Tuesday, July 14, 2015

WAZIRI SAADA MKUYA SALUM AMWAKILISHIA RAIS KIKWETE KWENYE MKUTANO WA UFADHILI WA MAENDELEO ADDIS ABABA

Waziri wa   Fedha  Mhe. Saada Mkuya  Salum

Na  Mwandishi Maalum, New York
Mkutano wa Mkubwa watatu wa  Kimataifa,  unaojadili Ufadhili wa Maendeleo (FFD3) , umeanza jana  jumatatu  jijini  Adds Ababa, Ethiopia
Ujumbe  Tanzania katika mkutano huu ambao   utakafanyika kwa siku tatu unaongozwa na  Waziri wa   Fedha  Mhe. Saada Mkuya  Salum akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe.  Jakaya Mrisho Kikwete.
Mhe.  Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum atauhutubia mkutano huo  siku ya  jumanne.
Viongozi  wengine wa Tanzania wanaohudhuria na kushiriki  mkutano huu  muhimu katika kuchangiza vyanzo vya  rasmali  za kusaidia maendeleo  na kuwaondoa  mamilioni  ya watu kutoka lindi la umaskini hususani kwa mataifa yanaoyendelea ni pamoja na Waziri  wa fedha kutoka  Serikali ya  Mapinduzi Zanzibar,  Mhe.   Omar Yusus Mzee , Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw.  Silvanus Likwelile ,  Mkurugenzi  Mtendaji, Kamisheni ya Mipango,  Dr. Philip Mpango  na  Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon pamoja na mambo mengine amesisitiza haja  na umuhimu wa  uwepo wa uhakika wa  raslimali ambazo si tu zitatumika katika   uboreshaji wa maisha ya watu ambao wanazidi kuongezea duniani lakini  pia  kuilinda sayari duani .
Ban ki   Moon amewaeleza washiriki wa mkutano huo wakiwamo wajumbe kutoka   Mataifa yaliyoendelea na   Mashirika ya Kimataifa   kuwa mwaka 2015  unatakiwa kuwa  mwaka wa vitendo na maamuzi.
Akayaainisha   mambo   muhimu matatu  ambayo yanaufanya  mwaka huu wa 2015 kuwa wa vitendo na  kufanya maamuzi.  Kuwa   kwanza kufanyika kwa mkutano huo wa Tatu wa Kimataifa wa  Ufadhili wa maendeleo ambao pamoja na  mambo mengine utapokea na kupitisha tamko la mpango wa  ajenda ya utekelezaji wa mpango mpana juu ya ufadhili  wa maendeleo.
 Eneo la pili na ambalo ni muhimu kwa mwaka huu wa 2015 ni mkutano wa kilele wa kisiasa wa viongozi wakuu wa nchi na serikali  utakaofanyika mwezi Septemba hapa  Umoja wa Mataifa, ambapo viongozi hao wanatarajiwa   kupokea na  kupitisha malengo mapya ya maendeleo endelevu kwa miaka 15 ijayo.
Eneo la tatu na muhimu kwa mwaka huu ni   Mkutano wa Kimataifa kuhusu mabadiliko ya Tabia nchi ambao utafanyika mwezi Desemba huko Paris, Ufarasa.
 Akizungumza zaidi kuhusu mkutano wa ufadhili wa maendeleo,   Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema,   ahadi  tu za maneno  zinazoishia katika makaratasi hazina  tija kwani  kinachotakiwa ni     utoaji wa raslimali fedha pamoja na kuibua vyanzo vipya vya  mapato ili  hatimaye    utekelezaji wa maeneo hayo matatu utakuwa ndoto.

 Akaongeza kuwa kwa wajumbe  kupitisha ajenda  hiyo ya mpango wa utekelezaji kuhusu ufadhili wa maendeleo ambao  pia umeainisha masuala  mengi muhimu yanayohusiana na  utekelezaji wa  malengo  mapya ya maendeleo endelevu ni moja ya hatua  muhimu   sana ya kuanzisha  mwongo   mpya  wa ushirikiano wa  kimataifa.

No comments: