Na Mwandishi Wetu
“Suala la maadili si jipya, Watanzania watakumbuka tangu enzi la Azimio la Arusha misingi ya maadili imekuwa ikisisitizwa kama kijenzi muhimu cha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma,” ni kauli ya Tixon Nzunda, Naibu Kamishna wa Maadili aliyoitoa siku ya uzinduzi wa Ahadi ya Uadilifu, Agosti 14, 2015, Ikulu Dar es Salaam.
Kauli hii inasadifu ninachotaka kukieleza hapa katika makala haya na kwa hakika kumpa kongole Rais anayemaliza muda wake, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuamua kuhuisha suala la maadili kama kijenzi muhimu cha ufanisi katika utendaji wa sekta za umma na binafsi.
Itakumbukwa kuwa Ijumaa iliyopita Reais Kikwete alizindua kile kinachoitwa Ahadi ya Uadilifu ambapo viongozi kadhaa wa umma na kutoka sekta binafsi walitia saini hadharani ahadi za kuendesha shughuli zao kimaadili zaidi.
Ahadi ya Uadilifu kimsingi ni tamko rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na mwenendo wa kimaadili na kuunga mkono Kampeni ya Kitaifa ya Maadili na Mapambano dhidi ya Rushwa. Kwa kusaini tamko hilo mhusika au taasisi inakuwa vimejipambanua kwa umma kuwa hawatajiingiza katika masuala yasiyo ya kimaadili katika utoaji wa huduma na uzalishaji.
Wazo la kuwa na Ahadi ya Uadilifu ni ubunifu kutoka maabara ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) iliyokuwa ikiangalia mbinu za kuboresha sekta ya mazingira ya biashara nchini.
Kwa mujibu wa wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi waliokusanyika katika kufanya uchambuzi huo, ilionekana dhahiri kuwa rushwa bado ni tatizo katika uendeshaji wa shughuli za umma na binafsi.
Pamoja na kuwepo sheria, kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili na kupambana na rushwa bado matokeo ya kuridhisha hasa katika kuinua utendaji na maadili katika uendeshaji wa biashara yavikupatikana.
Wananchi bado wanalalamika kuwepo kwa urasimu usio wa lazima wenye lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa na huduma zisizoridhisha katika utumishi wa umma. Wafanyabishara binafsi nao wapo baadhi hawana maadili na hata kufikia hatua ya kuchochea utoajiwa rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na viwango.
Vile vile Sekta Binafsi haijashirikishwa vya kutosha katika Mkakati wa Kupambana na Rushwa na utamaduni umekuwa ni watu kuamini kuwa Rushwa iko katika sekta ya umma tu wakati wanaotoa rushwa kubwa wako katika Sekta Binafsi.
Ni dhahiri kuwa Sheria, Kanuni, Miongozo na Mikakati iliyopo pekee haiwezi kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la rushwa na maadili. Hivyo kuhitaji mkakati wa ziada ambao utajenga mwitikio na dhamira kwa viongozi wa umma na kuishirikisha Sekta Binafsi katika mapambano dhidi ya rushwa na utovu wa maadili.
Hivyo kusainiwa kwa tamko la ahadi ya uaminifu kutasaidia kukuza maadili na kupambana na vitendo vya rushwa katika sekta ya umma na binafsi; ahadi au tamko hili linashawishi viongozi, watumishi wa umma na makampuni binafsi kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata misingi ya maadili na kupambana na rushwa kwa hiari yao wenyewe.
Katika tamko hilo kunawekwa kauli thabiti ya kimaadili ambayo inaonesha nia ya kufanyabiashara au kutekeleza majukumu ya umma kwa uadilifu na inakumbushwa Makampuni, Viongozi na Watumishi wa Umma juu ya wajibu wao wa kuzingatia Kanuni za Maadili na Mapambano dhidi ya rushwa.
Misingi ya tamko hili imebebwa katika kukuza Uwazi, Uadilifu, Uwajibikaji na Utaalamu katika uendeshaji shughuli za umma; Kukuza mwitikio wa kupambana na rushwa kwa kuimarisha taratibu za udhibiti wa ndani.
Misingi mingine ni pamoja na kusimamia masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, na Kanuni za Maadili ya Kitaaluma;
Pia ipo hoja ya kuimarisha mahusiano ya viongozi wa umma, watumishi wa umma au wamiliki na watendaji wa makampuni na wananchi au wateja wengine; Kudhibiti vitendo vya utovu wa maadili mahali pa kazi na kukuza uzalendo.
Ili kufikia malengo ya ahadi hii Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Miradi (PDB) inayoratibu BRN ndiye mwangalizi mkuu wa kuona suala hili linaleta tija katika kufikiwa malengo mapana ya BRN.
Hata hivyo Sekretarieti ya Maadili ndiyo imepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa kila siku wa ahadi hizi ambapo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Watumishi wa Umma kwa kuwashirikisha Watendaji Wakuu wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ili kuhakikisha utekelezaji unakuwa wa mafanikio kwa upande wa sekta binafsi Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Makampuni binafsi.
Inategemewa kuwa utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu utajenga mwitikio na dhamira ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji, ari ya kupambana na rushwa na utoaji wa huduma bora katika Sekta ya Umma na Binafsi.
Pia, utahamasisha Viongozi, Watumishi wa Umma na kuzingatia misingi ya maadili na Mapambano dhidi ya Rushwa. Aidha, kuwashirikisha wananchi kufuatilia vitendo vya utovu wa maadili miongoni mwa Watumishi wa Umma, Viongozi wa Umma na Sekta Binafsi na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Kwa namna hii hususani katika eneo la utoaji wa huduma na uzalishaji wa bidhaa watanzania watarajie kuimarika sana kwa uadilifu katika utendaji wa wahusika na kusaidia kufikia malengo ya BRN.
No comments:
Post a Comment