Bwana Nixson Mlumba – AfisaManunuzi wa ACACIA akifafanua jambo wakati wa Kikao hicho |
Baadhi ya Wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini maelezo ya kutoka kwa Uongozi wa Kampuni ya Acacia wakati wa Kikao hicho. |
Mmoja wa wafanyabiashara wa mkoa wa Shinyanga akichangia mawazo wakati wa kikao. |
Wafanyabiasha wa mkoa wa Shinyanga wakiwa katika picha ya Pamoja na mkuu wa Mkoa na viongozi kutoka kampuni ya ACACIA. |
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini aliyekuwa Shinyanga.
WAFANYABIASHARA wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuchangamkia Fursa mbalimbali za biashara zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu Buzwagi unaomilikiwa na kampuni ya Acacia.
Meneja mkuu wa Mgodi huo Injinia Filbert Rweyemamu ametoa wito huo katika kikao baina ya uongozi wa Mgodi wa Buzwagi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga ambapo alisema mgodi wa Migodi inayomilikiwa na Acacia imejikuta ikishindwa kufanya kazi na wafanyabiashara wa mkoani humo kutokana na wengi wao kushindwa kukidhi vigezo vya taratibu za manunuzi kutokana na wengi wao kuwa na mitaji midogo hali ambayo imepelekea huduma nyingi za manunuzi kuwategemea wafanyabiashara wakubwa kutoka maeneo mengine.
“Nia ya Kampuni ya ACACIA ni kufanya kazi na wafanyabiashara wanaotuzunguka lakini kuna chanagamoto ya wengi wenu kushindwa kufikia vigezo vya manunuzi ambavyo ACACIA imejiwekea, niwaase kupitia vikao hivi ambavyo vimelenga kuwapatia uelewa mkajipange na ikiwezekana jiungeni katika vikundi ambavyo vitakuwa na mitaji mikubwa itakayowawezesha kuwa na uhakika wa kufanya kazi na migodi yetu” Alisema Injinia Rweyemamu.
Injinia Rweyemamu ameongeza kuwa kwa sasa huduma nyingi Pamoja na bidhaa vikiwemo vipuli vya magali na mitambo wamekuwa wakitegemea wasambazaji wakubwa kutoka nje, huku akisisitiza kuwa kama wafanyabiashara wa mkoa wa Shinyanga wangeungana na kuwa na biashara hizo Migodi yetu isingelazimika kuagiza bidhaa hizo nje.
Kwaupande wake mtaalamu wa masuala ya manunuzi ya ndani na Maendeleo ya biashara wa ACACIA Bwana Nixson Mlumba akitoa taarifa za namna ambavyo wafanyabiashara wa Shinyanga wamekuwa wakishiriki kufanya biashara na ACACIA amesema takwini zinaonyesha ushiriki mdogo sana wa wafanyabiashara wa mkoa huo huku wengi wao wakishindwa kufikia vigezo vya manunuzi ya ACACIA kutokana na wengi wao kuendesha biashara kinyume cha Sheria.
“Kama alivyosema meneja wa mgodi wa Buzwagi, Fursa zipo cha msingi zingatie sharia za nchi na jiunge kwa Pamoja ili muweze kuongeza mitaji ya biashara zenu, Hatupendi kufanyabiashara na mtu ambaye baada ya kumpatia tenda atashindwa kutuhudumia kwa mujibu wa Mahitaji yetu” alisema Nixon
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephina Matiro alisema kuwa fursa hii ambayo inatolewa na kampuni ya ACACIA haina budi kuchangamkiwa na wafanyabiashara wote wa kanda ya Ziwa kwani itasaidia katika kuongeza pato lao Pamoja na pato la Taifa.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassor Rufunga awali alisema kuwa mgodi wa Buzwagi umekuwa kifua mbele katika suala la shughuli za maendeleo ndani ya Mkoa huo huku ukishirikiana na wakandarasi wa ndani ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa madarasa na zahanati.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema licha ya wakandarasi wa shughuli za ujenzi kuonyesha uwezo mzuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, bado wafanya biashara wengine wameshindwa kuchangamkia fursa hizo zinazotolewa na Mgodi, hali ambayo imepekea fursa hizo kutumiwa na wafanyabiashara wa maeneo mengine ya nchi na wakati mwingine wafanyabiashara wa nje ya nchi.
Mkutano huo uliofanyika katika hotel ya Submarine wilayani Kahama ulilenga kuwasaidia wafanyabiashara wa mkoa huo kupata ufahamu juu ya masuala mbalimbali ya manunuzi katika kampuni hiyo.
No comments:
Post a Comment