WAZIRI wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu, akisalimiana na baadhi ya wadau wa masuala ya uhifadhi
na utalii wakati alipofungua mkutano wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa
mfumo wa usimamizi na uendeshaji Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya
Wanyamapori Tanzania (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akifuatilia majadiliano
wakati wa mkutano wa wadau na viongozi wa Maeneo ya Jumuia ya
Hifadhi ya Wanyamapori nchini (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akizungumza na
wadau na viongozi wa Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori nchini
(WMA), ulioanza jana jijini Arusha kujadili uboreshaji mfumo wa
usimamizi na uendeshaji jumuia hizo.
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akisalimiana na mdau wa
masuala ya utalii na uhifadhi nchini, Willy Chambulo, muda mfupi baada
ya kufungua mkutano wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa mfumo wa
usimamizi na uendeshaji Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori
Tanzania (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.
KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO KATI YA WIZARA NA WMAs
UKUMBI WA NAURA SPRINGS, ARUSHA,
TAREHE 2 & 3 JULAI, 2015.
Mhe. Mahmood
Mgimwa - Naibu Waziri,Wizara ya Maliasili na Utalii;
Dkt. Adelherm Meru - Katibu
Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Bw. Herman Keraryo - Mkurugenzi,
Idara ya Wanyamapori;
Dkt. Simon Mduma - Mkurugenzi Mkuu,Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori;
Dkt.
Freddy Manongi - Mhifadhi Mkuu, Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorogoro;
Bw. Allan Kijazi - Mkurugenzi
Mkuu, Hifadhi za Taifa;
Mwenyekiti, Muungano wa Jumuiya
Zilizoidhinishwa;
Wakurugenzi/ Wawakilishi wa Mashirika
yasiyo ya Kiserikali
(USAID, WWF, FZS, AWF, WCS);
Viongozi wa Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi
za Wanyamapori;
Wawakilishi kutoka Sekta binafsi;
Watumishi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii;
Maafisa Wanyamapori wa Wilaya;
Mabibi na Mabwana.
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika mkutano huu muhimu
unaolenga kutathmini ustawi na changamoto zilizojitokeza/zinazojitokeza katika usimamizi
wa shughuli za uhifadhi kwenye Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori “Wildlife
Management Areas” (WMAs) nchini.
Wageni Waalikwa, Mabibi
na Mabwana
Sera ya wanyamapori ya mwaka 1998 kwa mara ya kwanza nchini ilielekeza
kuanzisha dhana ya ushirikishaji wa jamii katika uhifadhi wa wanyamapori. Dhana
hii inatoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kutenga maeneo ya
ardhi ya vijiji ili kusimamia na kunufaika moja kwa moja kupitia rasilimali ya
wanyamapori. Utekelezaji wa dhana hii ulianza rasmi mwaka 2003 na hadi sasa
maeneo ya WMAs 21 zenye ukubwa wa kilometa za mraba 36237.7 yameidhinishwa na
kutangazwa katika gazeti la serikali. Aidha, maeneo mengine 17 ya WMA yapo
katika hatua mbalimbali za uanzishwaji.
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana
Kwa miaka 12 ya utekelezaji wa dhana hii tumeshuhudia mwamko katika
jamii kushiriki katika kiuhifadhi, na wao kujipatia manufaa ikiwemo ajira, kipato
katika ngazi ya jumuia, vijiji husika na kuchangia katika miradi ya maendeleo katika
sekta za elimu, afya, maji. Pamoja na mafanikio haya bado kumekuwepo na
changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa dhana hii nchini.
Hivyo mkutano huu ni mwendelezo wa
matokeo ya tuliyojifunza wakati wa kutekeleza dhana ya kushirikisha jamii
katika uhifadhi kwa kuwaleta pamoja wadau muhimu na wataalamu ili kubadilishana
uelewa, uzoefu, matokeo ya tafiti, na kutoa fursa ya mjadiliano rasmi yenye
malengo kujitathimini mahali tulipotoka, tulipo na tunapotakiwa kwenda.
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana
Naomba nijikite katika changamoto chache lakini muhimu ambazo mimi kama
Waziri mwenye dhamana nimeziona katika kutekeleza majukumu yangu ambayo
ningependa kupitia mkutano huu uziangalie kwa kina na kutusaidia kutoa ushauri
wa kuandaa maelekezo ya kisera yatakayoweza kutoa majibu kama ifuatavyo:
1.
Kuchangia uboreshaji wa utawala bora katika rasilimali za
wanyamapori na matokeo ya jamii na uhifadhi wa wanyamapori, ikiwa pamoja na
kuhakikisha utawala bora kulingana na maslahi na haki za jamii (muingiliano wa
mamlaka kati ya viongozi wa wilaya, vijiji na wale wa jumuiya/WMA na mgongano
wa maslahi).
2.
Migogoro inayotokana na uwekezaji katika maeneo ya WMA
mfano MBOMIPA.
3.
Mgogoro unaotokana na gharama za watalii katika hoteli na
loji zilizopo ndani ya hifadhi za Taifa na zile zilizopo ndani ya WMAs
zinazopakana.
4.
Uwiano wa mgawanyo wa mafao yatokanayo na uwekezaji katika
maeneo ya WMAs kati ya Jumuiya/WMA, Serikali kuu, halmashauri za wilaya na vijiji
wanachama.
5.
Matumizi ya fedha/mapato zinazotokana katika WMA na katika
vijiji kutofanya kazi zitarajiwa.
6.
Ucheleweshaji wa mgao wa fedha unaotakiwa kupelekwa katika
WMAs kutoka Serikalini.
Wageni Waalikwa
Mabibi na Mabwana,
Mkutano huu ambao ni wa kwanza kufanyika na kukutanisha Wizara, Jumuiya
Zilizoidhinishwa na Wawezeshaji wa WMAs ni fursa muhimu ambayo ikitumika
ipasavyo na kwa nia njema itatoa suluhisho lkwa changamoto nilizozianisha hajo
juu. Hivyo natoa wito kwa washiriki wa mkutano huu kuhakikisha fursa hii
haipote bali itoe tija katika ustawi wa dhana ya kushirikisha jamii katika
uhifadhi endelevu na wenye manufaa kwa jamii.
Wageni Waalikwa
Mabibi na Mabwana
Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru
wawezeshaji katika uanzishaji na uendeshaji wa WMA. Kipekee nitambue michango
iliyotolewa na USAID, WWF, FZS, AWF,
WCS, KfW, BTC, DANIDA, GTZ (GIZ) na AFRICARE. Aidha, ninawashukuru USAID, AWF
na WWF kwa ufadhili wao katika kufanikisha mkutano huu. Ni matumaini yangu kuwa
mkutano huu utaleta tija inayokusudiwa ili kuhakikisha kuwa shughuli za
uhifadhi katika WMA zinaendeshwa kwa ufanisi.
Natangaza rasmi Mkutano huu umefunguliwa.
No comments:
Post a Comment