzania kwa ujumla wanapata huduma bora, huku simu hizo zikiwaa na huduma zote za mitandao kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter, na mengineyo bila kusahau ofa ya vifurushi vya internet kutoka Vodacom bure kwa kipindi cha miezi sita,” alisema.
Kwa mujibu wa Ngula, ili mtu aweze kukopeshwa simu hizo kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa na Bayport, anatakiwa kutembelea tawi la ofisi ya Bayport zilizoenea nchi nzima au kwa wakala na kupewa fomu ya mkopo na endapo utaidhinishwa atafanikiwa kupata simu hizo kwa kufikishiwa hadi eneo analoishi ndani ya siku tatu tu.
Bayport ni taasisi ya kifedha inayotoa huduma bora za kifedha, ambapo imekuwa ikizindua huduma mbalimbali kama vile mikopo ya bidhaa, viwanja vya mradi wa Vikuruti, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, mikopo ya fedha na nyinginezo zinazowakwamua kiuchumi wateja wao ambao ni watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa na Bayport, huku huduma hizo zikitolewa pia kwa njia ya mtandao wa www.kopabayport.co.tz.
No comments:
Post a Comment