Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linatarajia kutoa shilingi milioni 700 kwa Benki ya Posta Tanzania kama dhamana ya mikopo itakayotolewa na benki hiyo kwa wajasiriamali hapa nchni.
Mpango huu uko chini ya Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulioanzishwa mwaka 2008 ambao pamoja na majukumu mengine unatumika kutoa au kudhamini mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali nchini.
Fedha hizo zitawekwa katika akaunti maalum katika Benki ya Posta kama dhamana ya mikopo na benki hiyo itatumia fedha zake kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa makundi husika kwa kiwango cha mara tatu ya dhamana iliyowekwa na Baraza.
Mikopo itatolewa kwa riba ya asilimia 11 kwa mwaka.
“Tunaanza na Benki ya Posta na baadae nyingine zitakazofanya kazi na sisi, utekelezaji unaanza mara moja kwanza na kiwango hiki cha fedha ambacho kitaongezeka,” alisema.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa kutiliana saini hati ya makubaliano ba benki ya posta kudhamini mikopo kwa wajasiriamali kupitia SACCOS na vikundi vya VICOBA, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bi. Beng’i Issa alisema makubaliano hayo ni moja ya kukabiliana na tatizo kubwa la ajira nchini.
Mfuko huo unatumika kuhifadhi fedha zinazotolewa na serikali kila mwaka na unatumika kufidia mabenki yatakayopata hasara kwa kutoa mikopo iliyodhaminiwa na NEEC.
Alifafanua kwamba mpango huo unawalenga wanachama wa vyama vya SACCOS hasa za akina mama na za vijana wanaotoa huduma ya usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda na vikundi vya vikoba.
Alisema kuwa NEEC itashirikiana na benki hiyo pia kutoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali kama utunzaji wa kumbukumbu na mahesabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi, alisema, benki yake ni benki ya wananchi na hivyo unayo furaha kubwa kushirikiana na NEEC, ili kuwakwamua wananchi kiuchumi kwa kupata mikopo itakayowazsaidia kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
“Benki ya Posta inayo furaha kubwa kushirikiana na Baraza hili ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za kifedha kwa gharama nafuu kupitia mpango huu,” alifafanua Moshingi.
Hivi karibuni, NEEC ilifikia makubaliano na Cambridge Development Initiative (CDI) ya Chuo Kikuu cha Cambridge cha Uingereza ili kuimarisha mafunzo ya maswala ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini.
Takwimu zinaonyesha kwamba vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka ni kati ya 800,000 hadi 1,000,000 ambao wanapigania nafasi za ajira zisizozidi 60,000 katika sekta ya umma na nafasi takribani 300,000 katika sekta binafsi.
Ili kufaidika na mikopo hiyo, SACCO lazima iwe na kiwango cha marejesho ya mikopo kisichopungua asilimia 95 na pia kufuata taratibu zote za ushirika wa akiba na mikopo.
Sharti lingine ni mikopo yote kukatiwa bima na uzoefu wa SACCOS husika kusimamia mikopo kwa muda usiopungua miaka miwili.
No comments:
Post a Comment