Friday, August 7, 2015

MAALIM AZINDUA UVUNAJI MATIKITI MAJI MUWANDA ZANZIBAR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizindua uvunaji wa matikiti maji kwa wakulima wa shehia ya Donge Muwanda.
 Mkulima wa matikiti maji na pilipili boga Bw. Salum Khamis Kiregu akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhusiana na changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa pamoja na badhi ya wakulima wa Donge Mchangani na Muwanda, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Affan Othman Maalim (wa pili kushoto). Picha na OMKR.
 
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu juhudi zinazochukuliwa na wananchi wa Donge katika kuendeleza kilimo cha matunda na mboga mboga.

Amesema iwapo kilimo hicho kitawekeza mikakati imara, kinaweza kuwa mkombozi wa kweli kwa wakulima na kuweza kuweza kuongeza kipato chao.
Maalim Seif ameeleza hayo wakati akizindua uvunaji wa matikiti maji na pilipili boga katika shehia za Donge mchangani na Muwanda katika Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.

Amesema katika siku za hivi karibuni, kilimo hicho kimepata mafanikio makubwa na kupunguza uagiziaji wa bidhaa hizo nje ya Zanzibar kutoka asilimia 80 hadi asilimia 20.

Amefahamisha kuwa lengo la Serikali ni kuimarisha zaidi kilimo cha matunda na mboga mboga ili kuweza kukidhi soko la ndani na kuacha kuagizia bidhaa hizo kutoka nje ya Zanzibar.

Amesema kinachohitajika hivi sasa ni kwa Serikali kuongeza mashirikiano na wakulima, ili kusaidia kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji pamoja na pembejeo.

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameiagiza Wizara ya Kilimo kupeleka mabwana na mabibi shamba wa kutosha katika shehia hizo za Mchangani na Muwanda, ili kusaidia utaalamu kwa wakulima hao na kuweza kuzalisha zaidi.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Affan Othman Maalim, amesema tayari Serikali imeanza kufanya utafiti kujua maeneo ya kuchimba visima ili kuwasaidia wakulima hao kuondokana na tatizo la upungufu wa maji.

Hata hivyo amewashauri wakulima hao kujikusanya pamoja ili kurahisisha miundombinu ya maji kuweza kuwafikia walengwa.

Kuhusu tatizo la pembejeo, Bw. Affan amesema Wizara ya Kilimo inaandaa utaratibu wa kulipeleka suala hilo katika ngazi za juu, ili kuwawezesha wakulima wa matunda na mboga mboga kuweza kupatiwa ruzuku za pembejeo za kilimo kama wanavyopatiwa wakulima wa mpunga.

Mapema mmoja kati ya wakulima hao Bw. Salum Khamis Kiregu, amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa licha ya mafanikio wanayoyapata, bado wanakabiliwa na tatizo la soko la kuuzia bidhaa hizo, na kuiomba serikali kuandaa mazingira bora ya soko kwa wakulima hao.

Amesema hivi sasa wanalazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini kupitia kwa wafanyabiashara, jambo ambalo limekuwa likipunguza kipato chao licha ya kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi.

Bw. Kiregu ameeleza matatizo mengine yanayowakabili kuwa ni pamoja wadudu waharibifu na maradhi ya mimea, na kuwaomba wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima ili kusaidia kukabiliana na changamoto.

No comments: